*Ni zile zilizopitwa na wakati, asema…
*Aipongeza TAMWA kwa utendaji kazi
Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amezielekeza Wizara kuendelea kufanya maboresho na mapitio ya baadhi ya sera na sheria zilizopitwa na wakati ili kutungwa mpya.
Naibu Waziri wa Habari, Mhandisi Kundo Mathew aliyasema hayo jana kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliani na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.
Kauli hiyo aliitoa katika maadhimisho ya miaka 36 ya Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA).
“Rais Dkt. Samia anatambua kazi zinazofanywa na TAMWA katika jamii.
“Ametuelekeza kama Wizara tuendelee kufanya mapitio, maboresho ya baadhi ya sera zilizopitwa na wakati zisizoendana na wakati wa sasa,” alisema.
Alieleza kuwa, Rais Dkt. Samia anatambua mchango mkubwa unaotolewa na TAMWA serikalini, utungaji wa sera na sheria zinazoendana na mahitaji ya jamii.
Mathew alisema, tayari Rais Dkt. Samia amepokea ushauri walioutoa serikalini kuhusu sheria ya habari, utangazaji pamoja na ukatili wa kijinsia.
Alisema serikali itaendelea kupokea ushauri wa TAMWA na kuzifanyia kazi changamoto zote ambazo zitakua ndani ya uwezo wa serikali.
“Tasnia ya habari ina changamoto nyingi hivyo Wizara inaendelea kuzishughulikia ikiwemo mabadiliko ya sheria mbalimbali ili kukidhi upatikanaji taarifa na uhuru wa kujieleza.
“Katika uhuru wa kujieleza serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samian na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwiny, tayari wamehakikisha uhuru wa kujieleza uko vizuri ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” aliongeza.
Aliongeza kuwa; “Wanahabari na vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa tayari vimefunguliwa kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia,” alisema.
Aliongeza kuwa, tangu serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, hakuna chombo cha habari kilichofungiwa au mwandishi wa habari kutotendewa haki ndani ya mipaka ya Tanzania.
“Tuendelee kuiunga mkono serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia, amekua sikio la Watanzania linalotoa majibu kwa vitendo badala ya maneno,” alieleza.
Takwimu za TAMWA zinaonesha asilimia 64 ya wanahabari wanaume wanauhakika wa kupewa mikataba ya kazi katika vyombo vya habari ukilinganisha na asilimia 36 ya wanahabari wanawake.
Aliwahimiza wanawake kutumia vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kushiriki katika maendeleo, kutoa na kupata taarifa muhimu hasa kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Selestine Kakele, alisema serikali itaendelea kushirikiana na TAMWA kutatua changamoto zao.
Aliipongeza TAMWA kwa kusimamia dhamira ya kujenga jamii ya Watanzania yenye usawa ambao unazingatia mlengo wa jinsia.
“Sote tukisimama kama taifa na kusema tumepiga hatua katika eneo hili hatuwezi kuitenga TAMWA, tutaendelea kutunga, kutekeleza sera, sheria, kushirikisha wadau katika eneo hili,” alisema.
Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe, alisema anaamini waliopo kwenye tasnia ya habari wanathamini ushirikiano uliopo kati ya serikali na vyombo vya habari hasa kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknoloji ya Habari..
“Ushirikiano huu upo katika michakato mbalimbali yenye lengo la kujumuisha sauti zetu katika maboresho ambayo yanakusudiwa kwenye sera na sheria ili tuwe na mifumo bora ya kuimarisha haki za wananchi kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari,” alisema.
Alisema michakato inayoendelea ya sheria ya vyombo vya habari ni kielelezo tosha cha serikali kutambua mchango wa vyombo vya habari kuongeza kasi ya utekelezaji mipango ya maendeleo ya taifa.
Kamati inayoundwa kuchunguza hali ya uchumi katika vyombo vya habari nchini itaweka wazi changamoto ili zitafutiwe ufumbuzi, kuleta tija katika sekta hiyo.
Alifafanua kuwa, kamati hiyo italeta mwanga juu ya changamoto zinasosababisha vyombo vya habari kulegea kiuchumi kwenye maeneo ya sera, sheria na teknolojia.
“Tunafahamu miongoni mwa changamoto za vyombo vya habari ni ukosefu wa rasilimali fedha inayoathiri uwezo wa vyombo katika kuajir,i kuweka maslahi bora kwa waajiriwa, kutoa mafunzo endelevu ya kitaaluma na kugharamia vitendea kazi vya kisasa,” alisema.
TAMWA itaendelea kuwa mstari wa mbele kuinua weledi, viwango vya wanahabari wanawake wa Bara na Zanzibar, kutafuta fursa ndani, nje ya nchi ili kufanya kazi kwa karibu zaidi za kijinsia, kuimarisha utumiaji tafiti za masuala ya wanawake katika vipindi, makala.
Shebe alisema TAMWA imebobea katika uchechemuzi wa masuala ya wanawake na watoto na kujikita zaidi kwenye taarifa za kiutafiti.
Alisema bado kuna kazi ya kupambana na umaskini kwa wanawake, wasichana unaochangia udhalilishaji, rushwa ya ngono, ukandamizaji, kwenye mashirika binafsi na umma hivyo kuleta uoga na hofu kwenye upatikanaji huduma za maendeleo miongoni mwa wanawake.
“Tafiti zinaonesha kwenye vyuo na vyumba vya habari, yapo matatizo, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ikiwemo rushwa ya ngono, TAMWA kwa kushirikiana na asasi nyingine tunalifanyia kazi ili kulitokomeza,” alisema.