Simba SC, Singida FG kuumana nusu fainali Mapinduzi Cup

Na Badrudin Yahaya

STRAIKA Mkongo wa timu ya Simba SC, Jean Baleke, amefunga bao muhimu kwa upande wa timu yake na kuiwezesha kuibuka na ushindi wa 1-0 katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Mapinduzi Cup dhidi ya Jamhuri FC.

Ushindi huo, umewaifanya Simba kutinga hatua ya nusu fainali na kuungana na timu za Mlandege, APR na Singida FG katika hatua hiyo.

Katika mchezo huo, kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo na kukabidhiwa kitita cha shilingi 750,000.

Simba sasa itakabiliana na Singida FG katika mchezo wa nusu fainali ambao utachezwa Alhamisi.

Mchezo wa kwanza wa nusu fainali utachezwa Jumanne kati ya Mlandege dhidi ya APR.

Katika hatua nyingine, timu ya Simba, imetangaza kukamilisha usajili wa Winga, Ladack Chasambi kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Mchezaji huyo alipandishwa na Mtibwa Sugar msimu huu kutoka timu ya vijana na amefunga bao moja huku akitengeneza mengine mawili.

Chasambi ambaye mara kadhaa amejumuishwa kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ msimu huu, anaungana na nyota wengine wapya ambao walitambulishwa awali, Saleh Karabaka na Babacar Sarr chini ya Kocha, Abdelhak Benchikha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *