Samia: Tumedharimia kupitia upya mifumo ya utoaji haki

Na Janeth Jovin, Dar es Salaam

VIONGOZI mbalimbali wa dini nchini kila mara wamekuwa wakiwataka watanzania kudumisha amani huku wakiitaka Serikali kusimamia utoaji haki kwa watu wote.

Hata hivyo Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inaboresha mifumo ya utoaji haki nchini.

Katika kuhakikisha adhma hiyo inatimia, Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassani amesema kuwa Serikali yake imejikita katika kupitia upya mifumo ya utoaji haki iliyopo ambayo imechangia kuvuruga mifumo ya haki jinai na kupuuza mifumo ya maadili na kusababisha baadhi ya wananchi wasio na uwezo kiuchumi kupoteza haki zao.

Akisoma hotuba katika mkutano wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) jijini Dar es Salaam, kwa niaba ya Rais Dkt. Samia, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, anasema kuwa serikali iliamua kuanzisha tume ya muda mfupi ya haki jinai ambayo imelenga kuboresha taasisi za haki jinai na kutoa fursa kwa wadau kuchangia maoni.

Dkt. Ackson anasema kuwa serikali inaendelea ujenzi wa Vituo Jumuishi vya utoaji wa haki, huku akibainisha kuwa wamewahimiza majaji na mahakimu kuharakisha usikilizaji wa mashauri ili kuongeza kasi ya utoaji haki nchini.

“Nimefurahi kusikia miongoni mwa malengo ya TAWLA ni kuwasaidia wanasheria kujiendeleza kitaalama ili kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya kisheria kwa ajili ya kupata haki zao,” anasema Dkt. Ackson kwa niaba ya Rais Samian a kuongeza.

“Mmekuwa mkitoa msaada wa kisheria, kuelimisha jamii kuhusu haki za kisheria kwa kutumia vyombo vya habari pamoja na kutetea haki za binadamu, ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya wanawake na nchi kwa ujumla.”

Aidha, anasema wanawake wanasheria nchini wanatakiwa kutumia taaluma yao vizuri katika kuhakikisha wanalinda na kutetea haki za wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya uhalilishaji na ukatili.

Anasema ni muhimu wanawake wa TAWLA kuendelee kushirikiana na Serikali katika kubainisha sheria ambazo zimekua zikikandamiza haki za wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum.

“Hiyo ni kwa sababu serikali haiwezi kutenda yote hayo peke yake isipokuwa kwa msaada wa taasisi mbalimbali kama TAWLA ambazo zinapaswa kuwa jicho la serikali na anaahidi kwamba tupo tayari kusikiliza na kujadiliana kwa kina ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

“Tuendelee kufanya kazi kwa mshikamano na kuwa na nia moja iliyothabiti, nimefurahi kusikia miongoni mwa malengo ya TAWLA ni kuwasaidia wanasheria kujiendeleza kitaalama ili kuwasaidia wanawake wenye matatizo ya kisheria kwa ajili ya kupata haki zao,” anasema Dkt. Ackson kwa niaba ya Rais Samia.

Anasema Serikali inayapa kipaumbele masuala ya wanawake  na usawa wa kijinsia na kuyatafutia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wanawake katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba wataendelea kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Hata hivyo, Dkt. Ackson alikuwa anamwakilisha Rais Dkt. Samia katika mkutano huo, anasema kuwa TAWLA wamekuwa wakitoa huduma katika mikoa sita nchini jambo ambalo la kupongezwa kwani inaonesha nia ya dhati pamoja na kuhakikisha wanawafikia wanawake wa mikoa ya mbali ili wapate msaada wa kisheria.

Anasema wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwa serikali ikiwemo ushiriki wao katika kutunga sheria ya mtoto namba 21 mwaka 2009 ambayo inalinda haki na usawa wa watoto.

“Mmeshiriki katika mchakato wa kupata Katiba mpya kwa kuhakikisha katiba inayoandiwa inalinda haki za kijinsia, hivyo kila kiongozi na mwanachama wa TAWLA ni muhimu kufanya juhudi za kutafuta na kufikia usawa kijinsia pamoja uwezeshaji kwa wanawake,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa TAWLA, Lulu Ng’wanakilala, anasema kwa kipindi cha miaka 33 chama hicho kimeweza kuwatumia mawakili wake zaidi ya 400 kwa kuwasaidia wanawake mahakamani ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za mawakili.

Ng’wanakilala anasema kuwa lengo ni kutoa huduma kila mkoa hivyo ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Dkt. Samia kuwapa maeneo ya kujenga Ofisi ili waweze kuwafikia wanawake wenye uhitaji wa msaada wa kisheria.

“Tumeweza kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake milioni 12 kupitia Ofisi zetu zilizopo Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza na Dodoma,” anasema Ng’wanakilala.

Anasema ili kuwafikia watu wengi wamezindua huduma ya kutoa msaada wa kisheria kwa njia ya simu bila malipo pamoja na kuandaa mafunzo na machapisho kupitia vyombo vya habari na kufanikiwa kuwafikia watu milioni 17.

Aidha, anasema wamekuwa mstari wa mbele katika kutetea mabadiliko ya sheria mbalimbali kandamizi na kuhamasisha kutungwa kwa sheria zinazowalinda wanawake na watoto na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Pia alibainisha kuwa Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kujifunza mbinu bora kuhusu usawa wa kijinsia, kuzingatia usawa ili kuongeza upatikanaji wa haki kwa wanawake’.

Kila mwaka mwezi Mei TAWLA wanakuwa na mkutano mkuu ambao unatanguliwa na mafunzo ya sheria ambayo yana lengo la kuwasaidia wanawake kukua kitaaluma.

Kupitia mkutano mkuu baadhi ya wanawake wamepata Tuzo ya Wanawake Wanasheria Vinara kwa wanawake ambao wamekuwa chachu ya kuleta maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *