Serikali yaja na mpango wa kusimamia mandeleo ngazi ya kata

Na WMJJWM-Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeandaa mpango mkakati wa kusimamia maendeleo kuanzia katika ngazi ya Kata utakaoshirikisha wananchi kuwajengea uwezo wa kushiriki na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Ili kutekeleza hilo Serikali imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalam wa ngazi ya Kata ili waweze kusimamia utekelezaji wa mpango huo katika maeneo yao.

Akifungua mafunzo kwa wataalamu hao kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Oktoba 05, 2023 jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Wakili Amon Mpanju amesema mafunzo hayo yatasaidia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na kusimamia Maendeleo mwaka 2022/23 – 2025/26.

Wakili Mpanju amesema utekelezaji wa Mpango huu utaimarisha uwezo wa watendaji wa Serikali ngazi ya Msingi katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii kwa kutumia rasilimali zilizopo bila kuisubiri Serikali kutatua changamoto hizo.

Aidha amesema mafunzo kwa wataalamu hawa yataongeza uwezo wa jamii kusimamia na kuelezea manufaa ya miradi ngazi ya jamii na Kitaifa. Vilevile, utapanua wigo wa wananchi kuwasiliana na Serikali kuanzia ngazi ya kijiji/Mtaa hadi Taifa pamoja na kuongeza uwezo wa Wataalam kutumia TEHAMA na hatimaye kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

“Nimefahamishwa kwamba mafunzo haya yanafanyika kwa mara ya kwanza  kwa wataalam wa ngazi ya kata ikiwa ni sehemu ya Mpango huu umeandaliwa kwa ajili ya kuwezesha wananchi kuwa kitovu cha maendeleo ngazi ya jamii,” amesema Wakili Mpanju.

Ameyataja mambo mengine muhimu katika utekelezaji wa mpango huo ni kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwajibika ili kuwa na kazi zenye matokeo na tija na kufanya vikao vya kufuatilia utekelezaji wa Mpango.

Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema washiriki wa mafunzo hayo watakwenda kujifunza juu ya Mpango wa Taifa wa Kuhamasisha na Kusimamia Maendeleo, dhana ya uzalendo na  kujitegemea na kutumia jitihada ili kukamilisha miradi inayolenga kutatua changamoto zao na kujiletea maendeleo.

MWISHO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *