Samia anavyoisimamia falsafa ya ‘Elimu ni Kazi’

Na Daniel Mbega,
Kisarawe

“VIJANA wetu lazima wapate elimu inayoendana na Afrika. Hii ina maana kwamba, elimu ambayo siyo tu inatolewa Afrika lakini pia inayolenga kukidhi matakwa ya sasa ya Afrika.”
Hayo ni maneno aliyoyatoa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Oktoba 25, 1961 akizungumzia kuhusu elimu na sheria.
Mwalimu Nyerere aliamini kwamba, elimu pekee ndiyo ingeleta maendeleo ya Tanzania, na hata Afrika kwa ujumla, na ndiyo maana hata katika hotuba zake nyingi alisisitiza umuhimu wa watoto kufundishwa namna ya kujitegemea na siyo kufaulu mitihani tu.
Kama Mwalimu Nyerere alivyoamiani, vivyo hivyo Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, anaamini na anatekeleza falsafa hii kwa vitendo.
Rais Samia tangu ameingia madarakani amekuwa akihimiza elimu, na ndiyo maana akaongeza namna ya utoaji wa elimu bure bila malipo, kwamba sasa watoto wetu watasoma hadi kidato cha sita bila kulipa ada.
Na Rais Samia anahimiza wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule, huku akitilia mkazo watoto walioko katika mazingira magumu, wakiwemo wa vijijini.
Kutokana na kuamini kwamba, elimu inaweza kuwafanya watoto waziishi ndoto zao, ndiyo maana akatangaza kwamba, mabinti wote waliopata ujauzito wakiwa shule na kusitisha masomo yao, sasa warejee darasani kumalizia pale walipoishia na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.
Mwalimu aliamini elimu ni ule ujuzi ambao unamwezesha mtu kujitegemea katika mazingira yanayomzunguka, na siyo fikra zile za kale za kuona kwamba eti mtu mwenye elimu mahali pake pa kazi ni ofisini tu.
Suala hili Mwalimu alijitahidi kulikemea kwa kutumia busara, akifafanua kwa hekima katika hotuba zake mbili alizowahi kuzitoa mjini Tabora (Mei 4, 1967) na mjini Mbeya (Mei 14, 1967) ambapo alisema shabaha ya elimu ya msingi lazima ibadilike.
Rais Samia, ambaye naye mzazi wake alikuwa mwalimu, anaishi katika misingi ya Nyerere, na katika hili ameelekeza nguvu zake kwa watoto kupata elimu itakayowafanya wajiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Kwa kutambua mfumo wa elimu umebadilika kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ndiyo maana anawahimiza watoto wakazane kusoma sayansi, na kwamba wanaofaulu vizuri wanasomeshwa bure masomo yao ya elimu ya juu.
Mwalimu Nyerere yeye alisikitika sana kubaini kwamba miaka ya nyuma wakati nafasi za elimu zilipokuwa chache watu waliona kuwa elimu ya msingi ilikuwa maandalizi siyo ya maisha bali ya kuendelea zaidi kielimu na kupata kazi za ofisini.
Lakini akasema kwa kuupanua mfumo wa elimu kwa wote (Universal Primary Education – UPE), elimu ya msingi inaweza kuwa maandalizi ya maisha kijijini na siyo kazi za maofisini tu.
“.. Elimu ya primary kama mnavyojua walimu wenzangu, mimi sikuwahi kufundisha katika primary kwa hiyo sijui matatizo yake ya kufundisha. Nimefundisha katika sekondari tu na nimeanzia hapa hapa Tabora. Kwa hiyo najua matatizo ya sekondari skuli lakini siyo haya ninataka kuzungumza; wala si matatizo ya walimu ninataka kuzungumza; ni matatizo ya nchi,” alisema.
“Primary, kama mnavyojua kwanza mpaka sasa ni nusu tu ya watoto wetu ambao wanapata nafasi ya kusoma. Kabla ya uhuru tulikuwa tuna ngazi mbili za shule za primary. Tunayo ile miaka minne ya kwanza, halafu wachache hupenya wakaingia katika miaka minne mingine inayofuata ambayo tunaita middle school. Halafu wachache hupenya wakaingia katika miaka miwili inayofuata iliyokuwa ya standard nine na standard ten ya sekondari skuli. Halafu tena tunachuja chuja.
“Tulikuwa na ngazi nyingi sana za kuchuja chuja. Sisi tukaahidi katika TANU. Tukaahidi kwamba tutafanya mambo mawili. La kwanza, tutajitahidi kuondoa ngazi hii hapa baada ya miaka minne. Pili, kwamba primary nzima tutaifanya miaka minane. Miaka minane ile tukaijaribu ikatushinda. Tukaona mirefu. Tukaipunguza tukafanya kwamba elimu ya primary tutaifanya iwe miaka saba tu basi.
“Basi ndivyo ilivyo sasa, na ndivyo tunavyojitahidi, na mwaka jana, nadhani, tukaanza kupata mgogoro wetu wa kwanza kabisa walipomaliza watoto wengi, nadhani wanakaribia 50,000 waliomaliza standard seven. Wachache wakaingia form one. Wengine hawakupata nafasi kuingia form one. Tukapata kelele za wazee. Tulipata kelele nyingi sana mwaka jana. Na mwaka huu tumepata zingine, na nadhani tutaendelea kupata kwa watoto kukosa nafasi ya kuingia form one.
“Na wazee wanasema: “Mwanangu mimi hakushindwa; mbona kakosa nafasi ya kuingia katika form one? Na wengine wale tunajibu hivi hivi. Tunasema: Mtoto ameshindwa, huyu ameshindwa, huyo ameshindwa.” Na washindwaji hawa ni 90 kwa 100 ya watoto wote… waliofaulu ni wale 10 kwa 100… ndio lugha tunayoitumia. Kusema kweli tunaitumia mpaka sasa. tunajaribu kuifuta ile lugha lakini tunaitumia mpaka sasa.”
Mwalimu alisema kwamba walikuwa wanaogopa kutokana na wingi wa watoto wanaomaliza shule halafu hawana mahali pa kwenda, yaani wanakosa nafasi za kwenda sekondari wakati huo, kutokana na uhaba wa shule za sekondari uliokuwepo.
“Wazee wanauliza; “Mwanangu nitamfanyaje? Sasa mtoto wangu ameshindwa kwenda darasa la nane, form one. Mimi nitamfanyaje mwanangu?” miezi ya nyuma nilipopita katika mzunguko ule nilioutaja hapa nilikuwa Musoma, wazee wangu kule wakataka kunikabidhi watoto wao. Wanasema:- “Nenda nao huko huko Dar es Salaam. Mimi nitawafanyaje watoto hawa. Wameshindwa! Nenda nao huko wewe utajua la kufanya.” Nenda nao watoto wenu? Mimi watoto wote hawa wa standard seven nitawabeba! Wa Tanzania nzima nitakwenda nao wapi? Mzee anaulia: Sasa mtoto huyu ana miaka 13 tu, 14 tu, mnasema eti alime? Atalimaje mtoto wa miaka 13 tu, 14 tu, atawezaje kulima?
“Swali hilo anayejiuliza si swali la kweli. Upande mmoja si swali la kweli hata kidogo. Ni swali la mazowea tu. Anasahau mzee huyu huyu, ama mwalimu, wakati mwingine mtu mwenye akili nzuri kabisa anakuuliza swali hili… anasema umri wake mdogo mno hawezi kulima. Upande mmoja ni kweli, watoto hawa wana umri mdogo lakini si umri unaoleta problem. Tatizo ni kwamba wamesoma watoto hawa. Maana swali hili haliulizwi kwa mtoto mwenye umri kama huo ambaye hakusoma. Haliulizwi. Wanasaga watoto wale nyumbani, wanaleta kuni… wanalima… wanachunga ng’ombe… wanavuna. Haliulizwi swali hili juu ya watoto ambao hawakupata nafasi ya kwenda shule. Wao wanasema atalimaje na mwanangu kasoma? Kusoma huko kwa kulima ni kusoma gani? Maana nia ya kusoma, madhumuni ya kusoma ni kuepuka jembe. Anasoma mtu aepukane na maisha haya ya vijijini ya majembe majembe haya.
“Elimu ilikuwa ni utaratibu wa kuhama vijijini… ukianza kumsomesha mtoto unajua safari yake ya kuhama imeanza. Ilikuwa inaanza hivi unaiona. Na hasa kwa sababu shule tulikuwa hatuna nyingi, watu waliweza kujua kwamba anakwenda huyu sasa. Halafu baada ya hapo tena nimefanya safari na kumaliza standard four. Kwangu standard five nimekuja Tabora. Kutoka Musoma unakwenda kuifuata standard five Tabora. Ndio unakwenda hivyo!
“Unahama. Na kusema kweli wengine hatujarudi tena. Tumekwenda moja kwa moja. Sasa ikawa ndio mazowea kwamba mtoto akishapata nafasi ya kusoma, kusoma ni kutokana na kilimo. Anakuwa kalani na kalamu anaiweka hapa kichwani. Lazima awe ana kalamu msomaji huyu na shughuli zake hazitokani na kilimo kilimo. Hata unaporudi nyumbani… wanakufanyia kazi wale wa nyumbani. Shughuli hizi za kufagia fagia au kazi za mikono wenyewe nyumbani wanakufanyia. Wanasema huyu kasoma! Mpaka wewe mwenyewe uwe mtundu kidogo useme nitafanya. Uweze kushika ufagio ufagie mahala, au uchukue vyombo usafishe, au uchukue debe uende kuchota maji… kwa sababu watu wa nyumbani hawakutazamii uchote maji. Binti aliyesoma debe kichwani si mahala pake.
“Haya ndio mawazo yetu. Na hii ni kwa sababu siku zile elimu ndivyo ilivyokuwa. Ilikuwa ni kitu cha bahati bahati. Anakipata mtu mmoja kwa bahati, na makusudi yake ni hayo, unampata mtu akawatumikie wakoloni wanaomtaka kwa shughuli fulani fulani… Elimu haikuwa ni haki ya kila mtu. Elimu ikishakuwa ni haki ya kila mtu, lazima iwe si elimu ya kuhamisha mtu. Lazima iwe elimu ya kumwezesha mtu yule mahali pake alipo, maisha yake yanakuwa mazuri zaidi.”
Ingawa maneno haya aliyasema Mwalimu Nyerere miaka 49 iliyopita, lakini bado yangali vichwani mwa watu wengi, kwa sababu tunashuhudia kwamba hata kiwango cha elimu kinachotolewa sasa shuleni hakikidhi haja kwa mtoto kujitegemea hapo baadaye.
Maadamu tumekusudia kuwafundisha na kuwaelimisha watoto wetu, ni lazima tuondokane na mawazo kwamba elimu ni ya kuwahamisha wasomi kutoka vijijini.
Serikali ya Rais Samia inatambua hili na imeandaa mikakati kabambe kuhakikisha kwamba, watoto wanapata siyo elimu tu, bali ujuzi ambao utawafanya wajiajiri katika muktadha wa kujitegemea ili kujiletea maendeleo.
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na mipango ya kujenga vyuo vya ufundi nchini, ambavyo vitasaidia kuwapa stadi mbalimbali siyo watoto pekee, bali wananchi kwa ujumla, ili kutumia stadi hizo kujiletea maendele maendeleo kiuchumi na kijamii.
Na katika kuzienenda falsafa za Mwalimu Nyerere za Elimu ni Kazi, Rais Samia anajitahidi kujenga shule bora, mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ya kuboresha mitaala iendane na matakwa ya sasa yatakayofanya watoto wafikirie kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *