Samamba awataka maofisa madini kusimamia migodini

Na Mwandishi Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Ismail Samamba, amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kuweka nguvu kwenye usimamizi wa usalama na mazingira kwenye migodi ya madini hasa katika msimu huu wa mvua ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea na kusababisha vifo.

Samamba ametoa agizo hilo jana Novemba 21, 2024 jijini Dar es Salaam, kwenye kikao chake na Menejimenti ya Tume ya Madini ikijumuisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, Wakurugenzi, Mameneja na Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa.

“Ninawataka kufanya ukaguzi mkubwa kwenye migodi yote ya madini nchini hasa katika kipindi hiki cha mvua na kusitisha shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo hatarishi ili kuepuka ajali zinazoweza kutokea,’’ amesisitiza Samamba.

Katika hatua nyingine, amewapongeza Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa kwa mwenendo bora wa ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu ikiwa ni pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.

“ Katika kipindi cha kwanza cha mwaka wa fedha 2024/25 mwenendo wa makusanyo ya maduhuli ambapo mpaka sasa wastani wa kiasi cha Sh. bilioni 395 zimeshakusanywa, nawapongeza kwa kazi nzuri sana na kuwataka kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli pamoja na kuwapo kwa changamoto ya kushuka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia na kipindi cha mvua ambacho kinatarajiwa kuanza hivi karibuni,’’ amesisitiza Mhandisi Samamba.

Katika hatua nyingine, amewataka maofisa hao kutoa elimu kwa wadau wa madini kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya madini katika mikoa yao kupitia warsha, maonesho na makongamano mbalimbali.

Aidha, amewataka kuendelea kusimamia kwa karibu watumishi waliopo chini yao na kusisitiza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kutosha na uboreshaji wa maslahi ya watumishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *