Simba SC yaanza kuivutia kasi Al-Ahli Tripol

Na Badrudin Yahaya

KLABU ya Simba SC, imeendelea na maandalizi kuelekea mchezo wao wa kwanza wa michuano ya Shirikisho Afrika ambapo itacheza Septemba 15 ugenini dhidi ya Al-Ahli Tripol ya Libya.

Katika kipindi hiki cha mapumziko kupisha mechi za timu za taifa, mastaa wa Simba SC ambao hawakuitwa kwenye timu za taifa wapo jijini Dar es Salaam wakipiga tizi kali chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Akizungumza leo na Gazeti la mtandaoni la Tanzania Leo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema  wachezaji wote wapo kwenye programu ya kocha wakijiandaa na mchezo wa kwanza wa kimataifa msimu huu.

Kumbuka kuwa, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa ni wa kwanza kwao kwakuwa hawakushiriki hatua ya awali kama walivyofanya Tripol ambao walicheza dhidi ya Uhamiaji ya Zanzibar.

“Kikosi kamili kipo Dar es Salaam na tunaendelea na mazoezi makali kwaajili ya kujiweka sawa, kulikuwa na mapumziko ya siku mbili mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Al-Hilal lakini tayari tumerejea mazoezini,” amesema.

Aidha, Ally ameongeza kwa kusema Fadlu ameomba kupata mchezo mmoja wa kirafiki kwa ajili ya kuwajenga zaidi wachezaji wake na hivyo kuna uwezekano mwishoni mwa wiki hii wakacheza.

Katika hatua nyingine, nyota wa Simba, Fabrice Ngoma amejiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya kuendelea na maandalizi.

Mchezaji huyo mara ya mwisho alionekana uwanjani Agosti 11, wakati Simba walipocheza mechi ya kuwania mshindi watatu wa michuano ya Ngao ya Jamii dhidi ya Coastal Union.

Kwenye mchezo huo, Ngoma alipewa kadi nyekundu ambayo ilimlazimu kukosa mechi moja ya kwanza ya ligi lakini mchezaji huyo hakujumuishwa kwenye mechi iliyofuata dhidi ya Fountain Gate kitu ambacho kilizua maswali kutoka kwa wadau.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *