Na Martha Saranga
BBC, Dar es Salaam
“SAFARI yangu kama msichana wa Kitanzania ninafahamu umasikini unavyozima ndoto za wasichana.
“Kati ya wanafunzi 200 waliohitimu na mimi kidato cha nne, ni 9 tu ndiyo tulifaulu kuendelea na masomo ya kidato cha tano, ambapo wasichana tulikuwa watatu pekee.
“Matokeo hayo yaliniumiza sana kuona kwa nini wenzangu wengi hawakuweza kufanya vizuri mitihani yao na wengi maisha yao yakaishia mtaani, lakini nikagundua kwamba mazingira hayakuwa wezeshi na bado hata sisi tulikuwa na kazi nzito ya kuhakikisha tunafanya vizuri huko tunakoendelea.
Lydia Charles Moyo (31) ni mmoja kati ya washindi sita waliopata tuzo ya shirika la kimataifa la Global Citizen mwaka 2024, kwa kuonesha juhudi za vijana duniani katika kuleta mabadiliko na vilevile kutunukiwa tuzo yenye thamani kubwa barani Afrika ya KBF.
Anasema, wakati anahojiwa na Global Citizen kuwashawishi kwa nini anastahili tuzo hiyo alitumia simulizi yake kuwaelezea namna alivyokuwa katika hali duni na kuwa na chachu ya mabadiliko katika jamii yake.
Global Citizen ni Shirika la Utetezi na Uhamasishaji la Kimataifa linalopigania kumaliza umaskini.
“…Kupata tuzo hii inabidi wadau duniani wakupendekeze ndiyo ufae, sijui nani alinipendekeza, sikutarajia lakini baadaye katika mchujo kati ya vijana 500 nami nikawa miongoni mwa vijana 6 waliopata tuzo,” anasema Lydia.
Tuzo ya pili ni mchakato ambao ulianza mwaka 2023 Februari, taasisi mbalimbali zilituma maombi ambapo zaidi ya taasisi 400 ziliomba na kuchujwa hadi kubaki 25, ambazo zilitakiwa kutuma video ya dakika mbili ya kuelezea kila kitu ili wafanye maamuzi kutoka katika video hizo.
Lidya kupitia taasisi yake ya @herinitiative ameshinda tuzo ya thamani kubwa ya KBF Africa ya Wakfu wa Mfalme Baudouin (King Baudouin Foundation) kutokana na kazi zake za uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake, ili kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kupambana na ukosefu wa ajira Afrika Mashariki.
Alipokea zaidi ya shilingi milioni 560 za Kitanzania kusaidia wanawake zaidi ya 100,000 kote Afrika Mashariki kufikia ustahimilivu wa kifedha.
Safari yake kitaaluma yenye mabonde na milima
“Masomo na changamoto nilizopitia katika maisha ya kila siku ndizo zilinipa msukumo nikajikuta nikianzisha hii taasisi ya Her Initiative,” anasimulia Lydia.
Nilimaliza shule ya msingi nikiwa na ndoto ya kusoma shule ya sekondari ya Jangwani, yaani simulizi na taswira niliyokuwa ninaiweka kwenye kichwa changu ni kuvaa sketi ya rangi ya chungwa ya Jangwani.
Mwaka 2007, matokeo yalipotoka nikabahatika nimechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Kata ambayo wakati huo haikuwa na mazingira rafiki kielimu.
“Kulikuwa hakuna maabara wala madarasa ya kutosha, hakukuwa na walimu wa kutosha, nakumbuka kidato cha pili hatukuwa na mwalimu wa hesabu lakini bado tulifanya mtihani wa taif,” anaeleza Lydia.
Anasema, alikuwa akitamani sana kusoma katika shule maarufu zilizokuwa na mazingira mazuri ya kielimu lakini hakuwa na namna zaidi ya kuyakabili mazingira magumu ya shule ya Kata ya King’ongo Sekondari katika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Lydia anakiri kuwa aliweka juhudi kubwa sana katika masomo haswa alipokuwa akiona jitihada za mama yake za kumtaka asome.
Alichaguliwa kusoma kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Tambaza ndipo hapo alianza harakati za kuelimisha wasichana wenzake kujitambua na kujithamini.
Anasema, alizunguka katika shule mbalimbali kutoa elimu na uhamasishaji haswa kwa wasichana ili wajitambue na kupata ujasiri wa kuzikabili changamoto zao.
Alianza kuwatafuta wasichana na wanawake maarufu ambao kwa wakati huo walikuwa tayari wanafanya mambo chanya kwenye jamii nchini Tanzania.
“Msemo wangu ulikuwa, Sisi hatuna hela tunaomba tu uje, na walikuwa wanakuja,” anasema Lidya akitabasamu.
“ilikuwa nawapigia simu kina Nancy Sumari, Jokate Mwegelo na wengineo nao walikuja na kuzungumza na wasichana,” anaeleza.
Baada ya kumaliza kidato cha sita alipata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Anasema maisha ya chuo hayakuwa rahisi, ndiyo wakati aliposhuhudia baadhi ya wasichana wakijiingiza katika tabia hatarishi ili kutafuta kipato cha ziada.
“Kama msichana niligundua nina mahitaji mengi kuliko uwezo niliokuwa nao,” anasema.
Akiwa chuoni msukumo wa kuanzisha tamasha la ujasiriamali chuoni hapo lililoitwa ‘Panda’ kwa maana ya kupanda mbegu ya kujitegemea, ulimjia.
Ni tamasha ambalo aliwaalika wajasiriamali wakubwa Tanzania kuzungumza na wasichana. Wakiwapa wasichana wa vyuoni nafasi ya kuonesha biashara zao au mawazo yao ya ubunifu wakati huohuo akijipatia ufadhili ambao ulimuwezesha kujikimu.
Anasema, amelelewa na mama peke yake, ambaye alikuwa mtumishi wa hali ya chini wa serikali ambaye alisoma mpaka darasa la saba tu.
Mama yake hakuelewa nini hasa Lydia alichokuwa akifanya lakini hakuacha kumuuliza na kumtia moyo.
Harakati za kiuchumi zilizogeuza tamasha kuwa taasisi
“Panda ni safari ya msichana wa Kitanzania kujikwamua kiuchumi,” anaeleza Lydia.
Mwanzoni ilianza kama tamasha la kuonesha wazo ujuzi au biashara za wanawake lakini baadaye aliamua kuifanya kuwa taasisi ambayo inasaidia wasichana kutengeneza kipato, kuanzisha biashara kuzikuza na kupata rasilimali ili kukuza biashara zao zaidi.
“Mwaka 2021, baada ya Uviko-19 tukajifunza mabadiliko yaliyotokea kote ulimwenguni ili kutunza afya zetu, tuliamua kutengeneza jukwaa la kidijitali la wasichana ili kukutana nao mtandaoni badala ya ana kwa ana,” anasema Lydia.
Jukwaa la Panda dijitali liko katika lugha ya Kiswahili kwa ajili ya wasichana wa Kitanzania kupata elimu na fursa za kibiashara.
Mfumo mseto umetumika kwenye Panda dijitali ili kukidhi mahitaji ya msichana aliyeko kijijini na mjini.
Lydia anafurahia kwamba wasichana wanapata fursa ya kujisajili na kupata fursa mbalimbali ikiwemo kukutana na wataalamu.
Panda dijitali hii inatoa huduma bure ili kuwawezesha wasichana wa kila tabaka kupata fursa na kuitumia ambapo hadi sasa zaidi ya wasicha 6,000 wanaitumia na idadi kubwa ni kutoka vijijini.
Baada ya kupitia changamoto za kimfumo katika kuimarisha taasisi, Lydia aliandika barua kwa wadau wa maendeleo na kuwataka kutowaita tena kama hawako tayari kuwafadhili kukuza ndoto hizi.
Umuhimu wa kustahimili maneno ya kukatisha tamaa
Utamaduni unamzuia msichana kufika mbali. kila siku msichana anapaswa kufungua masanduku ambayo tamaduni mbaya zimewafungia.
Rushwa ya ngono ni changamoto kubwa sana ambayo inazima ndoto za wasichana.
“Sijui kama inawakuta wavulana, lakini kwa wasichana ni tatizo kubwa. Inahitaji uwe jasiri na ujue mifumo ya kuripoti,” anasema.
Lydia anashukuru taasisi yake ambayo inashirikiana na wadau muhimu wa kupambana na rushwa ya ngono na kutengeneza mifumo ambayo inalinda utu wa msichana.
“Changamoto hii imenifanya niwe tayari kukabiliana na lolote, yaani siku hizi ninalipenda zaidi jibu la “NO” HAPANA… kuliko NDIYO.
“Suala la rushwa ya ngono limekuwa kikwazo kwa wasichana wengi kufikia ndoto zao.
“Nimewahi kukutana na changamoto hiyo sikujua kama ningeweza kuripoti kwa kuwa bado sikuwa na elimu ya kutosha ya kukabiliana na rushwa ya ngono.
”Sikujua namna ambavyo ningeweza kuripoti kujipanga na kukusanya Ushahidi,” anasisitiza.
Ndoto ya baadaye ya Lydia Charles
Anasema ndoto yake kubwa ni kuweza kufadhili wasichana wenye ndoto kubwa.
”Kuna masuluhisho mengi ya Changamoto za jamii lakini wasichana wanakosa fedha ili kufanya hivyo.”
Moja ya vitu ambavyo amejifunza Lydia ni kuamini ndoto yake binafsi kabla ya kutegemea wengine wamuamini.
Anasema wasichana wasichoke kugonga milango mingi ipo itakayofunguka.
Kwa wale waliolelewa na mzazi mmoja, Lydia anawataka kuachana na fikra hasi.
Ni vizuri kulelewa na wazazi wote lakini kama imetokea basi wasichana waendelee kufungua masanduku kwamba haijalishi mzazi mmoja, au umelelewa kijijini kila kitu kinawezekana.