Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia ambazo pia zitahudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika.
Rais Samia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema.
Rais Samia pia amealikwa kufanya ziara ya kitaifa nchini Zambia kuanzia jana Jumatatu, Oktoba 23 – 25 ,2023 ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia.
Ziara hiyo ni ya kwanza ya Kitaifa ya Rais kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022, itakumbukwa kuwa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umejengwa na misingi ya kindugu.
Rais Samia pia amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tarehe 25 Oktoba, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa nne kuhutubia Bunge hilo.
Ziara hiyo inalenga kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zambia katika maeneo ya kimkakati ya sekta za uchukuzi, nishati, biashara na miundombinu na kuongeza kuwa katika ziara hiyo Mhesimiwa Rais Dkt. Samia na Mwenyeji wake watajadili namna ya kuboresha miundombinu inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia ikiwemo Bomba la Mafuta la Tazama, Reli ya Tazara na Barabara ya TanZam.
Aidha, malengo mengine ya ziara hiyo ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wafanyabiasha na wasafirishaji ili waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, kuibua fursa mpya za ushirikiano na kuieleza jumuiya ya wafanyabiashara Zambia kuhusu maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Dar es Salaam.
Akielezea kuhusu urari wa biashara kati ya Tanzania na Zambia, Mhe. Waziri Makamba amesema mwenendo wa ukuaji wa Biashara kati ya Tanzania na Zambia umeendelea kuongezeka kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mwaka 2016 Tanzania iliuza nchini Zambia bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 70,815.40 na kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 183,648.5 kwa mwaka 2022.