Serikali yaendelea kuimarisha viwanda na biashara huku mauzo Afrika yakipanda kwa asilimia 40

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali imejipanga kuimarisha uendelevu wa sekta ya viwanda na biashara nchini kupitia sera, sheria na mifumo rafiki inayochochea ukuaji wa uchumi shindani na jumuishi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari, Kapinga amesema mauzo ya bidhaa za Tanzania katika nchi za Afrika yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.94 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka 2023, hali inayoonesha mafanikio ya jitihada za Serikali katika kukuza biashara ya nje.

Ameeleza dhamira ya Serikali ni kuhakikisha sekta ya viwanda na biashara inakuwa mhimili mkuu wa mabadiliko ya kiuchumi kwa kuongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Aidha, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka mkazo katika viwanda na uzalishaji kama msingi wa maendeleo endelevu na uchumi shirikishi.

Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, maboresho ya sera na sheria yameanza kuzaa matunda, ambapo thamani ya mauzo ya nje ya bidhaa na huduma imeendelea kuongezeka, huku bidhaa za viwandani kama saruji, mabati na vioo zikianza kuuzwa kwa wingi katika masoko ya nje kutokana na uzalishaji mkubwa.

Ameongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka hadi asilimia 7.3 mwaka 2024, huku sekta ya biashara ikifikia asilimia 8.6, ishara ya kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Serikali pia imehuisha zaidi ya sheria na kanuni 13 zilizorahisisha taratibu za kuanzisha biashara, kupunguza gharama na muda wa kupata leseni, hatua iliyosababisha ongezeko la usajili wa makampuni na kuongezeka kwa idadi ya viwanda nchini, ikiwemo zaidi ya viwanda 2,000 vilivyoanzishwa Mkoa wa Pwani ndani ya miaka minne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *