Rais Samia: Tanzania inafaa kwa uwekezaji

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inafaa kwa uwekezaji kwa sababu ina utajiri wa vyanzo vya nishati kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za maendeleo.

Aliyasema hayo Novemba 8, 2023 wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Uwekezaji barani Afrika, lililofanyika Marrakesh nchini Morocco.

“Lakini tena kwa vyanzo vya nishati, Tanzania ina gesi, tunayo nishati ya jua na tuna umeme wa maji hivyo vyanzo vya nishati Tanzania ni tajiri sana. Kitu pekee ni kuwekeza na kuhakikisha tuna nguvu ya kutosha kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za maendeleo.

“Tunaungwa na anga, Air Tanzania sasa inasafirisha watu na bidhaa kwa nchi jirani na hata nje ya Afrika. Hivyo ndivyo tunavyounganishwa,” alisema.

Alisema, kwa sasa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea nchini pamoja na kufanya marekebisho ya Reli ya zamani ya Kati ambayo itaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Burundi kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kisha Rwanda na pia Uganda itaunganishwa kupitia reli hiyo.

Alisema zipo agenda ambazo anaziwekea mkazo ambazo ni sekta ya elimu na afya.

Aliongeza kuwa, kwa kutambua sekta ya afya na elimu inamchango kwenye ukuaji wa uchumi aliamua kuziwekea mkazo.

Alisema kazi kubwa ilifanywa awamu iliyopita ambapo aliamua kufanya zaidi kwenye utoaji wa afya bora kwa wananchi kwa kujenga hospitali kuanzia ngazi ya vijiji, usambazaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na upatikanaji wa wataalamu wa afya.

“Kwenye afya nadhani kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kila mtu, kwa kutoa bima ya afya nchi nzima hiki ndicho tunakifanyia kazi kwa sasa,” alisema.

Alisema, pia serikali imebeba agenda ya lishe ambapo waliona ni muhimu kwa ukuaji wa vijana nchini.

Akizungumzia elimu, Rais Samia alisema serikali imeamua kutoa elimu bure nchi nzima.

Alisema kuwa na elimu bure ambapo kwa vijana hasa wasichana wanaopata changangamoto na kukatisha masomo yao kurudi kwenye mfumo rasmi na kuendelea na masomo.

Rais Samia aliongeza kuwa ili kuendana na mapinduzi ya viwanda, serikali inatekeleza utoaji wa masomo ya sayansi kwa wasichana ili kupunguza gap katika ufanyaji kazi.

Alisema licha ya hivyo, serikali imewaingiza wanawake na vijana kwenye Mpango wa Jenga Kesho yako iliyo Bora (BBT), kwa kujihusisha kwenye kilimo, uvuvi, ufugaji na kulina asali.

“Tumetengeneza mradi unaitwa Jenga Kesho yako iliyo Bora (BBT), hii ni uboreshaji na ufanyaji biashara katika sekta ya kilimo, ikijumuisha uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji, usindikaji na kuweka majukwaa kidijitali kwa vijana,” alisema.

Aliongeza kuwa, majukwaa hayo yataangalia shughuli za kilimo, masoko, na namna ya kupata kipato kwa mkulima mdogo.

Alisema anatarajia hadi kufikia mwaka 2030 sekta ya kilimo itakua itaongeza Pato la Taifa kutoka asilimia 4.6 ya sasa hadi kufikia asilimia 10.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *