Simba SC yaingia mkataba na Knauf wa mil. 200/-

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Soka ya Simba, imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Kampuni ya kuzalisha vifaa vya ujenzi ya Knauf kutoka Ujerumani wenye thamani ya sh. milioni 200.

Knauf inazalisha bidhaa zenye hadhi ya Ujerumani hapa Tanzania, ambazo ni jipsam bodi, jipsam plasta na nyinginezo nyingi.

Akizungumza wakati wa kuingia mkataba huo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kanda Afrika Mashariki ya Knauf, Ilse Boshoff, amesema uhusiano huo ni mkubwa ambao utakuwa na faida kwa pande zote mbili kitaifa na Kimataifa na ndicho kilichowavutia kuja kwao.

Boshoff amesema Knauf inatengeneza bidhaa bora za ujenzi na ilianza kufanya kazi nchini tangu mwaka 2015 na tayari imewekeza sh. bilioni 148.

“Tupo nchi zaidi ya 90 duniani na malengo yetu ni kuzidi kujitanua zaidi na matumaini yetu uhusiano huu na Simba utakuwa msaada kwetu kuendelea kujulikana zaidi tukiendelea kuzalisha bidhaa bora za ujenzi kutoka Ujerumani,” amesema Boshoff.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, amesema mkataba huo utakuza chapa ya Knauf pamoja na Simba pia, ambapo alisema hawakuangalia thamani yake bali umuhimu wa kuendelea kujitangaza kimataifa.

Mangungu akiwa na Boshoff, wakionesha nakala za mkataba

“Sisi kama Simba hatukuangalia zaidi thamani ya mkataba bali tumeangalia kujitangaza na kuvutia kampuni zingine ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza kwetu na tunawakaribisha,” amesema Mangungu.

Pia Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amewaomba Wanasimba kununua bidhaa kutoka kwa Knauf kwakuwa wamejiridhisha kuwa vifaa vyao ni bora na vinaendana na klabu yao.

“Mwanasimba yoyote anayetaka kujenga hasa akiwa kwenye hatua ya kumalizia ujenzi wake, Kampuni ya Knauf imekuja kwa ajili yake. Sisi tumejiridhisha kuwa Knauf inazalisha bidhaa bora kabla ya kukubali mkataba huu kwahiyo Wanasimba wote tunatakiwa kuiunga mkono,” amesema Ahmed.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *