Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Dkt Frank Walter Steinmeier, leo anatembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya MajiMaji Songea.
Makumbusho hiyo ina historia kubwa ya vita vya MajiMaji wakati wa harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas alisema maandalizi ya kuupokea ugeni huo yamekamilika ambapo baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Songea ataenda moja kwa moja katika Makumbusho hhayo.
Alisema akiwa katika Makumbusho hayo atapata historia yake, kutoa heshima kwa mashujaa waliokufa katika vita hivyo vilivyopiganwa mwaka 1905-1907.
Kanali Thomas alisema pia kiongozi huyo atatoa heshima kwa mashujaa wa Vita vya Majimaji, kukutana na baadhi ya wahanga wa vita hivyo, kutembelea Shule ya Msingi MajiMaji.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamshna Benard Wakulyamba, alisema Wizara hiyo na Makumbusho ya Taifa wanaosimamia Makumbusho hayo wamekamilisha maandalizi na kumpokea kiongozi huyo.
Rais Dkt. Steinmeier yupo nchini kwa ziara ya kikazi siku tatu kuanzia Oktoba 30, 2023 hadi leo. Ziara hiyo mbali ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo kati yanchi huzo, imelenga kukuza, kuimarisha biashara, uwekezaji.