Serengeti hifadhi bora Afrika mara 5 mfululizo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
HIFADHI ya Taifa ya Serengeti-Tanzania, imeshinda tuzo ya hifadhi bora barani Afrika mwaka 2023.
Ushindi huo ni wa tano mfululizo kwa hifadhi hiyo kutwaa tuzo kuanzia mwaka 2019 hadi sasa.
Kupitia akaunti yao ya X (twitter), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ilisema; “Ahsante wote walioshiriki kupiga kura na kuiwezesha Serengeti kutwaa tuzo hii kwa mara nyingine, tunatoa shukrani za dhati kutoka moyoni! Asante kwa wote waliopiga kura na kufanikisha ushindi huu.
“Kwa pamoja, tunasherehekea ushindi mzuri wa Serengeti mara tano katika Tuzo za Utalii za Dunia,” ilifafanua taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa tovuti ya World Travel Awards, hifadhi teule zilizowania tuzo hiyo mwaka 2023 ni pamoja na Hifadhi Kuu ya Wanyama ya Kalahari (Botswana).
Nyingine ni Hifadhi ya Kitaifa ya Etosha (Namibia), Hifadhi ya Taifa ya Bonde la Kidepo (Uganda), Hifadhi ya Kitaifa ya Kruger (Afrika Kusini) na Hifadhi ya Kitaifa ya Masai Mara (Kenya).
Hifadhi ya Serengeti ni maskani ya mamia ya wanyama wakiwemo nyumbu, pundamilia, pofu, simba, duma, fisi na swala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *