Simba SC yaivutia kasi Wydad Casablanca michuano ya CAF

Na Badrudin Yahaya

TIMU ya Simba SC, imeanza mazoezi maalum kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca utakaopigwa nchini Morocco.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi ugenini ukiwa ni wa raundi ya nne hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Hadi sasa Simba inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi B ikiwa na alama 2 ikitanguliwa na Janweng Galaxy na Asec Mimosa zenye alama 4 kila moja huku Casablanca ikishika mkia ikiwa haina alama.

Akizungumza na mtandao wa Tanzania Leo, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kimerejea mazoezini kuhakikisha kinashinda mechi yao ijayo ugenini.

“Tumeanza mazoezi maalum kwa ajili ya kukabiliana na Wydad Casablanca ugenini, tunajua hautakuwa mchezo mwepesi ikizingatiwa wapinzani wetu hawana alama, hivyo tunajiandaa kwenda kufanya vizuri,” amesema Ally.

Amesema baada ya mapumziko ya siku kadhaa, kikosi kimerejea na morali ya hali ya juu kwa kila mchezaji kuonesha jinsi gani anaweza kuaminiwa na Kocha mpya, Mualgeria Abdelhak Benchikha.

Amesema kundi lao bado halijatoa mwelekeo wa moja kwa moja kuwa timu gani itafuzu hatua ya robo fainali na ndio maana wanaendelea kupambana kuvuna alama ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua hiyo.

Baada ya mchezo huo, Simba itakabiliana na kibarua kingine katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mchezo utakaopigwa Desemba 15 kabla ya kurudiana na Casablanca Desemba 19 jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *