Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Simba Queens, imetwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga JKT Queens kwa jumla ya mikwaju ya penalti 5-4.
Mchezo huo wa fainali ya michuano hiyo, umefanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambapo ndani ya dakika 90 timu hizo zilitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1.
JKT Queens katika mchezo huo ndio walikuwa wa kwanza kuandika bao kupitia kwa mshambuliaji wao, Stumai Abdallah akiunganisha vyema mpira wa kona ndani ya eneo la hatari.
Hata hivyo bao hilo halikudumu kwani mchezaji wa Simba Queens, Danai Bhobho alisawazisha na kufanya mchezo huo kufika hadi mapumziko matokeo yakiwa 1-1.
Kipindi cha pili, kila timu ilijaribu kuongeza bao la ushindi lakini umakini katika idara ya ulinzi kwa pande zote ulifanya mchezo kuisha kwa matokeo ya 1-1 na ndipo Mwamuzi, Tatu Malogo alipoamuru kutafuta bingwa kwa mikwaju ya penalti.
Simba walikwamisha penalti zao zote 5 lakini kwa upande wa JKT Queens, mchezaji mmoja alikosa penalti yake na kuwapa ubingwa Simba Queens.
Kwa ushindi huo, Simba watalamba kiasi cha shilingi milioni 5 kutoka kwa mdhamini wa shindano hilo, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom huku JKT Queens wao wakiambulia sh. milioni 3.5.
Mshindi wa tatu, timu ya Yanga Princess wao watapata sh. milioni 1.5 na Fountain Gate mshindi wa nne watapata sh. milioni 1.
Kuisha kwa shindano hilo la Ngao ya Jamii ni kiashiria kuanza kwa Ligi ya Wanawake Tanzania Bara ambayo itatimua vumbi Jumamosi.