Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imewekeza kwenye utafiti wa madini kwa lengo la kupata taarifa sahihi za uwepo wa mashapu ya madini ili kuwarahisishia wawekezaji kuwekeza.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishari, Dkt. Doto Biteko aliyasema hayo jana kwa niaba ya Rais Dkt. Samia wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa 5 wa kitaifa wa madini na wawekezaji wa mwaka 2023.
Alisema sekta ya madini ni nguzo muhimu na chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi na wananchi kwa ujumla.
“Kutokana na taarifa za awali za wakala wa nishati, mahitaji ya madini ya nishati ya kimkakati yataongezeka mara tatu ya mahitaji yaliyopo sasa.
“Ni fursa muhimu kuwekeza kuanzia kwenye utafutaji, uchimbaji, uchimbaji, uongezaji thamani, biashara ya madini ili yalete manufaa kwa watu, nchi, kuifanya Tanzania kuwa sehemu ya rasilimali,” alisema.
Aliongeza kuwa, licha ya Tanzania kuwa na madini mbalimbali ya kimkakati yanayohitajika duniani, bado kuna changamoto ya uwepo wa taarifa za jiolojia katika maeneo mbalimbali yatakayosaidia kugundua na kuchimba madini nchini.
“Serikali imeamua kuwekeza kwenye utafiti wa hali ya juu ili iweze kupata taarifa zaidi za uwepo wa mashapu ya madini na kuwarahisishia wawekezaji nchini kuwekeza kukiwa na taarifa za awali.
“Upatikanaji taarifa hizi utasaidia si tu wawekezaji bali serikali kubainisha viashiria vya uwepo wa madini katika miamba mbalimbali na kuwezesha kufanya utafiti wa madini ya aina mbalimbali nchini,” aliongeza.
Dkt. Biteko alisema, hatua hiyo inalenga kuwarahisishia watafiti, wawekezaji kupita maeneo yatakayokuwa na taarifa zaidi badala ya kuwa katika maeneo ambayo hayana taarifa sahihi jambo ambalo litawapunguzia gharama za utafiti katika hatua za ugunduzi.
Alisema ugunduzi wa mashapu ya madini utawezesha kufungua migodi zaidi nchini, kuongeza mapato ya serikali na ajira kwa wananchi.
Alitoa wito kwa waadu wa maendeleo kuunga mkono juhudi za serikali ili kuhakikisha mpango huo unatumika kuleta manufaa kwa sababu sekta hiyo ni nguzo muhimu ya kuleta chachu ya maendeleo ya nchi na wananchi.
Ukuaji wa sekta hiyo, itafungamanisha sekta zingine ikiwemo kilimo zinazotumia madini kama mbolea, betri za magari, simu.
“Nitoe wito kwa wawekezaji kuwekeza kwenye mnyororo wa madini ikiwemo kujenga viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumia malighafi za madini.
“Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, tunapeleka umeme kwenye baadhi ya migodi ambayo haina umeme,” alisema.
Alifafanua kuwa, zaidi ya migodi 350 ya wachimbaji wadogo imeunganishwa na umeme wa gridi ya taifa ili kuwapunguzia gharama wachimbaji katika shughuli za uchimbaji madini.
Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara sehemu zenye uchimbaji wa madini, ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea ili kusafirisha bidhaa kutoka mgodini kwenda kwenye masoko makubwa duniani.
Pia Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara katika migodi mikubwa na ya kati ili kutoa unafuu wa ubebaji mizigo kwani serikali inaamini wachimbaji wadogo wana fursa ya kukuza uchumi, kutoa ajira kwa vijana hivyo wataendelea kusaidiwa katika maeneo yao.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, aliseam mkutano huo utatoa uzoefu na ujuzi wa shughuli za sekta ya madini, kuwezesha wadau wa madini kupata taarifa mbalimbali kuhusu maendeleo ya sekta hiyo.
“Mkutano huu utatoa fursa ya kuhamasisha na kukuza uwekezaji katika sekta ya madini na kuufahamisha ulimwengu rasilimali tulizonazo, utayari wetu kwa kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuendeleza rasilimali madini tulizonazo,” alisema.
Aliongeza kuwa, mkutano huo ni sehemu ya fursa ya uwekezaji katika sekta ya madini kutoka ndani, nje ya nchi baada ya kutambua fursa zilizopo nchini.
Alisema pia fursa mbalimbali za upatikanaji mitaji, matumizi ya teknolojia ya kisasa, utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani madini kwa kuzingatia uhifadhi wa utunzaji mazingira.
Mavunde alisema pia mkutano huo pia utaangazia masuala ya madini mkakati kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi na ili kufikia hatua ya kuvuna madini, lazima shughuli za utafutaji wa ufanyike ili kugundua mashapu yanayoweza kuchimbwa kibiashara.
“Utafutaji wa madini unakua rahisi pale ambapo zipo taarifa za awali za kijiolojia zinazoashiria uwepo wa madini mbalimbali,” aliongeza.
Alieleza kuwa, nchi nyingi duniani zilizofanikiwa katika shughuli za uchimbaji madini, zimewekeza katika upatikanaji taarifa za kijiolojia.
Taarifa hizo hutumika katika utafutaji wa kina wa madini unaowezesha kupata mashapu ya upatikanaji wa migodi.
“Tanzania tumejaaliwa kuwa na madini mbalimbali ya vito, Tanzanite, madini ya ujenzi, madini ya viwandani, madini ya Metal na nishati.
“Haya yote yanatakiwa kuendelezwa kwa manufaa ya ukuaji wa uchumi wa wananchi na taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa, wakati mikakati ya Rais Dkt. Samia, kuikuza sekta ya madini, alitoa maelekezo ya kuhakikisha Wizara inaongeza, kuboresha utafiti wa jiosayansi ili kuiwezesha nchi kupata taarifa mbalimbali, kuboresha kanzi data ya miamba na madini.
“Hadi sasa hatujawa na taarifa za kutosha za kijiolojia zinazoweza kuwafanya wawekezaji kufanya shughuli za utafutaji wa kina wa madini.
“Ni asilimia 16 tu ya nchi yetu ndiyo iliyofanyiwa utafiti wa teknolojia ya kisasa ambayo huwezesha kubaini maeneo yenye viashiria vya uwepo wa madini mbalimbali,” aliongeza.
Alifafanua kuwa kwa kutambua umuhimu wa kupatikana kwa taarifa hizo, Wizara imejipanga kufanya utafiti wa kijiolojia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuboresha taarifa za kijiolojia.
Mavunde alisema, kupitia utafiti wa kina utakaofanywa, sekta zingine zitanufaika na taarifa hasa Wizara ya Maji, Kilimo kwenye uzalishaji wa mbolea.
Upatikanaji taarifa za kijiolojia katika maeneo mengi ya nchi utahamasisha kasi ya uwekezaji katika utafutaji madini nchini.
Alisema utekelezaji wa dira ya 2030 utakua chachu ya kuongezeka shughuli za utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani biashara ya madini na uanzishwaji wa viwnada vinavyotumia madini mbalimbali hasa viwanda vya kuzalisha mbolea, saruji, chuma, gypsum board, nyaya za umeme na chokaa.