Samatta rasmi atua PAOK

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Fenerbahce ya nchini Uturuki, imethibitisha kuachana na straika wake, Mtanzania Mbwana Samatta ambaye sasa amejiunga na PAOK Thessaloniki ya Ligi Kuu Ugiriki (Super League) kwa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja.

Samatta amejiunga na klabu hiyo baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Fenerbahce.

Msimu uliopita Samatta ameichezea KRC Genk kwa mkopo baada ya kukosa nafasi ya kucheza ndani ya timu hiyo ambapo pia aliwahi kucheza kwa mkopo Royal Antwerp zote za nchini Ubelgiji.

Mtandao huu ndio ulikuwa wa kwanza kuripoti taarifa hiyo ya Samatta wiki iliyopita ambayo jana kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mtandao wa Klabu ya Fenerbahce, ambayo hutumia jezi za njano, imethibitisha rasmi uhamisho huo.

Samatta amejiunga na Fenerbahce akitokea Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne ambao ulitakiwa kumalizika mwakani.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, ambaye amewahi kutamba pia na TP Mazembe na Simba SC, kwa ujumla wake amecheza mechi 357 na kufunga mabao 119 pamoja na asisti 33.

Lakini pia akiwa nahodha wa Taifa Stars, amefunga mabao 22 katika mechi 72 alizocheza.

PAOK FC ambayo ni ya tatu kuwa na mashabiki wengi nchini Ugiriki, hivi karibuni ilicheza mechi ya kirafiki na KRC Genk na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika kujiandaa na msimu mpya wa 2023/24.

Timu hiyo inatumia Uwanja wa Toumba wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 29,000, ilishika nafasi ya nne msimu uliopita nyuma ya mabingwa AEK Anthens, Panathinakois na Olimpiacos, imewahi kutwaa ubingwa wa Super League mara tatu na kutwaa Kombe la Ugiriki mara nane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *