*Vigogo wahofiwa kuhamia CCM, kisa…
*Wengi wakoshwa na kasi ya maendeleo
Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam
WIMBI la baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani vikiwemo NCCR-Mageuzi, CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na ACT-Wazalendo kuachia nafasi zao na kujiunga CCM lipo mbioni kujirudia.
Mwaka 2016 wakati wa utawala wa Hayati Dkt. John Magufuli, viongozi mbalimbali wa upinzani wakiwemo wabunge na madiwani, waliachia nafasi zao na kujiunga CCM wakitoa sababu mbalimbali.
Sababu kubwa ni kuiunga mkono serikali ya Hayati Dkt. Magufuli kutokana na mapinduzi ya maendeleo ambayo alikuwa akiyafanya katika utawala wake.
Baada ya Rais Dkt. Samia kuingia madarakani Machi 19, 2021, kasi ya maendeleo imeongezeka mara dufu.
Rais Dkt. Samia ameongeza kasi ya utekelezaji miradi ambayo aliikuta na kuanzisha mingine ambayo imekuwa na tija kubwa kwa maslahi ya nchi na Watanzania.
Sifa kubwa inayomfanya Rais Dkt. Samia akubalike katika uongozi wake ni uzalendo alionao, uongozi bora, kusimamia haki bila kujali itikadi za kisiasa.
Pia mapinduzi makubwa ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu, kilimo, maji, teknolojia, barabara ni mtaji mkubwa wa CCM juu ya kukubalika na wananchi.
Wakati Rais Dkt. Samia akiendelea kutekeleza miradi inayowagua wananchi moja kwa moja, taarifa zinasema ndani ya vyama hivyo (upinzani), baadhi ya viongozi kutoka ngazi ya Wilaya, Mkoa, Kanda wamepanga kuachia nafasi zao na kujiunga CCM.
Hatua hiyo inatokana na viongozi hao kufurahishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia akisimamia haki, demokrasia na utawala bora.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Leo, umebaini kuwa, viongozi hao wameanza kuukubali uongozi wa Rais Dkt. Samia kupitia vikao vyao vya ndani.
Taarifa zinasema, baadhi ya viongozi hao wameanza kugawanyika, wengi wao wakiukubali uongozi wa Rais Dkt. Samia na chama tawala CCM jinsi kinavyoisimamia serikali, kutekelezani ilani ya chama chao kwa vitendo.
Baadhi ya viongozi hao wanasema, baada ya Rais Dkt. Samia kuingia madarakani, walitegemea kukiona CCM kikipoteza mwelekeo lakini hali imekuwa tofauti.
“Hali imekuwa tofauti kabisa, tunaiona CCM ambayo imebeba jukumu la kuisimamia serikali, kufuatilia uhai wa chama, utekelezaji wa miradi iliyopo kwenye ilani kwa kushirikisha wananchi wa maeneo husika.
“Ushirikishaji huo haubagui chama cha siasa, hata sisi wapinzani tunashirikishwa, hii ndiyo siasa tuliyoitamani na kuipigania miaka mingi, mkombozi amepatikana, hatuna sababu ya kutomuunga mkono.
“Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, CCM kitapata ushindi wa kishindo, kazi ya kuijenga nchi sio ndogo,” alisema kiongozi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini (jina tunalo).
Kauli ya kiongozi huyo imeungwa mkono na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdallah Juma Sadala (Mabodi) aliyesema, CCM kimejihakikishia ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.
Mabodi alisema, imani hiyo inatokana na kazi kubwa, nzuri inayofanywa na Rais Dkt. Samia pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambao wanasimamia utekelezwaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Aliwapongeza viongozi hao kwa kutekeleza miradi ya maendeleo iliyopo kwenye Ilani ya CCM na mingine mingi ambayo haipo katika ilani ili kuongeza kasi ya mapinduzi makubwa ya kijamii na kiuchumi.
Wapo viongozi wengi kutoka upinzania wanaomuunga mkono Rais Dkt. Samia ambaye dhamira yake ni kuwaletea Watanzania maendeleo ya kiuchumi, kijamii mijini, vijijini na kuwapatia huduma bora.