Na Daniel Mbega, Kisarawe
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshinda katika kigezo cha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi endelevu unaoendana na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).
Na ameyafanya hayo si kwa bahati mbaya, bali kwa kuzingatia ushirikiano wa kidiplomasia katika kuyafikia malengo husika, kama lilivyo Lengo Namba 17 la Maendeleo Endelevu.
Ni juzi tu alikuwa na ugeni mkubwa wa Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Dkt. Frank Walter Steinmeier, ambaye aliongozana na wafanyabiashara wakubwa takriban 12 ambao walishiriki Jukwaa la Biashara baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na Ujerumani mnamo Oktoba 31, 2023 jijini Dar es Salaam.
Ujio wa Dkt. Steinmeier siyo wa bahati mbaya, bali unakwenda sambamba na mikakati ya Serikali ya Rais Samia, ambaye siyo tu kwamba ameifungua Tanzania katika diplomasia ya kimataifa, bali analenga kuhakikisha kwamba diplomasia ya uchumi, tena shirikishi, inatamalaki.
Wale ambao wana kawaida ya kubeza kila jambo linalofanywa na Serikali, yaani ‘Wagomvi Waandamizi’, wameshikwa na butwaa kwa kasi anayokwenda nayo Rais Samia.
Yawezekana hawajui kusoma, lakini wanaweza kuona kwa macho namna mambo yanavyokwenda.
Ndiyo maana ninasema, kwa mafanikio anayokwenda nayo Rais Samia, kamwe asitokee mtu ‘akapiga ngoma za vita’, kwa sababu atakuwa anatuyumbisha.
Zamani zile ngoma za vita zilipigwa pale kulipokuwa na dharura, wakati mwingine walitumia mpaka baragumu kama ishara ya watu kukusanyika na kujiandaa.
Leo hii wapo wanaopiga ‘ngoma za vita’ kwa kutumia mitandao ya kijamii, wakibeza kila jambo jema linalofanywa na Serikali. Hawa tusiwape nafasi kwa sababu tunaona namna Tanzania inavyopasua anga kimataifa.
Kupitia ushirikiano wa kidiplomasia ndipo nchi inaweza kutekeleza hata Lengo Namba 9 la kuwa na taifa la Viwanda, Ubunifu na Miundombinu kwa kujenga miundombinu yenye kustahimili changamoto, kukuza viwanda endelevu na kuendeleza ubunifu.
Lakini kwa kuimarisha mbinu za utekelezaji na kuhuisha ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu, pia Rais Samia anatekeleza Lengo Namba 1 la Kutokomeza Umasikini kwa kukomesha aina zote za umasikini kila mahali, kwani wananchi wanapowezeshwa kiuchumi, hata matabaka ya kipato nayo yanapungua.
Ujerumani ni nchi ambayo imekuwa na ushirikiano na Tanzania kwa miaka mingi, ukiachilia mbali kwamba ndilo lilikuwa koloni la kwanza katika iliyokuwa Dola ya Ujerumani ya Afrika Mashariki (German East Africa) ikihusisha pia mataifa ya sasa ya Rwanda na Burundi, na imewekeza miradi mingi hapa nchini, kikiwemo Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill kinachozalisha saruji ya Twiga.
Na ziara ya Rais Steinmeier siyo tu ya kihistoria, bali imefungua fursa nyingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi.
“Tunakuhakikishia sisi watu wa Ujerumani tunaendelea kuwa mshirika wa Tanzania kwa karibu. Hatupo hapa kwa ajili ya kujenga mahusiano lakini tupo hapa kuahidi tutaendelea kuwekeza katika ukanda huu, nimefurahishwa na moyo wako wa kuendelea kudumisha uhusiano huu na kuufanya uwe mzuri zaidi hata kwa ajili ya kesho yetu,” alisema Rais Steinmeier alipokutana na Rais Samia katika Ikulu ya Dar es Salaam Novemba 31, 2023.
Suala la uwekezaji, rasilimali, kilimo, afya na nishati mbadala ambayo ni sekta muhimu ni mambo ambayo yamepewa kipaumbele na Rais huyo wa Ujerumani na akaahidi kutoa ushirikiano kwa faida ya mataifa yote mwawili.
“Kule Ujerumani tupo katika nmchakato wa kubadili na kuangalia namna gani ya kuendana na mabadiliko ya tabia nchi ili tufikie lengo la kupunguza matumizi makubwa ya kaboni katika masuala ya nishati,” alisema.
Akaeleza kuwa, watashirikiana katika sekta ya nishati kwa kubadilishana uwezo, ziara hiyo italeta matunda katika masuala ya kiuchumi na sekta zingine mbalimbali.
“Nina uhakika tutaendelea kusimama na kutumia zaidi fursa zilizopo kutokana na mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili, katika safari mbili nilizokuja Tanzania nimejifunza mengi, natamani kukutana na wabunifu ambao ni vijana wa Kitanzania.
“Nimefurahishwa sana, tutaweza kusimama na wabunifu vijana katika hili, suala la ushirika wa kiuchumi na namna gani ya kutoa mitaji zaidi itakayowasaidia katika uzoefu ili kuwa na watu wenye maarifa katika masuala ya kidigitali,” alisema.
Pia wamekubaliana kufanya utafiti kwa mambo yaliyotokea enzi za ukoloni, kuanzisha ukurasa mpya na walioathiriwa na Vita vya Maji Maji, kukutana na wahanga na kuzungumza nao kwa kuwa walipitia kipindi kigumu.
“Yote ambayo watanieleza nitakwenda kuyawasilisha Ujerumani, kuangalia namna gani ya kurudisha mabaki ya watu yaliyopo Ujerumani,” aliongeza.
Ujerumani na Tanzania zimekuwa zikishirikiana katika sekta ya afya, elimu, usambazaji wa maji safi na salama, hifadhi ya mazingira, ulinzi na usalama, haki za binadamu na utawala bora na hifadhi ya maliasili.
Na kuna takriban miradi 100 ya Ujerumani katika ngazi mbalimbali imewekezwa Tanzania.
Ni ukweli ulio wazi kwamba, ziara hii ni ishara ya diplomasia ya uchumi kukua kwani huo ni muendelezo wa viongozi mbalimbali kuja hapa nchini kwa ajili ya kuimarisha uhusiano.
Taarifa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na TIC, zinaeleza kwamba, Tanzania imekuwa ikiiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka.
Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni Kahawa, Tumbaku, Pamba, Asali, Samaki, Nta na vito vya thamani.
Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi), Magari, Vifaa na Mashine za Umeme.
Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini.
Kwa mujibu wa TIC hadi Agosti 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani 408.11 milioni ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira 16,121.
Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imesajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani 300 milioni iliyozalisha ajira 905.
Si kiongozi wa kwanza
Rais Steinmeier si kiongozi wa kwanza kuzuru nchini wakati huu wa utawala wa Rais Samia, kwani tunakumbuka Rais Evariste Ndahishimiye wa Burundi alikuja nchini Oktoba 23, 2021, takriban miezi saba baada ya Rais Samia kuingia madarakani.
Na katika ziara hiyo tulishuhudia uwepo wa uwekezaji mkubwa wa Burundi kutokana na kiwanda kikubwa cha mbolea mkoani Dodoma, bila kusahau kwamba, Burundi ni miongoni mwa nchi zinazoitegemea Bandari ya Dar es Salaam kusafirishia shehena zake.
Mnamo Machi 29, 2023, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris alizuru Tanzania kwa ziara yake ya siku 3, ambayo kimsingi ilifungua milango mingi ya fursa za maendeleo kijamii na kiuchumi.
Hii ilikuwa ziara muhimu hasa kwa Tanzania ambayo inaendelea kupambana kujenga uchumi imara zaidi na kupambana na umaskini hasa kwa kuzingatia Tanzania ni moja ya mataifa yenye fursa nyingi za uwekezaji na biashara duniani.
Tunazo fursa nyingi za uwekezaji kwenye gesi asilia kule Mtwara, madini, bahari, ardhi, eneo zima la utalii kupitia mbuga zetu za wanyama, uvuvi, masuala ya vijana na mengine mengi.
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kinasema kwamba Marekani ni moja ya mataifa yaliyo kwenye tano bora kwa uwekezaji mkubwa nchini ambapo mpaka sasa imewekeza kwenye miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10 iliyotoa ajira zaidi ya 50,000 kwa Watanzania.
Jirani yetu mwingine, Rais Paul Kagame wa Rwanda, naye alizuru nchini Aprili 27, 2023 kwa ziara ya siku mbili, ambapo mataifa hayo mawili yanategemeana kiuchumi kutokana na Rwanda pia kuitegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa kusafirisha mizigo yake kutoka na kwenda ng’ambo. Hadi mwaka 2021 Rwanda ilikuwa ikisafirisha tani milioni 1.366 kupitia bandari hiyo.
Moja ya malengo ya ziara ya Rais Kagame yalikuwa kuimarisha ushirikiano kupitia bandari hiyo ambayo imekuwa ikifanyiwa maboresho ili kukidhi mahitaji ya nchi jirani zinazoitegemea, na kwa sasa tayari Tanzania na DP World zimeingia makubaliano ya uwekezaji ili kuleta ufanisi.
Mnamo Julai 17, Rais wa Hungary, Katalin Novak, alifanya ziara ya siku nne nchini katika jitihada za Rais Samia kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.
Masuala ya uwekezaji katika kilimo, utangazaji na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali yalijadiliwa kwa kina na Hungary ikaahidi kuwekeza nchini katika sekta hizo.
Mabasi ya Ikarus, ambayo yalitamba sana miaka ya 1970 na 1980, yalikuwa yakitengenezwa nchini Hungary, na katika kipindi hicho wakati nchi hizo zinaendelea kuipambania siasa ya ujamaa na kujitegemea, ushirikiano ulikuwa wa kiwango cha juu.
Ziara za nje
Katika kuhakikisha anakuza diplomasia ya uchumi, Rais Samia amefanya ziara nyingi nje ya nchi, na mojawapo ni ya Oktoba 23 hadi 25, 2023 wakati alipozuru nchini Zambia na kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa taifa hilo pamoja na kulihutubia Bunge la Zambia, akiwa kiongozi wa nne wa kigeni kupewa heshima hiyo.
Ziara hiyo ilikuwa na umuhimu mkubwa kiuchumi kwa mataifa yote mawili kwa sababu ililenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu.
Katika ziara hiyo Rais Samia na mwenyeji wake walijadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la Tazama, Reli ya Tazara na Barabara ya TanZam.
Mwenendo wa ukuaji wa biashara baina ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022, yaani baada ya miaka sita.
Nchi hizo mbili zimelenga kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.
Hili la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam linabeba dhima kubwa ya ziara ya Rais Samia nchini Zambia, ambayo imekuja takriban siku moja tu baada ya kusainiwa kwa mikataba mitatu Oktoba 22, 2023 baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai kwa ajili ya uendeshaji wa sehemu ya Bandari hiyo.
Zambia ni miongoni mwa mataifa matano yasiyo na bandari (landlocked countries) ambayo yanaitegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo yao. Nchi nyingine ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Malawi na Rwanda.
Ziara hiyo ya Zambia ilifanyika takriban wiki mbili baada ya Rais Samia kuzuru Qatar na baaye India, ambako aliandamana na wafanyabiashara wengi wa Tanzania na kwa hakika fursa nyingi za uchumi zitapatikana.
Rais Samia alikwishazuru sehemu mbalimbali, Marekani, Ufaransa na China, ambako alikwenda Novemba 3, 2022 na kukutana na Rais Xi Jingping.
China’s investment in Tanzania reaches $1.8 billion after 10 years
CHINEDU OKAFOR
March 26, 2023 9:10 AM
President of Tanzania Samia Suluhu Hassan and President of China, President Xi Xinping
President of Tanzania Samia Suluhu Hassan and President of China, President Xi Xinping
Since President Xi Jinping’s visit to Tanzania 10 years ago, China’s investment in Tanzania has hit $1.8 billion.
This was announced during a conference commemorating President Xi Jinping’s visit to Tanzania.
Uwekezaji wa China nchini Tanzania ni mara 2.5 kulinganisha na ule wa mwaka 2012. Katika miaka 10 kufuatia ziara ya Rais Xi Jingping nchini Tanzania, China imewekeza katika miradi mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.8.
Uwekezaji huo ni wa miradi 1,908 yenye thmani ya Dola bilioni 1.6 kwa Tanzania Bara na miradi 15 yenye thamani ya Dola milioni 220 upande wa Zanzibar.
Ni ukweli usiopingika kwamba, China ndiye mwekezaji kinara nchini Tanzania ambapo kwa mwaka 2022, ujazo wa biashara kwa nchi hizo mbili uliongezeka kwa asilimia 23.7 mwaka hadi mwaka na kufikia Dola za Marekani bilioni 83.1, kiasi ambacho ni mara 35 ya kile cha mwaka 2012.
Haya yote yanafanyika bila kutaja makongamano kadhaa yaliyowakutanisha viongozi wa mataifa ya Afrika, kama Kongamano la Kilimo na Chakula la Afrika (Afro World Agri Food Conference, Exhibition and Awards) lililofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 10 – 12 Agosti, 2023 Diamond Jubilee, Dar es Salaam, na Kongamano la 13 la Mifumo ya Chakula frika (AGRF) lililofanyika jijini Dar es Salaam pia kati ya Septemba 5 na 9, 2023.
Kwa kuzingatia haya machache, hakika Rais Samia ameshinda katika diplomasia ya uchumi na anastahili kuungwa mkono na mpenda maendeleo yeyote.
Kijijini Msanga-Ngongele,
Kisarawe
+255 629 299688