Samia: Mahakama tumieni teknolojia

  • Asema teknolojia itasadia kuharakisha usikilizaji wa kesi SADC
  • Aeleza Tanzania ilivyonufaika wakati wa janga la Uviko-19

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka Mahakama kutoka nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia teknolojia za kisasa katika kusikiliza kesi na kutatua migogoro mbalimbali ya kibiashara inayojitokeza barani Afrika.

Aliyasema hayo jana, Oktoba 23, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), uliofanyika jijini Arusha.

Mkutano huo umehusisha Majaji Wakuu wa nchi wanachama wa jukwaa hilo ikiwemo Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji, Seychelles, Bostwana, Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho , Mauritius, Zambia, Afrika Kusini na wenyeji Tanzania.

Alisema, ni lazima nchi hizo zijipange kusuluhisha migogoro inayoibuka sasa, ambayo mingi inachagizwa na ukuaji wa ubunifu wa teknolojia.

Rais Samia alisema, majaji hao wanapaswa kuzijengea uwezo mahakama katika nchi zao ili ziwe na uwezo wa kutatua migogoro kwenye eneo huru la biashara barani Afrika.

Alibainisha kwamba, Tanzania ilitumia teknolojia ya kisasa kutatua changamoto wakati wa Uviko-19 ikiwemo kutumia teknolojia kuendesha kesi mbalimbali za kimahakama kwa njia ya mtandao bila watu kwenda mahakamani.

“Hapa Tanzania hatukuweza kuifunga nchi (lockdown) au kuacha kufanya kazi ila tulitumia teknolojia za kisasa katika kutoa huduma kwa wananchi katika sekta mbalimbali huku Mahakama ikiwa ni miongoni mwa Sekta mojawapo.

“Nchini Tanzania moja ya eneo ambalo tulitafutia utatuzi wa kiteknolojia ili kupunguza madhara hasi ya Corona ni usimamizi wa haki kupitia teknolojia rafiki za nyumbani ambapo Mahakama ilihakikisha utoaji wa huduma kwa wote waliokuwa na uhitaji na pia iliweza kuhakikisha usalama wa watumishi wake wanaofanya kazi mahakamani,” alisema.

Aliongeza: “Ubunifu wa kutumia njia tofauti za teknolojia za kisasa ulisaidia kurahisisha uwezo wa kusikiliza kesi zote na kupitia utafiti na ushahidi kwa kina, pia kujitoa katika njia za kutafuta suluhisho la kina zaidi, matumizi ya Akili Mnemba (AI) yalitumika katika ufikishaji wa haki.”

Alisema, ukuaji wa teknolojia ni muhimu kwenye kukuza uchumi wa nchi ambayo inahitajika kutumika katika uhakika wa chakula kwa bara la Afrika, kuondoa changamoto ya ajira kupitia kilimo biashara na uwekezaji.

Rais Samia alisema, Tanzania ni nchi ya nne barani Afrika kuratibisha uzinduzi wa eneo huru la biashara barani humo.

“Eneo la biashara huria la Bara la Afrika siyo tena ndoto, bali ni ukweli, limewaleta pamoja nchi wanachama 55 wa Umoja wa Afrika,” alisema.

Alisema, kutokana na maendeleo hayo sasa eneo huru la Bara la Afrika si ndoto tena, bali limeweka pamoja wanachama kuunda bara moja la biashara ambalo litakuwa eneo kubwa la biashara huria yenye watu wapatao bilioni 1.3 na kukusanya pato la taifa kwa Dola za Marekani trilioni 3.4.

Aidha, alisema biashara huria itakuza shughuli za kiuchumi kwa wananchi, kuondoa vikwazo kwenye uingiaji na kukuza sekta binafsi katika soko huria la biashara Afrika.

Alisema eneo la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, kukuza ari kwa wafanyabiashara wadogo na wakati ambao italeta bidhaa mbalimbali na kubadilishana teknolojia.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Jukumu la Idara za Kitaifa za mahakama katika kutatua mizozo chini ya eneo huru la biashara barani Afrika, matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ufanisi katika utekelezaji, ndiyo iliyomvutia’.

“Ninajua mmesoma na mnafahamu kuhusu kutiwa saini kwa makubaliano ya kubuni eneo huru la kibiashara barani Afrika, Machi 2018, mnajua kuhusu kuratibishwa kwa makubaliano hayo nakuanza kutumika Aprili 29, 2019, na mnajua uzinduzi wa eneo huru la biashara barani Afrika Januari 2021, kwa hivyo sitaelezea mengi,” alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema, ana imani kwamba iwapo Soko la Bara Afrika litaungwa mkono na kutumika kikamilifu litafaidisha nchi za bara hilo kutokana na ukubwa wake.

Aliwataka majaji hao kutumia muda mchache katika majadiliano yao kutafuta njia za kuhakikisha wanashiriki kutatua mizozo katika eneo huru la biashara barani Afrika linatumia teknolojia ya kisasa kuharakisha utekelezaji wa haki.

Alisema Bara la Afrika ni tajiri kutokana na kuwa na rasilimali na rasilimali watu. 

Aidha, mkutano huo unahusisha majaji wakuu wa nchi wanachama wa jukwaa hilo kama Tanzania, Kenya, Uganda, Namibia, Zimbabwe, Eswatini, Msumbiji, Seychelles, Botswana, Angola, Zanzibar, Malawi, Lesotho, Mauritius, Zambia na Afrika Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *