Serikali yazitaka taasisi za miradi ya Magadi Soda kushirikiana kutekeleza mradi

Na Mwandishi Wetu, Arusha

SERIKALI imewataka viongozi wa taasisi zinazohusika na Mradi wa Kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka wilayani Monduli jijini hapa, kushirikiana kwa karibu kukamilisha taratibu zote zinazohitajika ili mradi huo kutekelezwa kwa wakati.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza ajira, malighafi za viwandani, kukuza biashara na uchumi wa Taifa.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandubya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali walipotembelea mradi huo kwa lengo la kuona utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali zitakazowezesha kuanza kutekelezwa rasmi kwa mradi huo.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, alisema ziara ya makatibu hao katika kutembelea mradi huo ni ishara tosha kuwa serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuona kuwa mradi huo unaanza kutekelezwa mara moja.

Ziara hii imeshirikisha wizara tatu na jumla ya taasisi nne na itafanya kazi kwa kushirikiana na vijiji vinne katika kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mradi na kuanza kutekelezwa kwa mradi huu ni dhahiri kuwa utasaidia katika kuboresha maisha ya wakazi wa Engaruka na Taifa kwa ujumla, kuongeza mapato kwa serikali na serikali ipo tayari kuhakikisha utekelezaji wake unaanza mara moja”. alisema Dkt. Abdallah.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mahimbali, alisema kuanza kuchimbwa kwa madini ya magadi soda nchini kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika kuagiza madini hayo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi viwandani ambapo takwimu zinaonyesha kuwa serikali hutumia kiasi cha zaidi ya sh. bilioni 1 kwa mwaka kuagiza nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya malighafi hiyo viwandani.

Sisi kama wasimamizi wa sekta ya madini hapa nchini tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa magadi soda ni madini muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa viwanda vingi hapa nchini kwa kuwa yanatumika kama malighafi na tuna viwanda ambavyo tayari vinategemea malighafi hii muhimu” alifafanua Mahimbali.

Mahimbali aliwataka wakazi wa Engaruka na Watanzania kiujumla kuhakikisha wanachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza pale ambapo mradi huu utakapoanza kutekelezwa hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt Nicolaus Shombe, alisema NDC kama mwekezaji kwa niaba ya serikali tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kufanyika kwa upembuzi yakinifu pamoja na tathmini ya mazingira huku akiishukuru serikali namna inavyouchukulia mradi huo kwa uzito wa kipekee na nia ya dhati iliyonayo ya kutaka kutekelezwa kwa mradi huu.

Pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Happyness Laizer pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli, Muhsin Kassim, wamesema wapo tayari kupokea mradi huo huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamikia fursa zitakazotokana na utekelezwaji wa Mradi huo.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Engaruka, viongozi wa eneo hilo, wakiwemo Diwani na Mtendaji wa Kata ya Engaruka pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vya Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai, wameonesha kufurahishwa na hatua ya serikali kuamua kutekeleza mradi huo utawakaowaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika upatikanaji wa ajira, ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *