Samia anavyohimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kimataifa

Na Daniel Mbega, Dar es Salaam

“KISWAHILI ni Lugha ya Ukombozi, ni Lugha ya Umoja, ni Lugha ya Amani na ni Lugha ya Biashara.”

Hii ni kauli thabiti ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa hotuba yake ya maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani, Julai 7, 2024.

Maadhimisho ya lugha ya Kiswahili Duniani yalitangazwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mnamo Julai Mosi, 2021, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja lilipopitisha azimio la kuitambua Julai 7 kuwa Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kiswahili.

Tanzania, kama nchi zingine katika Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kiswahili Julai 7, 2024, Rais Samia amezungumzia Kiswahili kama lugha iliyotumika wakati wa ukombozi wa Uhuru wa Tanganyika, Zanzibar, Kenya na nchi zingine za Afrika.

Ikumbukwe kwamba, Mnamo Julai 7, 1954, siku ambayo chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilizaliwa rasmi, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alishawishi na kupitisha lugha ya Kiswahili kama lugha ya ukombozi ya Waafrika.

Jomo Kenyatta au kwa jinale la asili ‘Kamau wa Muigai’ au kwa jina la ubatizo ‘Jonstone Kamau’, rais wa kwanza wa Kenya, akafuata nyayo za Nyerere na kutumia Kiswahili kuwaunganisha Wakenya katika harakati za kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni akitumia neno maarufu la ‘Harambee’ kama kauli mbiu yake.

Kwahiyo, Umoja wa Mataifa ulipoiweka Julai 7 ya kila mwaka kama siku maalum ya Lugha ya Umoja wa Kimataifa ya Kiswahili – kwa makusudi au kwa bahati mbaya – ulirejea siku ambayo lugha hiyo ilipitishwa rasmi na TANU kama lugha rasmi ya mapambano na ukombozi.

Kwa kipindi hicho, ukombozi unaozungumzwa ulikuwa ni wa kumuondoa Mwingereza na kuifanya Tanzania huru. Lakini leo hii Rais Samia anapoendelea kuhimiza matumizi ya lugha hii adhimu, anamaanisha azma ile ile ya Mwalimu Nyerere, ambaye kwa kutumia Kiswahili alileta ukombozi wa fikra, ukombozi wa kielimu, kiutamaduni, kiafya, kiuchumi na maendeleo kwa ujumla.

Rais Samia anaendelea kusafiri kwenye azma ya Nyerere, ambaye kupitia Kiswahili alileta umoja, amani, mshikamano na udugu ambao umeifanya Tanzania iwe namna ilivyo leo hii.

Mwanasiasa wa upinzani kutoka Afrika Kusini wa chama cha The Economic Freedom Fighters, Julius Sello Malema, alipata kusema kuhusu, njia bora ya kuwaunganisha Waafrika na kuachana na lugha zenye mizizi ya ukoloni:

“Jambo la maana kufanya, ikiwa tunataka kuliunganisha bara la Afrika, ni kukifundisha Kiswahili na kuzihimiza nchi nyingine kufundisha Kiswahili. Jambo la msingi ni mawasiliano.”

Elliot Berry almaarufu kama ‘mzungu mwitu’ ama ‘mwalimu wa Kiswahili’ ni mzaliwa wa Uingereza lakini amepata umaarufu nchini Kenya kwa ujuzi wake wa lugha ya Kiswahili japokuwa lafudhi yake imeshangaza wengi kwani ni ya jamii ya Waluhya kutoka Magharibi mwa Kenya.

Yeye anasema: “Lugha ya Kiswahili ni tamu… pia kuna maneno ambayo ukisema na kizungu, hayavutii kama vile ukisema kwa Kiswahili.”

Ukuaji wa Kiswahili

Umoja wa Mataifa haukukosea kukifanya Kiswahili kama lugha rasmi ya umoja huo, kama ilivyo kwa Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa sababu lugha hiyo inazungumzwa na watu wengi katika ukanda wote wa Pwani ya Bahari ya Hindi na mataifa ya jirani.

Kinazungumzwa sana nchini Tanzania, Kenya, Msumbiji na Uganda, lakini kinazungumzwa pia katika mataifa ya Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku idadi ya wazungumzaji wa asili ikitajwa kuwa milioni 200 na milioni 300 wengine ambao wanaichukulia kama lugha ya pili ya mawasiliano.

Mwaka 2015 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilianzisha Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (EAKC) ambayo imekuwa kama chombo kinara katika kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kwenye ukanda wote wa Afrika Mashariki pamoja na kuratibu maendeleo na ushirikiano.

Katika miaka ya karibuni, nchi kama Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Ethiopia na Sudan Kusini zimeanza kufundisha Kiswahili kama somo rasmi kwenye shule na zimeandaa mipango kamambe ya kukiendeleza.

Wanamapinduzi wote wa Kusini mwa Afrika waliishi Tanzania, nchi ambayo ilisaidia kupambana kudai uhuru wa mataifa mengi Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa maana hiyo, wengi wanafahamu umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika kuleta mapinduzi, uhuru na umoja.

Shikomor, lugha rasmi ya Visiwa vya Comoro na ile inayozungumzwa Mayotte (Shimaore), zinafanana kwa karibu na Kiswahili na wakati mwingine hutajwa kwamba ni lahaja za Kiswahili.

Kiswahili kipo katika kundi la lugha za Niger-Kongo na asili yake ni lugha ya biashara iliyoanzia Mashariki mwa Afrika na kaskazini mwa pwani ya Madagascar.

Niger-Kongo ni familia ya lugha dhahania zinazozungumzwa na sehemu kubwa ya Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, lakini miongoni mwa lugha hizo, Kiswahili ndicho kinazungumzwa na watu wengi zaidi.

Lugha nyingine katika familia hii ni Kikongo cha Kiatlantic, Kikongo cha Volta, Kikongo cha Benue, Kibantoid, Kibantoid cha Kusini, Kibantu, Kibantu za Kaskazini-Mashariki, Kibantu cha Pwani ya Kaskazini-Mashariki, na Kisabaki kinachozungumzwa ukanda wa Mto Tana na Mijikenda nchini Kenya.

Ukiacha Kiswahili, lugha nyingine za familia ya Niger-Kongo zinazozungumzwa sana na wenyeji ni Kiyoruba, Kigbo, Kifula, Kilingala, Kiewe, Kifon, Kiga-Dangme, Kishona, Kisesotho, Kixhosa, Kizulu, Kiakan, na Kimooré.

Lugha ya saba ya Umoja wa Mataifa

Kupitishwa kwa Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kiswahili ni mafanikio makubwa sana, kwani ndiyo lugha ya kwanza ya Kiafrika kuwemo kwenye orodha ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa, ikiwa ya saba. Lugha nyingine ni Kichina, Kihispaniola, Kiingereza, Kirusi, Kiarabu na Kifaransa, ambazo zinatumika kwenye mikutano na nyaraka rasmi za Umoja wa Mataifa wenye wanachama 193.

Kichina, au Mandarin Chinese, ndiyo lugha inayoongoza duniani kuzungumzwa na watu wengi na ndiyo lugha ya taifa ya China ikiwa na asili ya Wachina wa Enzi ya Han. Kwa sasa inazungumzwa na watu bilioni 1.35, au 17% ya idadi ya watu ulimwenguni.

Siku ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kichina ilipitishwa rasmi Novemba 12, 2010 na Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa, ambapo huadhimishwa kila tarehe 20 Aprili ya kila mwaka. Siku hii ilichaguliwa ili kumuenzi Cangjie, mtu anayetajwa kwamba ndiye aliyeanzisha herufi za Kichina takriban miaka 5,000 iliyopita. Maadhimisho ya kwanza yalifanyika Aprili 20, 2011.

Kihispaniola ndiyo lugha ya pili ya asili inayofuatia kwa kuzungumzwa na watu wengi duniani baada ya Kichina, ikiwa inazungumzwa na watu wa asili milioni 500 hususan Amerika Kusini na Hispania kwenyewe, lakini na wengine milioni 600 wanaoitumia kama lugha ya pili. Kihispaniola ni lugha rasmi katika mataifa 20. Lakini ni lugha ya nne inayozungumza na watu wengi duniani baada ya Kiingereza, Kichina, na Kihindustani (Hindi-Urdu).

Mnamo Oktoba 10, 2010, Umoja wa Mataifa ulipitia tarehe 23 Aprili ya kila mwaka kama Siku ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kihispaniola ili kutoa heshima kwa mwandishi wa Kihispaniola, Miguel de Cervantes Saavedra, aliyefariki duniani 22 Aprili 1616.

Kiingereza (hasa za Uingereza chenye tahajia ya Oxford) ndiyo lugha ya taifa ya Uingereza na Marekani. Ndiyo lugha maarufu kuliko zote ulimwenguni miongoni mwa lingua franca n ani lugha rasmi katika nchi 58 na maeneo 31 ambayo hayana uhuru kama maraifa, hususan yale ambayo yako chini ya Jumuiya ya Madola.

Kiingereza, ambacho asili yake ni Kijerumani Magharibi, ilipitishwa rasmi na Umoja wa Mataifa Oktoba 10, 2010 kusherehekea ‘kusherehekea lugha nyingi na tofauti za kitamaduni’, ambapo tangu wakati huo Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kiingereza hufanyika kila Aprili 23, ambayo ilichaguliwa kukumbuka siku aliyokufa William Shakespeare, mwandishi mashuhuri wa Kiingereza.

Kifaransa, ingawa ndiyo lugha rasmi ya Ufaransa, lakini ni lugha rasmi ya mataifa 27, hususan barani Afrika. Kifaransa pia ni mojawapo ya lugha zinazosambaa sana duniani ambapo nchi takriban 50 zinaitumia kama lugha rasmi ya mawasiliano au ndiyo lugha ya taifa.

Inazungumzwa kama lugha ya kwanza nchini Ufaransa, Canada (hususan kwenye majimbo ya Quebec, Ontario, na New Brunswick); Ubelgiji (Wallonia na Brussels); magharibi mwa Uswizi (hususan katika eneo la Romandy); sehemu za Luxembourg; sehemu za Marekani (majimbo ya Louisiana, Maine, New Hampshire, nd Vermont); Monaco; Bonde la Aosta Valley nchini Italia; na maeneo mengine ulimwenguni.

Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa uliipitisha Machi 20 ya kila mwaka kama siku ya kuadhimisha Kifaransa. Siku hiyo ilichaguliwa kwa vile ilikuwa “inalingana na kumbukumbu ya miaka 40 ya Shirika la Kimataifa la La Francophonie”, kikundi ambacho wanachama wake wanazungumza lugha moja, pamoja na maadili ya kibinadamu yanayokuzwa na lugha ya Kifaransa.

Kirusi, ambacho asili yake ni lugha ya Slavic ya Mashariki, ndiyo lugha rasmi iliyozungumzwa katika iliyokuwa Umoja wa Kisovieti wa Kisoshalisti (USSR). Kwa sasa ndiyo lugha rasmi katika mataifa ya Russia, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, na Tajikistan, na bado inaendelea kutumika katika mataifa ya Ukraine, Moldova, Caucasus, Asia ya Kati, na katika baadhi ya mataifa ya Baltic na Israel. Lugha hii inazungumzwa na watu milioni 258 ulimwenguni kote.

Mnamo Februari 2010, Umoja wa Mataifa uliipitisha Juni 6 ya kila mwaka kuwa Siku ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kirusi. Siku ya Lugha ya Kirusi ya Umoja wa Mataifa inaambatana na siku ya kuzaliwa ya Alexander Pushkin, mshairi wa Kirusi ambaye anachukuliwa kuwa baba wa lugha ya kisasa ya Kirusi.

Kiarabu, ambayo ni moja ya lugha za kale ikiwa inazungumzwa sana Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika kama lugha ya taifa kwa baadhi ya mataifa, ni lugha ya tatu miongoni mwa lugha zilizosambaa sana ikiwa pia lugha ya liturgia katika Dini ya Kiislamu.

Wakati wa Zama za Kati, Kiarabu ndiyo ilikuwa nyenzo muhimu ya utamaduni, hususan katika sayansi, hisabati na falsafa. Matokeo yake, lugha nyingi za Ulaya zikakopa maneno mengi kutoka kwenye Kiarabu, kama ilivyokuwa kwa lugha ya Kiswahili.

Mwaka 2010, Umoja wa Mataifa uliipitisha Desemba 18 kama siku maalumu ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kiarabu. Desemba 18 ilichaguliwa kuwa tarehe rasmi ya Lugha ya Kiarabu kwani ndiyo “siku ambayo katika mwaka 1973 Baraza Kuu la UN liliidhinisha Kiarabu kama lugha rasmi ya Umoja wa Mataifa”.

Ingawa si mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa, lakini mnamo Novemba 2019, wakati wa Mkutano Mkuu wa 40 wa UNESCO, waliamua kuipitisha Mei 5 ya kila mwaka kama Siku ya Lugha ya Kireno Duniani. Hata hivyo, siku hiyo (Dia Mundial da Língua Portuguesa) ilikuwa imeanza kuadhimishwa tangu Mei 5, 2009 kama Siku ya Utamaduni na Lugha ya Kireno.

Mwaka huu Siku ya Kiswahili Duniani, iliadhimishwa Julai 5, 2024, katika makao makuu ya Unesco huko Paris, Ufaransa chini ya kauli mbiu, “Kiswahili: Elimu na Utamaduni wa Amani.”

Utamaduni wa amani, ndipo hasa penye msingi wa makala yenyewe. Katika nchi kama Tanzania, ambapo Kiswahili kinaunganisha makabila zaidi ya 100, kuna hadithi tofauti na ile iliyopo Uganda ambako wanadai Kiswahili kilitumiwa na watu ‘wauaji’.

Kwa Tanzania, Kiswahili ni mfano wa lugha ambayo ni chanzo cha mshikamano kwenye taifa lenye watu wenye kutofauatiana mambo mengi ya kimila na kitamaduni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *