Na Mwandishi Wetu
MOJA ya mambo yanayopeperusha vema bendera ya Tanzania katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni utulivu wake kisiasa, ukuaji haraka wa uchumi na eneo kubwa la uwekezaji katika kilimo na kasi ya ongezeko la viwanda.
Hii ni kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, akiendeleza yale yaliyofanywa na watangulizi wake katika kuhakikisha anapambania kukua kwa uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kukuza diplomasia ya uchumi, kujenga uchumi fungamanishi na shirikishi kwa jamii, pamoja na kutenga bajeti kubwa katika sekta za kimkakati kama miundombinu, nishati na kilimo, ni mambo ambayo yanawavutia wawekezaji wengi wa ndani na nje kuingiza fedha zao.
Huenda mambo haya yasingefikiriwa sana wakati wazo la kuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki linaletwa mwaka 1967 na viongozi wa nchi tatu za Tanzania, Uganda na Kenya. Kwa sababu mbali ya mambo mengine, Kenya ilikuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo kwa nyanja zote.
Baadaye jumuiya hii ilivunjika mwaka 1977 na kurejea tena Julai 7, 2000 kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Lakini sasa hamu ya mataifa jirani kuwa sehemu ya mtangamano imeongezeka zaidi.
Mpaka sasa kuna nchi saba katika mtangamano huu ambapo mbali ya Tanzania, Kenya na Uganda, pia zimo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sudani ya Kusini. Makao makuu ya mtangamano huu yapo jijini Arusha, Tanzania.
Kuna mambo mengi yamepita kati ya mwaka 2000 hadi 2023 kuhakikisha kunakuwa na mambo mazuri baina ya nchi hizi ikiwemo kuwa na Mamlaka ya Shirikisho la Afrika Mashariki hadi kuwa na Dola moja.
Mwaka 2013 kulizinduliwa soko la pamoja, ajira na mtaji ndani ya kanda kwa lengo la kuwa na sarafu ya pamoja.
Mwaka 2013 ilisainiwa itifaki ya pamoja ili kuwa na sarafu ya Afrika Mashariki ndani ya miaka 10, mnamo mwaka 2018 kamati iliundwa kuanza taratibu za kuandaa Katiba. Hata hivyo, hakuna kilichofanyika hadi sasa.
Mivutano ya hapa na pale imekosa jibu la pamoja lakini hii yote ni kutokana na maslahi ya kila nchi kutaka kuwa ya kwanza kabla ya kuhakikisha maslahi ya pamoja.
Aidha, zipo hofu za hapa na pale pengine kati ya mataifa yote wanachama au kwa baadhi ya nchi kutokana na fursa zilizopo, wengi wakiamini baadhi ya nchi zinazimeza nchi nyingine.
Kwa mfano, ukiondoa nchi ya DRC, ambayo ndiyo inayoongoza kwa ukubwa katika utangamano huu ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba milioni 2.345, Tanzania inashika nafasi ya pili ikiwa na kilomita za mraba 945,087.
Kenya ina kilomita za mraba 582,646, Uganda ni kilomita za mraba 241,038, Burundi kilomita za mraba 27,834, Rwanda kilomita za mraba 26,338 na Sudani ya Kusini ina kilomita za mraba 644,329.
Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika zenye eneo kubwa lililo na utajiri wa rutuba kwa ajili ya kilimo cha mazao ya aina yoyote, kuanzia nafaka, matunda na mazao ya biashara kama Mkonge na miti.
Mei 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Geoffrey Kirenga, alipata kutamka maneno ya kutia faraja kwa Tanzania juu ya kilimo.
Alisema: “Asilimia 50 ya ardhi inayofaa kwa kilimo barani Afrika iko Tanzania, Zambia na Msumbiji. Ardhi yetu inafaa kwa kilimo, tangu Kaskazini hadi Kusini mwa nchi.”
Pengine pambo hili linawatamanisha majirani zetu wengi kwa kiwango kikubwa, lakini kama hiyo haitoshi, Tanzania imejizatiti katika kuimarisha mazingira ya biashara kwa wageni na wenyeji.
Mazingira ya biashara na uwekezaji kwa sasa ni mazuri kuliko ilivyokuwa nyuma maana kero nyingi za kibiashara zimetatuliwa na kubwa zaidi, wafanyabiashara wadogo, wa kati na hata wakubwa nchini wanahimizwa wazingatie ubora ili kukabili ushindani katika soko la EAC.
Katika hatua nyingine, fursa za jumla za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kuwa tishio si tu kwa Afrika bali kwa dunia nzima. Nchi hizi zikiamua kuungana kwa dhati na kushirikiana moja kwa moja kwenye nyanja zote na kuamua kuwa nchi moja, itakuwa nchi ya saba yenye nguvu duniani.
Kwa mujibu wa makadirio ya takwimu za mwaka 2022, nchi hizi saba, yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC na Sudani ya Kusini zikiungana zitakuwa na ukubwa kwa kilomota za mraba 4,819,363 na wakazi zaidi ya 281,050,447, ikiongozwa na Urusi, Canada, Marekani, China, Brazil na Australia.
Katika nyanja ya biashara Tanzania inazidi kufanya vizuri ukilinganisha na mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hii pengine ni faida ya kutojifungia mipaka katika kipindi cha Uviko-19. Nchi nyingi zilitetereka duniani lakini Tanzania ilibaki imara.
Kwa mfano, takwimu za mwaka 2020 zinaonyesha kuwa jumla ya biashara ya Tanzania na Nchi Wanachama wa EAC ilifikia Dola za Marekani milioni 1,136.9, zaidi ya Dola za Marekani milioni 1,003.6 mwaka 2019.
Huenda hapa katikati takwimu zikabadilika kulingana na mabadiliko ya fedha za kigeni na mtikisiko wa kiuchumi kwa sababu mbalimbali ikiwemo uhaba wa mafuta na vita vya Ukraine na Urusi vilivyotikisa maeneo mengi ya dunia.
Hata hivyo, bado Tanzania inabaki kuwa sehemu salama zaidi kiuwekezaji kwa sababu ya kuimarika hali ya kisiasa kulikoongeza utulivu wa wananchi na kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani maradufu.
Jitihada kubwa za Rais Samia katika kuwavutia wawekezaji na kuitangaza Tanzania kwenye uga wa kimataifa zimefanya mataifa mengi kuifuatilia nchi hii kuangalia fursa zilizopo, na wanapothibitisha kinachosemwa na mkuu wa nchi hawasiti kuja kuwekeza.
Kwa kawaida wageni wanapenda maeneo yenye amani, utulivu na usikilizano. Tanzania inajipambanua kwa sifa hiyo kwa miaka mingi.
Ukiondoa vurugu za kudai uhuru na vita vya wenyeji kupambana dhidi ya wageni weupe miaka ya nyuma, Tanzania haijawahi kuingia kwenye vurugu za aina yoyote zaidi ya vita dhidi ya Nduli Idd Amin wa Uganda mnamo mwaka 1979.
Kama hiyo haitoshi, Tanzania imekuwa msafirishaji mkubwa wa nafaka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ikiwamo Mchele, Mahindi, Mtama, Ufuta, Korosho na katika mifugo bado sifa yake iko palepale kuwa ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia.
Takwimu zinaonyesha Tanzania inamiliki robo tatu ya mifugo yote iliyopo barani Afrika. Kwa mujibu wa sensa ya taifa ya kilimo mwaka 2019/20 Tanzania ina Ng’ombe milioni 33.9, Mbuzi milioni 24.5, Kondoo milioni 8.5 na Kuku milioni 87.7.
Hizi zote ni fursa zinazoifanya Tanzania kutembea kifua mbele kwenye mtangamano huu, wananchi wa Tanzania hawana budi kuitumia nafasi hii kujitajirisha kwa sababu kupitia soko la pamoja bidhaa nyingi muhimu zitatoka katika ardhi ya Tanzania kulisha midomo 281,050,447.