Samia na Diplomasia ya Uchumi iliyoakisiwa na ziara ya Rais wa Romania

  • Yazalisha fursa lukuki katika ushirikiano masuala ya kimkakati

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

“ZIARA ya Rais wa Romania, Mheshimiwa Klaus Iohannis ni ya kihistoria na ya kwanza kwa kiongozi wa juu wa Taifa hilo kutembelea nchini Tanzania na imesaidia kuimarisha ushirikiano katika maeneno ya kimkakati.”

Haya ni baadhi ya maneno yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Novemba 17, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kikao chake na Rais Iohannis wa Romania kuhusu masuala waliyokubaliana na mgeni wake huyo.

Rais Iohannis alifanya ziara ya kwanza kabisa nchini Tanzania kwa kiongozi wa juu wa Serikali ya Romania, ambapo ziara hiyo ilikuwa ya siku nne kuanzia Novemba 16-19, 2023, ambayo ilikuwa ni mwaliko wa Rais Samia.

Dkt. Samia akaeleza kuwa, katika mazungumzo na mgeni wake walikubaliana kuwa mataifa yao yataimarisha ushirikiano katika sekta za afya, hususan utengenezaji wa dawa, usindikaji wa mazao ya kilimo, madini pamoja na mbinu za kukabiliana na majanga.

Maeneo mengine ya ushirikiano ambayo viongozi hao wamedhamiria kuyapa kipaumbele ni ufadhili wa masomo ambapo Romania itatoa nafasi 10 kwa ajili ya Watanzania kusoma masomo ya udaktari na ufamasia katika mwaka huu wa masomo.

Lakini Tanzania nayo ikatoa nafasi tano za masomo kwa wanafunzi wa Romania kuja kusoma nchini katika vyuo watakavyochagua wenyewe.

Rais Samia akaongeza kuwa, nchi hizo zimedhamiria kukuza kiwango cha biashara na uwekezaji ambacho kwa sasa hakiridhishi licha ya nchi zao kuwa na fursa lukuki za uwekezaji.

Viongozi hao pia waliokubaliana kushirikiana katika masuala ya kimataifa na hasa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo itajadiliwa kwa kina katika mkutano wa COP28 uliopangwa kufanyika Umoja wa Falme za Kiarabu mwishoni mwa Novemba 2023.

Naye Rais wa Romania, Klaus Iohannis akasema Romania imekuwa na ushirikiano mzuri na imara wakati wote, na lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kuimarisha zaidi uhusiano baina ya mataifa hayo.

“Tumekuwa na uhusiano mzuri na imara wakati wote, na katika kuendelea kuimarisha uhusiano wetu tumekubaliana kuimarisha uhusianio wetu kwenye maeneo ya kimkakati na Tanzania katika sekta za kilimo, ulinzi wa raia, ulinzi wa kimtandao, teknolojia na uchumi.

“Kusainiwa na hati hizi mbili za makubaliano ya ushirikiano ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wetu,” akaongeza Rais Iohannis.

Rais Iohannis hakuishia Tanzania Bara tu, bali alizuru Zanzibar Novemba 18, 2023 ambapo alikutana na kuzungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Rais Mwinyi alizikaribisha kampuni za Romania kuwekeza Zanzibar katika sekta za Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akasema, ziara ya Rais Iohannis ni heshima kubwa kwa Zanzibar na imedhihirisha kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa mbali kijiografia lakini zinaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Na Rais Iohannis akaeleza kufurahishwa kwake na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na Zanzibar ili kufanikisha utekelezaji wa Dira hiyo.

Akasema ziara yake ni moja ya jitihada za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Romania na Tanzania ambao mwezi Mei 2024 utafikisha miaka 60 tangu ulipoanzishwa mwaka 1964.

Fursa lukuki

Ziara ya Rais Iohannis imebeba fursa nyingi, si kwa Tanzania pekee, bali hata kwa Romania, kwa sababu zote zitanufaika.

Kubwa zaidi ambalo Watanzania wanaliona katika ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ni fursa ya kukuza uzalishaji katika sekta ya kilimo iwapo makubaliano yaliyofikiwa baina ya mataifa hayo yatatekelezwa kikamilifu.

Romania imekubali kuisaidia Tanzania katika usindikizaji wa mazao ya kilimo. Hii ikiwa na maana kwamba, Tanzania itanufaika na teknolojia za kisasa za kusindika mzao hayo ya kilimo na kuuza bidhaa nje badala ya malighafi, na kwa kufanya hivyo maana yake ni kwamba kutakuwa na tija kubwa kiuchumi.

Hiyo pia itasaidia kuongeza mapato ya fedha za kigeni iwapo bidhaa hizo zitauzwa nje ya nchi, na hasa zitakapokuwa zimesindikwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa kimataifa.

Sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na mara kwa mara Rais Samia amekuwa akihimiza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwenye sekta hiyo, kwani Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuzalisha chakula cha kutosheleza kulisha Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.

Ushirikiano wa Tanzania na Romania ambao umeongelewa unaanzia katika uhusiano wa kukuza taaluma, vyuo na wataalamu, kwa sababu wengi wamekuwa wakija mara nyingi wanakwenda moja kwa moja kwenye mazao, tofauti na taaluma ambayo ndiyo itasaidia kukuza kilimo.

Hati hizo mbili zilizosainiwa Novemba 17, 2023 jijini Dar es Salaam zinahusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi Kisayansi na Kiufundi katika sekta ya kilimo na mazingira pamoja na utiaji saini kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania kwa ajili ya kushirikiana katika kukabiliana na maafa na misaada ya kimataifa ya kibinadamu.

Kwa maana hiyo, Watanzania wanategemea kuona namna ambavyo wanaweza kunufaika na teknolojia, ujuzi pamoja na mbinu mbalimbali za kuongeza tija kwenye kilimo kutoka Romania kwa sababu ni nchi ambayo tumekuwa na uhusiano nayo kwa muda mrefu, hivyo ni wakati muhimu sana ambapo tunaweza kubadilishana uzoefu na kuongeza tija kwenye kilimo chetu.

Kutokana na athari za mazingira zinazoendelea kujitokeza duniani, Watanzania wanatarajia kuona tafiti mbalimbali zikifanyika na vyuo vilivyoingia makubaliano ili kukabiliana na changamoto zitokanazo na athari za mazingira.

Dunia inapitia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi hivyo wengi wanategemea kuona tafiti mbalimbali zikifanyika na nchi hizi mbili kupitia taasisi zake mbalimbali ikiwemo vyuo vikuu, Chuo Kikuu cha Sokoine kikiwa miongoni mwa taasisi hizo na vyuo vingine vipate nafasi ya kuhusishwa katika tafiti hizo ili kuhakikisha Tanzania inaweza kuongeza tija ya uzalishaji pamoja na usalama wa chakula.

Kwa ujumla, ziara ya Rais Iohannis inatazamwa kama tumaini jipya la kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Romania ambao ulipungua katika miaka ya karibuni.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaeleza kushuka kwa mauzo ya Tanzania katika taifa hilo kwa karibu mara mbili mwaka 2021 na 2022.

Kulingana na taarifa hiyo, mwaka 2021 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 7.9 milioni (takribani Shs. 19.7 bilioni) ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo iliuza Dola za Marekani 4.06 milioni (takribani Shs. 10.14 bilioni).

Manunuzi ya Romania kwa bidhaa za Tanzania yalipungua pia, ikinunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 11.6 milioni (takribani Shs. 28.97 bilioni) huku mwaka 2022 ikinunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani 2.4 milioni (takribani Shs. 5.9 bilioni).

Ziara hii ya Iohannis ni ukurasa mpya wa kuimarika kwa ushirikiano wa nchi hizo ulioanza mwaka 1964 katika sekta za afya na elimu.

Maeneo mapya ya ushirikiano yanatarajiwa kupatikana katika uwekezaji, elimu, utalii, afya na utamaduni.

Inaelezwa kwamba, kwa sasa uhusiano wa Tanzania na Romania unahusisha uwekezaji na biashara ya minofu ya samaki aina ya sangara, chai, tumbaku na parachichi.

Tanzania nayo inanunua bidhaa za mashine za umeme, vifaa vya matrekta, magari na vifaa vya matibabu kutoka Romania.

Lakini siyo biashara pekee, hata uwekezaji na sekta ya utalii inatarajiwa kuimarika kutokana na ziara hiyo, kwani kwa sasa Romania imewekeza nchini katika miradi ya usafirishaji, viwanda na utalii yenye thamani ya Dola za Marekani 6.04 milioni na kuzalisha ajira 89. Kwa sasa watalii kutoka Romania wameongezeka kutoka 6,418 mwaka 2018 hadi 12,148 mwaka 2022.

Kwa upande wa Zanzibar, imewekeza miradi mitatu yenye thamani ya Dola za Marekani 7.5 milioni kwa mwaka huu na kuzalisha ajira 64.

Samia na Diplomasia ya Uchumi

Anachokifanya Rais Samia kwa kuwaalika viongozi wa mataifa yaliyoendelea kuzuru nchini ni utekelezaji wa takwa la Umoja wa Mataifa kuhusu Ushirikiano katika Kufanikisha Malengo kwa dhamira ya kuimarisha mbinu za utekelezaji na kuhuisha ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu, mbalo ni Lengo Namba 17 la Umoja wa Mataifa miongoni mwa malengo 17 (SDGs) yaliyopitishwa Septemba 25, 2015.

Wakati wakuu wa nchi 193 walipokutana kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Septemba 25, 2015 ili kupitisha malengo hayo waliazimia mataifa yote yachukue jukumu la utekelezaji katika mpango kabambe wa miaka 15 baada ya kukamilika kwa miaka 15 ya awali (2000-2015) iliyokuwa na Malengo 7 ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).

Licha ya kwamba Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia yalipitishwa 2015, lakini kwa kipindi cha takriban miaka mitano iliyofuata, Lengo la 17 halikuweza kutekelezwa ipasavyo hadi Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

Na kwa sasa Rais Samia analitekeleza lengo hili kwa vitendo baada ya kubonyesha kitufe na kuirudisha Tanzania katika uga wa diplomasia ya kimataifa kama ilivyokuwa awali.

Lakini kadiri anavyotekeleza Lengo hilo Namba 17, ndivyo anavyoendelea kutekeleza mojawapo ya vipaumbele vikuu vya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 kwa Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi, ambavyo pia vimo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

Utekelezaji wa kipaumbele hiki ni mojawapo ya chachu zilizochechemua uchumi wa Tanzania ambao, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya mwezi Septemba 2023 inayosema ‘Tanzania Economic Update 2023’, umeendelea kuhimili vyema athari za Uviko-19 na changamoto zingine za dunia zilizojitokeza katika miaka mitatu iliyopita.

Kulingana na taarifa hiyo ya Benki ya Dunia, pamoja na changamoto zilizojitokeza, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na sababu kuu tatu, mojawapo ikiwa ni kuchochea na kuimarisha ushindani katika uchumi kwa muktadha wa kipaumbele cha Uchumi Shindani na Shirikishi.

Sababu ya pili ni kuendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuendelea kuaminiwa na taasisi za fedha duniani, pamoja na wadau wa maendeleo.

Mafanikio hayo yote ni jitihada za makusudi zinazofanywa na Serikali ya Samia, ambayo inaendelea kukua diplomasia ya uchumi na kujenga mazingira bora na wezeshi ya biashara na uwekezaji, ambayo yanaleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Na kimsingi, ziara ya Rais Iohannis wa Romania ni mfululizo wa viongozi kadhaa wa mataifa ya kigeni waliozuru nchini, ambapo ziara hiyo imekuja takriban wiki mbili tangu Rais wa Ujerumani, Dkt. Frank Walter Steinmeier, alipofanya ziara ya sikuta tatu nchini.

Ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris na Rais wa Hungary Katalin Novák ni muendelezo wa jitihada za Rais Samia kuimarisha diplomasia ya uchumi, kwani viongozi hao hawaji kutalii, bali wanakuja kutazama fursa za kuzikumbatia, jambo ambalo ni tija kwa Taifa.

Itakumbukwa pia kwamba, kati ya Juni 22-24, 2021, Naibu Waziri wa Poland, Paweł Jabłoński, alizuru nchini Tanzania, ziara ambayo ilikuwa na tija baina ya nchi zote mbili na matarajio ya kuimarishwa katika nyanja zote mbili za kisiasa na kiuchumi, zilikuwa ni mada husika.

Hungary, Poland na Romania ni nchi zilizokuwa zikifuata siasa ya Ujamaa na Ukomunisti na ndiyo maana hata uhusiano wao na Tanzania umeanza miaka mingi baada ya Uhuru wa Tanganyika, ingawa zenyewe ziliachana n sisa hiyo kati ya Oktoba 23, 1989 (Hungary) na Desemba 30, 1989 (Poland na Romania).

Kimsingi, Poland inaichukulia Tanzania kuwa washirika wa msingi katika Bara la Afrika, kwani ni miongoni mwa nchi nne za kipaumble Kusini mwa Jangwa la Sahara kama sehemu ya ushirikiano katika maendeleo.

Naibu Waziri Jabłoński pia alitembelea Wakala wa Mafunzo ya Ufugaji (LITA) Tengeru, yanayowezeshwa na Poland kwa zaidi ya miaka 10 kwa kuongeza weredi wa watendaji kuelimisha wataalam wa afya ya mifugo, kuboresha miundombinu na vitendea kazi na vifaa vya kisasa vya maabara.

Ziara hiyo pia ilijumuisha kituo cha shirika la APOPO kilichopo Morogoro, kinachohusika na upimaji na utambuzi wa maambukizi ya kifua kikuu na panya wakubwa wa kusini waliochomwa. Shukrani kwa msaada wa Poland, programu ya utambuzi wa kifua kikuu ilienea na kujumuisha baadhi ya hospitali katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.

Makamu kiongozi wa diplomasia wa Poland, pia alitembelea kwenye makaburi ya Wapoland Tengeru (eneo lenye makaburi mengi zaidi katika Tanzania ya raia walioenda uhamishoni wakisindikiza jeshi la Generali Anders), pia alikutana na jamii ya Wapoland na Wamishonari wanaofanya kazi Tanzania.

Kwa ujumla, fursa za ziara hizi ni nyingi na zinaonyesha namna Rais Samia alivyodhamiria kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuwashirikisha wawekezaji wa mataifa mengine,huku pia akitafuta fursa za kuwapatia ujuzi watalaamu wa Kitanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *