Samia anavyotekeleza kwa kasi miradi ya kimkakati

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

MATUKIO makubwa mawili yaliyotokea Ijumaa, Juni 14, 2024, yameleta historia ya pekee kuhusu utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na kubatilisha hoja za waliokuwa wanadhani asingeweza kuleta mabadiliko makubwa.

Kuanza kutoa huduma kwa miradi miwili mikubwa aliyoikuta, ambayo ameiendeleza kwa kasi kubwa, kumewafanya ‘wapinzani’ waliodhani angeitelekeza miradi iliyoachwa na mtangulizi kubaki wametunduwaa.

Kwanza, siku hiyo kwanza treni iendayo kasi ya SGR ilianza rasmi kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Morogoro, hii ni baada ya kukamilisha ujenzi wa kipande hicho cha reli ambacho wakati akiingia madarakani kilikuwa hakijavuka 70%.

Mradi wa SGR

Ikumbukwe kwamba, alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Rais Samia alikuta ujenzi wa reli hiyo ya kisasa uko katika vipande viwili tu: Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) na kipande cha Morogoro – Makutupora wilayani Manyoni (kilometa 422), na havikuwa vimefikia hatua kubwa.

Kasi yake ya kushangaza siyo tu ilifanya kukamilika kwa vipande hivyo viwili, lakini akaanzisha ujenzi wa vipande vinghine kama cha Mwanza – Isaka (kilometa 249), Makutupora-Tabora (kilometa 294), Tabora-Isaka (kilometa 130), na Tabora-Kigoma (kilometa 506) ambazo ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa kuweka kumbukumbu sawa, kipande cha reli cha Dar es Salaam – Morogoro (300 km) ujenzi wake ulianza rasmi Aprili 12, 2017 na hadi kufikia Aprili 2024 ulikuwa umekamilika kwa asilimia zote, ukiwa chini ya kampuni ya Yapı Merkezi ya Uturuki ikishirikiana na Mota Engil Africa ya Ureno.

Kipande cha Morogoro – Makutupora (Km 442) ujenzi wake ulianza rasmi Machi 14, 2018 chini ya kampuni ya Yapi Merkezi, ambapo hadi kufikia Aprili 2024, utekelezaji wake ulikuwa umefikia 96%, sehemu kubwa ikiwa umetekelezwa katika awamu ya sita chini ya Rais Samia.

Itakumbukwa kwamba, mnamo Aprili 21, 2024 yalifanyika majaribio ya safari kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliahidi kwamba, ifikapo Julai 2024 reli itaanza kwenda moja kwa moja hadi Dodoma kutoka Dar es Salaam, umbali wa kilometa 627 na ikisafiri kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.

Awamu ya tatu ni kipande cha Makutupora –Tabora (Km 294 + km 78 ya michepuo) ambapo kampuni ya Yapı Merkezi ilianza ujenzi wake Aprili 12, 2022, zikiwa ni jitihada kubwa za Rais Samia kuhakikisha ndoto ya watangulizi wake kuwa na mtandao bora wa reli inatimia.

Muda wa ujenzi wa kipande hicho ni miezi 46 ikiwemo kipindi cha majaribio, na mpaka sasa ujenzi wake umefikia 14%.

Kipande cha Tabora – Isaka (Km 130 + Km 35 za michepuo) kinajengwa pia na Yapi Merkazi na mkataba ulisainiwa Julai 4, 2022 huku ujenzi ukianza rasmi Januari 18, 2023 ambapo utachukua miezi 42 ikiwemo miezi sita ya majaribio. Hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa kipande hicho ni 5%.

Kipande cha tano ni cha Isaka – Mwanza (Km 249 + Km 92 za michepuo). Januari 2021 Serikali ilisaini mkataba na kampuni za China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction (CRCC).

Juni 14, 2021, Rais Samia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kipande hicho katika sherehe zilizofanyika Fela jijini Mwanza, ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia 54%.

Kipande kingine ni cha Tabora – Kigoma (Km 506) ambapo Desemba 20, 2022 Serikali iliingia mkataba na kampuni za China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway Construction Company (CRCC) kuanza ujenzi.

Hizi ni jitihada za makusudi za Rais Samia za kuhakikisha anaiunganisha Tanzania nan chi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda kwa mtandao wa reli.

Mradi wa umeme wa JNHPP

Ijumaa, Juni 14, 2024 wakati safari za treni ya mwendokasi zikianza Dar es Salaam kwenda Morogoro, mtambo namba nane wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kwa mara ya kwanza ukaingiza Megawati 235 zingine kwenye Gridi ya Taifa.

Hatua hiyo inafanya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme, kuwa na jumla ya Megawati 470 zinazotumika katika Gridi ya Taifa na kufanya nchi kuwa na ziada ya Megawati 70 baada ya kipindi kirefu.

Akiwa jijini Dodoma, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizindua Taarifa za Utendaji katika Sekta Ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa Mwaka 2022/2023, alitangaza hatua ya mtambo namba nane wa JNHPP kuanza kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.

Akasema, kwa sasa Megawati 470 zinazalishwa kutoka JNHPP na tayari zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Itakumbukwa kwamba, mnamo Februari 2024, Dkt. Biteko alitangaza mtambo namba tisa wa JNHPP kuanza kutoa Megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa, ambazo kwa namna ya pekee zilififisha makali ya mgawo wa umeme ulioanza tangu mwaka 2023, huku akisema upungufu ulikuwa Megawati 200 hadi 400.

Lakini hatua ya mtambo namba nane kuanza kutoa Megawati 235 na hivyo kufanya jumla ya Megawati 470 kutoka JNHPP, imesababisha Taifa sasa kuwa na ziada ya Megawati 70, ziada ambayo ni takriban sawa na uzalishaji wote wa Bwawa la Kufua Umeme la Mtera lililojengwa kati ya mwaka 1970 na 1988, likiwa na mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 80.

Hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa hakika amevuka malengo na makisio yaliyowekwa na taasisi za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia.

Uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati unaofanywa na Rais Samia umeleta matokeo ya haraka zaidi, kwani wakati anaingia madarakani Machi 19, 2021 alikuta utekelezaji wa mradi wa JNHPP ukiwa asilimia 37.

Lakini hadi Aprili 2024, utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 97.43 na ukaanza uzalishaji kupitia mtambo namba tisa unaoingiza katika Gridi ya Taifa jumla ya MW 235 na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme.

Mpaka kufikia hatua hiyo, Serikali imetumia Shs. trilioni 6.01 na kwa mujibu wa taarifa, hivi sasa kazi inaendelea ili kukamilisha ufungaji wa mitambo saba yenye uwezo wa kuzalisha MW 235 kila mmoja.

Ikumbukwe kuwa, Hayati Magufuli alifariki dunia katika kipindi ambacho utekelezaji wa mradi wa JNHPP ukiwa umefikia 33%.

Katika kipindi hicho, hakukuwa na aliyeamini kama kutakuwa na mwendelezo wa utekelezaji na ndipo matumaini ya kupatikana kwa nishati ya umeme wa uhakika yaliyeyuka vichwani mwa Watanzania.

Hata hivyo, Rais Samia ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, mradi huo uliendelea kujengwa hadi sasa umefikia asilimia 97.

Miradi mingineyo ya kimkakati

Wakati akiingia madarakani, Rais Samia alikuta miradi kadhaa iliyoanzishwa na mtangulizi wake, ambayo bila kusahau kwamba yeye ndiye alikuwa Makamu wa Rais na kwa hivyo anaijua na aliahidi kuiendeleza kwa kasi.

Rais Magufuli alikuwa ameanzisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa Daraja la Tanzanite, Daraja la Magufuli (Kigongo-Busisi), Daraja la juu la Mfugale na Daraja la juu la Kijazi (makutano ya barabara Ubungo).

Wakati anafariki, miradi iliyokuwa imekamilika kati ya hiyo ni Daraja la Mfugale na Daraja la Kijazi pale Ubungo, lakini miradi mingine ya kimkakati kama JNHPP na SGR ilikuwa katika hatua za utekelezaji.

Rais Samia alipoingia madarakani akaweka wazi msimamo wake juu ya yote yaliyoachwa na mtangulizi wake. Akasisitiza kuwa hakuna mradi hata mmoja utakaosimama, yote itaendelea kujengwa kama ilivyopangwa. Na ndivyo anavyofanya sasa, tena kwa kasi ya ajabu.

“Mimi na Hayati Magufuli ni kitu kimoja, kwa maana hiyo mambo mengi ambayo Serikali ninayoiongoza imepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Hayati Magufuli wakati akilizindua Bunge hili,” alisema Rais Samia katika hotuba yake ya kwanza bungeni jijini Dodoma Aprili 22, 2021.

Hilo linathibitika na kinachoshuhudiwa sasa ambapo miradi yote iliyoanzishwa na mtangulizi wake anaendelea kuitekeleza katika uongozi wake.

Rais Samia anatekeleza miradi hiyo, ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitatu Daraja la Magufuli (Kigongo–Busisi) linaendelea kutekelezwa, ambalo wakati Magufuli anafariki, utekelezaji wake ulikuwa 16%, lakini sasa umefikia 80.1% na ujenzi wake utakamilika Desemba.

Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya. Hayati Magufuli aliacha ndege 11, lakini kwa sasa Rais Samia amenunua ndege zingine tano ikiwemo ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F. Ndege aina ya Boeing 737-9 Max ilikwishapokelewa; na Serikali imelipa sehemu ya malipo ya ndege aina ya Boeing 737 Max 9, Boeing 787-8 na Boeing 737-7.

Hii ni mifano michache tu ya namna Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyodhamiria kuwaletea maendeleo kwa kasi Watanzania, bila kujali changamoto mbalimbali zilizopo, zikiwemo za baadhi ya wapinzani wanaokejeli licha ya matokeo chanya yanayoonekana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *