Serikali yatoa msimamo kuhusu uraia pacha

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa msimamo wake kuhusu masuala ya uraia pacha nchini baada ya hivi karibuni kuwa na mijadala mbalimbali ya uraia pacha.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Agnesta Kaiza Jana Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema kwamba sheria ya Tanzania hairuhusu uraia wa nchi nyingine kwa watu wazima bali kwa watoto chini ya miaka 18 tu.

“Uraia wa Tanzania unaoongozwa na Sheria ya Uraia sura ya 357 Toleo la mwaka 2002. Sheria hii inabainisha aina tatu tu za uraia wa Tanzania ambao ni Uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi pamoja na uraia wa tajirisi. Hivyo, kwa mujibu wa Sheria tajwa hapo juu, Serikali hairuhusu Uraia pacha kwa watu wazima isipokuwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 ambao wanakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine.” Alisema.

Mbunge Agnesta aliendelea kuhoji kama Sheria sio msahafu kwanini Serikali sasa isije na Muswada wa Sheria ya kuruhusu uraia pacha nchini ambapo Waziri Masauni alisema ni kweli Sheria hizi sio msahafu na kwamba Sheria zote zinatungwa kwa maslahi na matakwa ya watu hivyo Serikali bado haijajiridhisha kama Uraia pacha ni matakwa ya Watanzania walio wengi na kama Serikali ikijiridhisha basi haitaona shida kuja Muswada wa Sheria hiyo.

“Hata kwenye mchakato wa Katiba uliokwama ambao ulihusisha maoni ya wananchi mbalimbali, suala la uraia pacha halikuwa matakwa ya Watanzania walio wengi na ndio maana Serikali ilipendekeza hadhi maalum na sio Uraia pacha kwasababu halikuwa takwa la wananchi walio wengi.” Alisema Waziri Masauni.

Waziri Masauni aliongeza kuwa Serikali iko pamoja na Watanzania wote walio Nje na ndio maana kwasasa iko katika hatua za mwisho kabisa kuanzisha hadhi maalum ili kuwapa fursa mbalimbali kwa Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine.

One thought on “Serikali yatoa msimamo kuhusu uraia pacha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *