Na Badrudin Yahaya
Kocha wa timu ya Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amesema anapenda kucheza mechi kubwa na kwamba yupo tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga Jumapili utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha huyo amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es salaam kuelekea mchezo huo na amekiri kuwa presha ni sehemu ya kazi yake na amejiandaa kwa ajili ya kukabiliana nayo.
Aidha kocha huyo ameukubali ubora wa wapinzani wao Yanga hasa kwenye eneo la kiungo lakini amejinasibu kuwa atachagua wachezaji bora kabisa ambao wataweza kumpa matokeo chanya.
“Mimi ni raia wa Brazil ni nchi ya mpira, mimi binafsi napenda kucheza mechi kubwa na kwa siku ya kesho nimekiandaa kikosi changu kwa ajili ya kucheza mchezo dhidi ya Yanga,” amesema Robertinho.
“Mchezo huu utakuwa mgumu na hii ni kutokana na ubora wa wapinzani wetu hasa eneo lao la kiungo, hata hivyo mimi nitachagua wachezaji sahihi ambao wataweza kunipa matokeo,” amesema.
Simba wanaingia katika mchezo huo wakiwa kifua mbele hasa baada ya kuwatambia watani zao katika mechi mbili zilizopita ambazo zote zilikuwa chini ya Robertinho.
Kwenye msimamo wa ligi, Simba ipo nafasi ya pili wakiwa na alama 18 sawa na Yanga ambao wamecheza mechi moja ya ziada.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa saa 11 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati na kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) mageti yatakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi.