Samia ‘afunika’ Singida, Tabora

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

BAADA ya maadhimisho ya Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, mkoani Manyara Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alianza ziara katika Mikoa ya Singida na Tabora.

Okotba 15, 2023 Rais Samia alianza ziara ya kikazi mkoani Singida ambapo akiwa njiani alisalimiana na wananchi waliokuwa wamejipanga kwa ajili ya kumkaribisha.

Rais Samia amemaliza ziara yake ya siku 4 katika Mikoa ya Singida na Tabora huku akishuhudia mabilioni ya fedha alizotoa yakiwa yamebadilisha mikoa hiyo katika kila Nyanja ya maendeleo ya wananchi.

Kutokana na mabadiliko ya Mikoa hiyo, Rais Samia amewaachia neno kwamba, kwenye uchaguzi wa mwaka 2024 wachague viongozi watakaowatumikia.

“Tunapoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, nawaomba mchague viongozi watakaowatumikia, tujitahidi kujiepusha na makundi, uchaguzi pia una mkono wa Mungu, unaweza ukaitaka nafasi ya uongozi lakini Mungu hakukupangia, hivyo unapokosa usianze kutengeneza makundi tukaanza kubomoa chama chetu.

“Kuweka chuki na kufanya maendeleo yasipatikane, nawaomba dumisheni, upendo, umoja na mshikamano tufanye chaguzi zetu vizuri,” alisema Rais Samia akiwa Singida siku ya pili ya ziara yake.

Ziara ya Rais Samia katika Mikoa hiyo iliandika historia kubwa ambayo wananchi hawataisahau kwasababu walipata fursa ya kumuona Rais Samia na kumsikiliza.

Wakati akielekea Singida akitokea Manyara, shanwe na nderemo zilitolewa kwa wananchi pale ambapo Rais Samia aliposimama eneo la Katesh na kuzungumza nao.

Wananchi waliojitokeza kwa wingi bila hiyana kumlaki kwasababu wengine hawakuwahi kumuona zaidi ya kwenye televisheni na picha, wakitumia bendera, mabango na nyimbo za kilugha.

Akiwa mpakani mwa Manyara na Singida eneo la Sagara, Wananchi wa eneo hilo walionesha shauku ya kusalimiana naye ambapo ilimpasa kusimama ili walau kuzungumza nao na kuwasikia.

Rais Samia alianza ziara yake kwa kuzindua shule ya Msingi Imbele, mabweni ya madarasa ya Shule ya Sekondari Mwanamwema Shein kwa Niaba ya Shule Mpya 302 zilizojengwa nchi nzima kupitia mradi wa kuinua elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo ametoa wito kwa Wazazi kuwapeleka wototo Shule.

Rais Samia alisema lengo la mradi huo ni kuondoa msongamano katika madarasa ili kuongeza tija na ufanisi kwenye ufundishaji kutoka wanafunzi 120 kwa darasa hadi kufikia 45.

Alisema serikali imejenga shule kuanzia awali hadi sekondari bila kuchangisha hata shilingi na pia imeondoa ada hivyo wazazi wanawajibika kwa kununua sare na vifaa vya shule.

“Isingekuwa miradi hii ya Elimu wazazi mngetoa fedha nyingi sana kujenga shule lakini pia kulipa ada ya mtoto, hii ina maana kwamba Serikali imekuachia kipato chako ubaki nacho mfukoni, Serikali Ile gharama inabeba yenyewe ni kama Serikali inalipa mshahara kwa kila mzazi,” alisema.

Rais Samia alifanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Polisi Square wilayani Manyoni ambapo aliweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara ya Kiwango cha lami barabara ya Mkiwa-Itigi-Noranga (56.9) kwa kiwango cha lami yenye thamani y ash bilioni 67.2 ambayo ni sehemu ya barabara ya Makongoroshi -Rungwa-Itigi-Mkiwa (413km)

Ujenzi wa barabara hiyo, licha ya kuunganisha ushoroba wa Tanzania na Zambia pamoja na wa Kati itaunganisha pia Tanzania na Ukanda wa SADC na hivyo kuchochea shughuli za uzalishaji na biashara kwa kurahisisha usafiri na usafirishaji.

Akiwa Itigi wananchi walipanda juu ya miti kwa lengo la kumuona Rais na kuzungumza na wananchi wa Jimbo la Singida mashariki eneo la Puma.

Siku hiyo hiyo, Rais Samia alizindua jengo la Kituo cha polisi cha Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa kuwakilisha ufunguzi wa vituo vingine vya polisi Wilaya ya Ikungi pamoja na Mkalama.

Oktoba 16, 2023 Rais Samia alizindua daraja la Msingi lenye urefu wa mita 100 lililopo Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, lililogharimu Shs. bilioni 11.2.

Alisema daraja hilo lina umuhimu kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa wa Singida na Mikoa ya jirani ya Simiyu, Mwanza, Mara, Manyara, Arusha na maeneo mengine ya nchi.

Alisema daraja la msingi ni kiungo muhimu kati ya ukanda wa kati na nchi za Afrika Mashariki hususan kwenye mpaka wa Sirari mkoani Mara kupitia Simiyu.

“Matumaini yangu, uwepo wa daraja hili na mengine yote yaliyojengwa yatachochea zaidi biashara na mazao ya kilimo ufugaji na bidhaa kutoka kwenye viwanda vidogo vidogo,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi hao kufanya kazi kwa bidii ili kuwe na manufaa ya uwepo wa daraja hilo.

“Muhimu zaidi, tulitunze au tutunze miundombinu ya madaraja yote yaliyojengwa ili yaweze kutufaa leo na huko tunakokwenda, madaraja haya yanajengwa kwa gharama kubwa kama mlivyosikia jumla ya Shs. bilioni 11.208 zimetumika kwenye daraja la msingi,” alisema.   

Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mkoa wa Singida, yalimkuta Rais Samia kwenye ziara yake mkoani Singida yaliyosherehekewa katika uwanja wa Bombadia.

Rais Samia aliwataka viongozi wa Mkoa wa Singida kuwa na mikakati ya kutumia fursa za kiuchumi badala ya kujikita kwenye sekta moja ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Mkoa huo.

Katika hotuba yake, Rais Samia aliwahimiza wananchi kulima mazao ya alizeti, dengu na ufuta ambayo hustawi katika maeneo mengi ya Mkoa wa Singida pamoja na zao la Korosho ambalo pia linafanya vizuri katika maeneo mengi ya Mkoa huo.

Oktoba 17, Rais Samia alizindua mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwa ajili ya mji wa Shelui katika hafla ya fupi iliyofanyika katika Kijiji cha Kizonzo, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Aliwahutubia wananchi wa Iramba kweye mkutano wa hadhara uliofanyika Shelui.

Siku hiyo hiyo, Rais Samia alianza Ziara ya kikazi mkoani Tabora yeye lengo la kukagua na kufungua mirai mbalimbali ya maendeleo mkoani humo ambapo alifanya mkutano wa hadhara uwanja wa barafu Wilaya ya Igunga.

Aliwahutubia wananchi wa Iramba kweye mkutano wa hadhara uliofanyika Shelui kisha Samora Nzega ambapo kote huko wananchi wamekuwa wajikitokeza kwa wingi sana.

Akiwa kwenye uwanja wa Samora, Rais Samia aliwataka Wakala wa Mbegu nchini (ASA) kuzalisha mbegu zenye ubora kwa bei ambayo mkulima ataimudu.

Pia aliweka jiwe la msingi ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi ufundi stadi (VETA) cha Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kilichogharimu zaidi ya sh bilioni 2.6.

Chuo hicho chenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wanafunzi 900 wa kozi za muda mfupi kinalenga kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi na kujiajiri.

Alisema serikali imedhamiria kukuza ujuzi wa vijana kwasababu ndiyo nguvu kazi ya taifa hivyo vyuo vya VETA vinajengwa ili ziungane na miradi na mipango inayoanzishwa na serikali ili kujenga uchumi wa nchi.

Oktoba 18, 2023 aliweka jiwe la msingi mradi ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika shamba la mbegu za mazao ya kilimo eneo la Kilima.

Alizungumza na wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la wamachinga Parking Nzega mjini ili kujionea na kutatua changamoto mbalimbali ambapo alitoa sh bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.

Pia Rais Samia alitoa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo wa soko hilo na kununua bidhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *