Samatta ahesabu saa kutua PAOK Thessaloniki

Na Zahoro Mlanzi

NAHODHA wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, anatarajia kujiunga na timu ya PAOK Thessaloniki ya Ligi Kuu Ugiriki (Super League) akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Fenerbahce ya Uturuki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa na vyombo vya habari nchini Uturuki, viongozi wa nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania, wamesafiri hadi Ugiriki ili kumsimamia kufanyiwa vipimo vya afya na kusaini mkataba.

Samatta anatarajia kusaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Nyota huyo msimu uliopita alikuwa akiichezea timu yake ya zamani ya KRC Genk kwa mkopo, ambapo awali timu hiyo ilikuwa na mpango wa kumsajili jumla kabla ya dakika za mwisho kughaili.

Hata hivyo, mapema mwezi huu PAOK na Samatta, walifikia makubaliano ya kila kitu na kilichobakia ni vipimo vya afya na kusaini mkataba kitu ambacho kilitarajiwa kufanyika jana mjini Thessaloniki.

Samatta aliwahi pia kutamba na Genk, TP Mazembe, Antwerp, Fenerbahce, Simba SC na Aston Villa, ambapo kwa jumla amecheza mechi 357 na kufunga mabao 119 pamoja na asisti 33.

Lakini pia akiwa nahodha wa Taifa Stars, Samatta amelifungia taifa hilo mabao 22 katika mechi 72 alizocheza.

PAOK FC ambayo ni ya tatu kuwa na mashabiki wengi nchini Ugiriki, juzi ilicheza mechi ya kirafiki na KRC Genk na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 katika kujiandaa na msimu mpya wa 2023/24.

Timu hiyo inatumia Uwanja wa Toumba wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 29,000, ilishika nafasi ya nne msimu uliopita nyuma ya mabingwa AEK Anthens, Panathinakois na Olimpiacos, imewahi kutwaa ubingwa wa Super League mara tatu na kutwaa Kombe la Ugiriki mara nane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *