
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetangaza hatua madhubuti za kisera na kisheria baada ya matokeo ya utafiti wa mwaka 2024 kuonesha kupungua kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na vijana nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametangaza kuwa serikali itafanya tathmini na maboresho ya Sera na Sheria zilizopo ili kuhakikisha ulinzi wa watoto na vijana unaimarika zaidi kwa kutumia ushahidi wa takwimu zilizokusanywa kutoka utafiti huo.
“Matokeo haya yameonyesha hatua nzuri, lakini yanafungua ukurasa mpya wa wajibu kwa Serikali na Wadau kufanya maboresho makubwa zaidi ya kisheria, kitaasisi na huduma zinazotolewa kwa manusura wa ukatili,” amesema Dkt. Gwajima wakati wa kutangaza matokeo hayo leo Juni 9, 2025 jijini Dar es Salaam.
Utafiti unaonesha kupungua kwa ukatili wa kingono kwa watoto wa kike kutoka asilimia 33 mwaka 2009 hadi asilimia 11 mwaka 2024, ukatili wa kimwili kutoka asilimia 76 hadi 24 na ukatili wa kihisia kutoka asilimia 25 hadi 22. Kwa watoto wa kiume, ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 21 hadi 5, kimwili kutoka asilimia 74 hadi 21 na kihisia kutoka asilimia 31 hadi 16.
Hata hivyo, Dkt. Gwajima amesema matokeo hayo yatatumika kufanyia mapitio afua zilizomo ndani ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II), kuongeza bajeti, na kuimarisha rasilimali watu katika sekta husika.
“Ninaomba kusisitiza kuwa, haya siyo tu mafanikio ya kupungua kwa ukatili, bali ni mwongozo wa hatua zinazofuata kwa Serikali na wadau ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya ukatili wa aina yoyote,” amesema.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dkt. Amina Msengwa, amesema utafiti huo umefanyika katika mikoa yote 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia sampuli wakilishi ya kitaifa, hivyo una uwezo wa kuongoza maamuzi na sera bora.
Dkt. Gwajima pia amesisitiza kuwa ukatili wa watoto na vijana ni suala la ukiukaji wa haki za binadamu, linalochangia matatizo ya afya ya akili, matumizi ya dawa za kulevya na hatari ya kupata magonjwa ya zinaa, na hivyo kupunguza fursa za kimaendeleo na kuongeza umaskini.
