Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Simba SC, imeanza kampeni yao ya kuwania Kombe la Mapinduzi kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKU katika mchezo wa Kundi B.
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha, alionekana kuuchukulia kwa uzito mchezo huo na alipanga idadi kubwa ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza.
Mshambuliaji raia wa Zambia, Moses Phiri alikuwa wa kwanza kufunga bao dakika ya 8 kipindi cha kwanza lakini JKU walisawazisha bao hilo kupitia kwa Neva Kaboma zikiwa zimesalia sekunde chache kabla ya mapumziko.
Simba walijipatia ushindi wao kipindi cha pili kwa kuongeza mabao mawili kupitia kwa Mohamed Hassan aliyejifunga na bao lingine likifungwa na Saleh Karabaka ambaye amesajiliwa leo akitokea JKU.
Kwa ushindi huo, Simba wanakwea hadi nafasi ya pili wakiwa na alama tatu huku Singida FG wakiwa kileleni na alama 6.
Mchezaji wa Simba, Che Malone Fondoh alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo na kukabidhiwa kitita cha sh. 500,000 na wadhamini wa tuzo hiyo Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Kabla ya mchezo huo, kulikuwa na mchezo mwengine wa kundi hilo uliofanyika mapema ambapo Singida FG waliifunga APR mabao 3-1.
Kesho michuano hiyo, itaendelea kwa michezo ya Kundi C ambapo Jamhuri itacheza na KVZ wakati mechi ya usiku, Yanga itacheza na Jamus ya Sudan Kusini.