Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amechochea ari ya ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Afrika (African Super League) itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho Ijumaa, Oktoba 20, 2023.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema kwamba, Rais Samia ameahidi kutoa shilingi milioni 10 kwa kila goli ambalo Simba itafunga kwenye mechi hiyo muhimu.
Simba inaikabili Al Ahly ya Misri katika mchezo huo mgumu, ambapo inahitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo mapya ambayo mwaka huu yanashirikisha timu nane.
Timu hiyo zitarudiana baadaye jijini Cairo, ambapo mshindi atafuzu kwa hatua ya nusu fainali.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kutoa motisha kwa wanamichezo, kwani msimu uliopita alianza kwa kutoa zawadi ya shilingi milioni tano kwa kila goli wakati Simba na Yanga zikiwa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na la Shirikisho mtawalia.
Timu hizo zilipofuzu kwa robo fainali, Rais Samia akaongeza motisha na kutoa Shilingi milioni 10 kwa kila goli, kitendo kilicholeta hamasa kwa timu hizo kujitahidi hadi Yanga ikafanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho na kutolewa kwa Kanuni za Mashindano.
Msimu huu pia Rais Samia amekwishatangaza kwamba, zawadi zake zinaendelea kwa klabu hizo ambazo zimefuzu zote kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.