Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amepewa Tuzo ya Heshima na Pongezi yenye alama ya Namba moja kwa kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika Mkoa wa Shinyanga na Tanzania.
Tuzo hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga kwa niaba ya wanawake wa Mkoa huo, kuikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa huo, Christina Mndeme kwa niaba ya Rais Samia.
Akikabidhi tuzo hiyo, Samizi aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kutoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo, alisema Mkoa huo unajivunia maendeleo lukuki.
Maendeleo hayo yapo katika sekta zote ikiwemo ya afya, elimu maji na nishati ya umeme.
“Kongamano hilo lililenga kumpongeza Rais Dkt. Samia kutokana na maendeleo aliyoyaleta mkoani Shinyanga hivyo tumempa tuzo ya shukrani na pongezi kwa sababu vijiji vyote vimenufaika na mabilioani ya fedha anazozitoa ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema.
Akipokea tuzo hiyo, Mndeme aliwashukuru wanawake hao kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa huo.
“Naipongeza kamati ya maandalizi ya kongamano hili kwa kumpongeza Rais Dkt. Samia, nakiri kupokea tuzo hii yenye alama ya namba moja kutoka kwa wanawakw wa Mkoa wa Shinyanga, nitamfikishia Rais Dkt. Samia,” alisema.