Samia anavyoimarisha mtandao wa reli kuinua uchumi Tanzania

Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
JUHUDI za Serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato zimeonekana.
Ukiacha chungu kikubwa cha mapato, yaani Bandari ambayo sasa inaweza kuongeza ufanisi kufuatia uwezekano wa kampuni ya DP World ya Dubai kuwekeza, miundombinu, hasa ya reli, ni chanzo kingine kikuu cha mapato katika sekta ya usafirishaji wa mizigo.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuhakikisha kwamba, miundombinu ya reli inaboreshwa na kuimarisha mtandao wa reli nchini ili kukuza uchumi.
Siyo siri, kwamba Shirika la Reli Tanzania lilikufa kutokana na ufisadi na uzembe wa watendaji, ambao inaonekana dhahiri walikula njama za makusudi na wafanyabiashara wanaohusika na usafirishaji kupitia malori na mabasi, ili wafanyabiashara hao washike hatamu.
Reli ya Kati – pamoja na matawi yake ya Tanga-Arusha, Mwanza na Mpanda – ilizorota tangu walipolibinafsisha shirika hilo mwaka 2007, hivi sasa njia za Tanga-Arusha na hata Mpanda zimekufa huku miti mikubwa ikiwa imeota katikati ya reli. Reli ya Tanga-Moshi ambayo ilisitishwa tangu mwaka 1994 kwa treni za abiria, sasa imekwishafufuliwa.
Usafirishaji katika Reli ya Tazara, ambayo ni ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia, nao unasuasua huku shirika hilo limekuwa likikumbwa na migomo ya wafanyakazi kila uchao kutokana na malimbikizo ya mishahara.
Licha ya uboreshaji wa magari kwa sasa ambayo yanakwenda kwa kasi zaidi tofauti na zamani, pamoja na miundombinu bora ya barabara, usafiri wa reli bado unapaswa kuwepo kwa sababu unaweza kuingiza mapato makubwa kwa serikali.
Mizigo mingi inayosafirishwa na malori, iwe ndani ama nje ya nchi, inaweza kusafirishwa kwa treni na kuondoa msongamano wa malori pamoja na makontena bandarini kama ilivyo sasa. Hii ni kwa sababu, treni moja inaweza kubeba hata makontena 50 yenye urefu wa futi 40 kwa mara moja.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya kilometa 5,000 za reli zitajengwa katika miradi kadhaa ambayo tayari imekwishapitishwa ili kuwezesha treni za abiria za mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa kupita kwa urahisi huku zile za mizigo zikienda kwa kasi ya kilometa 80 kwa saa itakuwa ni ya kwanza kwa Afrika ikifuatiwa na nchi ya Morocco.
Julai 20, 2016 Benki ya Exim ya China ilikubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani 7.6 bilioni (sawa na zaidi ya Shs. 16 trilioni) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa ambao ulianza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang, aliwahi kuahidi alipokuwa katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kuwa pamoja na kutoa fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za Reli ya Kati, benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalam katika ujenzi na uendeshaji wa reli hiyo.
Reli mpya ya Kati inayojengwa kwa Standard Gauge badala ya Meter Gauge itakuwa na urefu wa jumla ya kilometa 2,561 ikihusisha njia kutoka Dar es Salaam-Kigoma, Tabora-Mwanza, Kaliua-Mpanda, Kalema-Uvinza/Gitega-Msongati nchini Burundi na Isaka-Rusumo hadi Kigali nchini Rwanda.
Ujenzi wa kipande cha kwanza cha Reli ya Kati chenye urefu wa kilometa 300 ulianza tangu Aprili, 2017 ambacho ni cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kikihusisha kilometa 205 za njia kuu na kilometa 95 za michepuko (Spurs) ni sehemu ya kilometa 1,219 zinazojengwa katika kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar-Tabora-Isaka-Mwanza.
Vipande vingine viwili – Morogoro-Makutupora na Isaka-Mwanza viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Februari 3, 2017 Serikali ilitiliana saini ya makubaliano ya ujenzi wa kipande cha reli katika mkataba wa ubia na kampuni za Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil Africa ya Ureno kwa gharama ya Dola 1.1 bilioni za Kimarekani (Shs.2.7 trilioni).
Katika mkataba huo, kampuni za Yapi Merkezi na Mota-Engil Africa kila moja ina asilimia 50 baada ya kushinda zabuni.
Ujenzi wa reli hiyo utaongeza chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na safari ya Dar es Salaam hadi Morogoro itatumia muda wa saa 1:16 wakati Dar es Salaam hadi Dodoma itatumia muda wa saa 2:30 na safari ya Dar hadi Mwanza itatumia muda wa saa 7:30.
Usafiri wa treni utakuwa ni wa haraka baada ya ule wa anga kuliko wa mabasi ambayo kwa kawaida yanatumia saa 3:15 kutoka Dar hadi Morogoro, saa 7:30 kutoka Dar hadi Dodoma na saa 14:00 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Ujenzi wa kipande cha Morogoro-Dodoma-Makutopora mkoani Singida (422km – ambapo 336km ni njia kuu na 86km za mchepuko) chenye stesheni nane unaendelea ukigharimu jumla ya Dola bilioni 1.46 (Shs.4.4 trilioni) ambao ni mkopo kutoka nje na ndani. Kampuni za Yapi Merkezi na Mota-Engil Africa ndizo zinazojenga pia kipande hiki.
Hata hivyo, ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar-Tabora-Isaka-Mwanza ni sehemu ya njia zote za Reli ya Kati inayohusisha jumla ya kilometa 2,561, ambapo kukamilika kwake kutarahisisha usafiri kwa nchi za Maziwa Makuu kama Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Njia hizo ni Tabora-Kigoma (411km); Kaliua-Mpanda (210km); Mpanda-Karema Port (111km), Uvinza-Kalelema Border (mpaka na Burundi – 203km); na Isaka-Keza/Rusumo-Ruvubu nchini Rwanda kilometa 407.
Reli ya zamani (hii inayotumika sasa) ilikuwa inaishia Mpanda, lakini tumeamua kuiongeza hadi Bandari ya Karema ambako itasaidia kubeba mizigo ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na abiria.
Aidha, mchepuko wa kutoka Uvinza hadi Kalelema kwenye mpaka na nchi ya Burundi nao utasaidia kutanua mtandao wa usafiri wa reli, kwani Warundi nao wataanza kujenga reli hiyo kutoka hapo mpakani hadi Gitega kupitia Musangati.
Kuhusu kipande cha Isaka-Keza, inaelezwa kwamba kutakuwa na makutano hapo Keza ambapo utakuwepo mchepuko wa kutoka Keza kupitia Kabanga (mpakani) hadi Gitega nchini Burundi, na kwamba kipande ambacho kitajengwa na Warundi ni kutoka Kabanga hadi Gitega.
Tanzania itajenga kipande cha Keza hadi Rusumo, mpakani na Rwanda, ambapo Wanyarwanda nao watajenga kipande cha kutoka hapo hadi Kigali.
Bajeti ya ujenzi wa reli hiyo kwa upande wa Tanzania itakuwa kiasi cha Shs. 16.7 trilioni (takriban Dola 7.5 bilioni za Marekani).
Sehemu ya Makutopora-Isaka kupitia Tabora yenye urefu wa 435km kutoka Makutopora bado haijapewa mkandarasi. Hapa Isaka njia za reli zitagawanywa; moja itaendelea hadi Mwanza ilhali mkono mwingine unatarajiwa kuendelea hadi Rusumo kwenye mpaka na Rwanda.
Hata hivyo, sehemu ya Isaka-Shinyanga-Mwanza yenye urefu wa 220km za njia kuu imepangwa kujengwa na makampuni mawili ya China ambayo ni China Civil Engineering Construction (CCEC) na China Railway Construction Company (CRCC).
Mkataba juu ya mradi huo wenye thamani ya Dola bilioni 1.37 ulitiwa saini Januari 2021 na mnamo Juni 14, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan akaweka jiwe la msingi kwa ujenzi mjini Mwanza.
Kipande cha reli kutoka Isaka-Rusumo kwenye mpaka wa Rwanda, na kuendelea hadi Kigali kina urefu wa 371km.
Ujenzi wa sehemu hii umekadiriwa kufika Dola milioni 942 za Marekani. Mnamo Aprili 2018 iliwahi kuripotiwa kwamba Benki ya Dunia ilikuwa imeonyesha nia ya kufadhili reli ya Isaka-Kigali Standard Gauge ambayo gharama yake ni Dola milioni 942.
Baada ya kumalizika kwa vipande hivyo, ujenzi wa vipande vya Tabora-Kigoma; Kaliua-Karema Port; Uvinza-Keza-Rusumo nao utaanza.
Awali, ujenzi wa reli yote ya kati ulikuwa ufanywe na kampuni ya Kichina ya China Railway Construction Corporation Limited (CRCC), lakini mchakato huo ukatenguliwa na kuanza upya baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani.
Upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli hiyo ulifanywa na kampuni ya Canarail kutoka Canada ukihusisha njia za Dar-Tabora, Isaka-Kigali, na Keza-Msongati.
Aidha, upembuzi wa njia ya Isaka-Mwanza ulifanywa na kampuni ya Cowi ya Denmark ambayo pia ilifanya kwa reli ya Tabora-Kigoma na Kaliua-Mpanda.
Kampuni ya Cowi pia ilifanya ubunifu wa msingi wa reli mpya kutoka Mpanda hadi Karema Port kwenye Ziwa Tanganyika, wakati ubunifu wa ujenzi wa reli kutoka Uvinza-Msongati nchini Burundi ulifanywa na kampuni ya HP Gauff ya Ujerumani.
Serikali pia ina mpango wa kuifufua njia ya reli ya kutoka Manyoni hadi Singida yenye urefu wa kilometa 115 pamoja na kipande cha kilometa 108 kutoka Kilosa hadi Kidatu kuunganisha na Reli ya Tazara katika jitihada zake za kuimarisha miundombinu ya reli nchini.
Kwa upande mwingine, Reli ya Kaskazini, zamani ikijulikana kama Reli ya Usambara, ndiyo reli ya kwanza kabisa kujengwa Tanganyika chini ya ukoloni wa Mjerumani ambayo ilianza mwaka 1891 hadi 1913 kabla ya kusimama kutokana na kuzuka kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, lakini baadaye ikamaliziwa na Waingereza mwaka 1929 ilipofika Arusha.
Reli hiyo ambayo kwa sasa imekufa tangu Shirika la Reli Tanzania lilipobinafsishwa mwaka 2007, sasa itajengwa tena kutoka Tanga hadi Arusha (438km) na baadaye Arusha hadi Musoma (670km) na hivyo kuunganisha eneo la Kaskazini na Ziwa Victoria.
Vile vile, kipande cha reli kutoka Ruvu hadi Tanga (569km) nacho kitatengenezwa.
Kukamilika kwa Reli ya Kaskazini kutasaidia kukuza utalii katika eneo hilo maarufu hasa kwa Hifadhi za Taifa nyingi kama Mkomazi, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Tarangire, Ngorongoro na Serengeti.
Lakini pia itakuza uchumi kutokana na kuwepo kwa machimbo ya magadi katika eneo la Engaruka pamoja na fosfeti kule Minjingu.
Uchunguzi unaonyesha kwamba, hivi sasa upembuzi yakinifu unaendelea katika baadhi ya vipande vya Reli ya Kaskazini (zamani ikifahamika kama Reli ya Usambara) kwa kuiboresha kuwa ya kisasa kutoka Ruvu-Mruazi (188km) na Tanga-Moshi-Arusha (438km).
Mpango huo ni pamoja na kujenga reli mpya kutoka Arusha-Musoma (600km) pamoja na tawi la kilometa 70 kwenda Shinyanga kuungana na Reli ya Kati, lakini pia kutakuwa na kipande cha kutoka Ziwa Manyara hadi Ziwa Magadi kwenye machimbo ya magadi katika eneo la Engaruka pamoja na fosfeti huko Minjingu.
Ujenzi wa Reli ya Kusini kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa umbali wa 860km, pamoja na tawi lake la 200km kwenda kwenye mgodi wa makaa ya mawe huko Mchuchuma na mgodi wa chuma huko Liganga ndio unaosubiriwa na wananchi wengi wa Kusini mwa Tanzania.
Mradi huo ambao uko katika hatua ya ubunifu wa ujenzi chini ya mshauri mwelekezi kampuni ya Dong Myeong Engineering Consultant ya Korea Kusini unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani 3.6 bilioni (takriban Shs. 7.2 trilioni) na utajengwa na kampuni ya China Railway No. 2 Engineering Group (CREGC) ambayo ni kampuni tanzu ya China Railway Group Limited.
Umuhimu wa reli hiyo ni mkubwa kwani maeneo ya kusini mbali ya kuwa na utajiri wa mafuta na gesi, lakini pia kuna hazina kubwa ya madini iliyoko Mchuchuma na Liganga wilayani Ludewa. Mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma unakadiliwa kuwa na hazina ya tani 540 milioni wakati hazina ya chuma cha pua iliyopo Liganga inakadiliwa kuwa tani 45 milioni.
Taarifa kutoka Serikali Kuu zinasema ujenzi wa reli ya Mtwara-Mbamba Bay-Mchuchuma unatafungua fursa za maendeleo katika Ushoroba wa Maendeleo Mtwara (MDC) unaohusisha mikoa nane ambayo ina idadi ya watu 9,432,285 (karibu 21.6% ya Watanzania wote), na pia kukuza mtandao wa biashara kati ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na Zambia kwa kupunguza gharama za usafirishaji na kuboresha uchumi kwa bidhaa za ndani na nje.
Malawi kwa kiasi kikubwa inategemea njia mbili za reli zinazoiunganisha na bandari katika Bahari ya Hindi – Reli ya Trans-Zambezia yenye urefu wa 269km ikitokea kwenye ukingo wa kusini wa Mto Zambezi hadi kwenye reli kuu ya kutoka Beira kwenda Zambia, na reli ya kwenda bandari ya Nacala nchini Msumbiji, hivyo endapo reli ya Mtwara-Mbamba Bay itajengwa inaweza kuisaidia Malawi kwa kiasi kikubwa.
Rasilimali za madini kusini mwa Tanzania, hususan katika Ushoroba wa Maendeleo wa Mtwara, ni nyingi kwa sasa na kwa mujibu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), huku kampuni nyingi za kigeni zikiwa zimeingia mikataba mbalimbali ya uchimbaji na utafiti.
Katika Pori la Akiba la Selous ambalo ni Urithi wa Dunia, tayari uchimbaji wa urani kwenye Mto Mkuju wilayani Namtumbo umekwishaanza tangu mwaka 2013 chini ya kampuni ya Uranium One inayomilikiwa na kampuni ya Atomredmetzoloto (ARMZ) iliyo chini ya Rosatom State Atomic Energy Corporation inayomilikiwa na serikali ya Russia.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Uranium One iliyofanya utafiti katika eneo hilo, Chris Sattler, alikaririwa Juni 21, 2011 akisema kiwango cha uzalishaji wa urani kinaweza kuwa kati ya tani 1,900 na 2,700 kwa mwaka, lakini kwa wastani unaweza kuzalisha tani 1,600 za urani ya manjano (yellowcake) kwa gharama ya Shs. 34,545 kwa paundi moja, hivyo kuifanya Tanzania nchi ya tatu kwa uzalishaji wa urani barani Afrika.
Wakati akizindua ofisi mpya za Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC) jijini Arusha Mei 7, 2010, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema Tanzania ilikuwa inaingia katika orodha ya nchi zinazozalisha kwa wingi urani duniani.
“Kama akiba yote tuliyonayo itatumiwa vizuri, Tanzania itakuwa nchi ya saba duniani kwa uzalishaji wa urani,” alisema Kikwete. Kwa ujumla, Tanzania ina akiba ya tani 20,769 za urani ghafi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka NDC, kuna maeneo yenye makaa ya mawe Mbamba Bay kwenye ukingo wa Ziwa Nyasa ambayo yana hazina ya tani 29 milioni ingawa iliyothibitishwa ni tani 2.4 milioni ambazo zinaweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo na kuzalisha tani 75,000 za ujazo kwa mwaka, hivyo kuzalisha Shs. 4.2 bilioni kwa mwaka.
Takwimu hizo zinathibitisha kuwepo kwa makaa ya mawe Namwele-Nkomolo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa wenye tani 1.5 milioni zilizothibitishwa na hazina ya tani 17.2 milioni ambazo zinaweza kuzalisha Shs. 19.8 bilioni kwa mwaka. Utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Edenville Energy ambayo pia ndiyo iliyofanya utafiti katika maeneo ya Muze.
“Mradi wa makaa ya mawe wa Muze ambao unaweza kuzalisha umeme kwenye ukingo wa Ziwa Rukwa una akiba ya tani 3.41 milioni na hazina ya tani 56.59 milioni ambazo zinaweza kuzalisha 300MW za umeme. Pato la mwaka linakadiriwa kufikia Shs. 188.4 bilioni,” takwimu hizo zinaonyesha.
Watafiti wanasema kwamba, endapo serikali itajenga kilometa hizo za reli na kuboresha huduma katika Reli ya Uhuru (Reli ya Tazara) yenye urefu wa 1,860km kutoka Dar es Salaam hadi New Kapri Mposhi kule Zambia, pato la taifa linaweza kuongezeka kwa usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na kuchochea maendeleo kwa wananchi wa Korido ya Maendeleo ya Mtwara.
0629-299688

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *