Samia: Watanzania tutunze mazingira

Na Mwandishi Wetu, Manyara

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Watanzania kutunza mazingira kwa zaidi ya asilimia 95 ya mabadiliko ya tabianchi yanatokana na shughuli za binadamu ambazo zinaathiri misimu ya mvua, kupotea kwa vyanzo vya maji.

Alisema serikali itafanya mapitio ya Sera, mitaala ya elimu katika ngazi zote ili kuwawezesha vijana nchini.

Lengo ni kuleta mageuzi makubwa ili elimu inayotolewa kwa viajana iakisi mazingira, mahitaji ya nchi na kuwawezesha wahitimu kujiajiri, kuajirika kiurahisi.

Rais Dkt. Samia aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Nyerere na Wiki ya Vijana kitaifa mkoani Manyara.

Aliongeza kuwa, dhamira ya Serikali ni kutengeneza vijana wenye mchango katika kukuza uchumi wa taifa ili kupunguza changamoto ya ajira.

“Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi 64 katika Wilaya mbalimbali nchini ili kuwapa vijana nafasi ya kutumia rasilimali zilizopo kujikwamua kiuchumi.

“Kama tutakuwa na vijana wazembe, wazururaji wasiowajibika utakuwa mzigo kwa taifa letu, tunataka tujenge taifa lenye vijana wachapakazi, wawajibikaji na wazalendo ili wachangie kikamilifu katika maendeleo yao wenyewe na taifa kwa ujumla,” alisema Rais Dkt. Samia.

Alisema baada ya ujenzi wa vyuo hivyo, Serikali itatengeneza vyuo vingine 50 ili kufikia lengo la kuwapa vijana ujuzi wa kuwa wajasirimali na kuingia katika kilimo, uvuvi na ufugaji.

Alieleza kuwa, serikali inaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha bei ya gesi inashuka, kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuacha matumizi ya mkaa ambao unaharibu ikolojia na una madhara kiafya.

Aliwataka wananchi hasa wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Pwani ya Bahari ya Hindi maeneo ya mabondeni, kuchukua tahadhari dhidi ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El Nino wakati wa msimu wa vuli.

Kupitia mbio za Mwenge mwaka huu, miradi 1,424 yenye thamani ya sh. trilioni 5.3 ilishughulikiwa katika halmashauri 195 nchini, kati ya hiyo miradi 7 yenye thamani ya sh. bilioni 1.9 ilibainika kuwa na dosari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *