Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anatarajia kuzindua mradi mkubwa wa maji unaotoa maji Ziwa Victoria hadi mkoani Singida.
Mradi huo ukikamilika utamaliza changamoto ya tatizo la maji katika Mkoa huo.
Rais Dkt. Samia yuko mkoani Singida kwa zaiara ya kikazi akikagua, kuweka mawe ya msingi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo ambapo maelfu ya wananchi walionekana kufurahia ujio wake.
Maeneo yote ambayo Rais Dkt. Samia amepita katika ziara hiyo alilakiwa na umati wa watu wakimuahidi kumpigia kura za ndiyo kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika 2025.
Sababu za wananchi hao kutaka aendelee katika kipindi kingine ni namna anavyoleta maendeleo kwa wananchi, kufuatilia miradi ya maendeleo kwa muda mfupi wa uongozi wake.
Akihutubia wananchi katika Uwanja wa Bombadier, Rais Dkt. Samia aliwataka viongozi wa Mkoa, Wilaya na Kata kusimamia kazi zao kwa kuhudumia wananchi na kutoa huduma bora.
Alisema ziara yake inaambatana na miaka 60 ya Mkoa wa Singida ambayo awali ilikuwa na Wilaya mbili lakini sasa ina Wilaya tano kutokana na ukuaji wa mahitaji ya maendeleo.
Alieleza kuwa, katika ziara yake anaendelea kuweka mawe ya msingi ili kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ili Mkoa uweze kuendelea.
Aliongeza kuwa, awamu mbalimbali za uongozi wa Mkoa huo zilikuwa zikiweka vipaumbele vya maendeleo na kuvitekeleza katika muktadhawa mahitaji ya vipindi husika.
Wakati wa kuadhimisha miaak 60 ya Mkoa huo, yapo maendeleo yaliyofikiwa kwa kuangalia maendeleo yanayopatikana.
Rais Dkt. Samia alisema sekta ya maji hadi sasa ipo katika hatua nzuri, hadi kufikia 2025 Mkoa huo uwe umepata maji, umeme. Hadi Desemba 2024 kuwe na asilimia 97 ya upatikanaji umeme mkoani humo.
Alisema Mkoa huo una changamoto za asili ambazo ni ya tabia nchi kutokana na kuwa miongoni mwa Mikoa inayopata kiasi kidogo cha mvua kwa mwaka.
“Kati ya miaka ya 1970 na 1980, Singida ulikuwa mkoa wa mwanzo au katika mikoa iliyokuwa ikipewa msaada wa chakula kila mwaka tena katika Wilaya zote.
“Lakini kutokana na juhudi za uongozi wa Mkoa uliokuwepo baada ya miaka hiyo, tatizo la njaa katika mkoa huo limepungua sana,” alieleza.
Alifafanua kuwa, licha ya mabadiliko ya tabia ya nchi, Mkoa huo unaweza kuzalisha zaidi hivyo waangalie tatizo lilipo kwa kuangalia mabadiliko ya tabia za watu ili kutumia fursa zilizopo.
Serikali imejitahidi kujenga vituo vya afya nchi nzima lakini kutokana na sababu zisizo eleweka zaidi ya vituo 15 vimechelewa kufunguliwa na kutoa huduma kwa wananchi.
“Vituo vilishajengwa, watumishi wapo na vifaa vipo lakini havijafunguliwa, hii huwezi kusema chochote ni tabia za watu, twendeni kwenye mabadiliko ya tabia za watu,”alisema.
Alisema licha ya changamoto zilizopo, wajielekeze kwenye fursa zilizopo katika Mkoa huo.
“Huwa nawaambia Mawaziri wangu tumieni fursa ili kunufaisha wananchi, msiwe majoka ya mdimu, zifungueni fursa zitumike zilete maendeleo kwa wananchi,” alisema.
Alieleza kuwa, Mkoa huo una ekari 26893 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji hivyo walitumie eneo hilo kuzalisha.
Tayari Serikali imetenga fedha ya kujenga mabwawa katika maeneo hayo ili maji yatumike, watu walime zaidi ya msimu mmoja.
“Niwaomba wanaosimamia hili kuharakisha utekelezaji wake ili maji yatakayotegwa kwenye msimu ya mvua yaweze kusaidia watu 2024,” alifafanua.
Rais Dkt. Samia alisema serikali itafanya maboresho ya skimu zote za umwagiliaji ili kulima mazao misimu miwili kwa mwaka.
Alielekeza wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame kwa muda mfupi kama alizeti, ufuta.
Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari hasa wananchi wanaoishi maeneo ya bondeni dhidi ya mvua ya El Nino inayotarajiwa kunyesha, kuzibua mitaro.
Kwa upande wake, Waziri wa TAMISEMI, Mohammed Mchengerwa, alisema hajashangaa kuona Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kati Singida, Dkt. Cyprian Hilinti kumuomba Rais Dkt. Samia aridhie kuwa Mama wa Taifa la Tanzania.
Alisema Rais Dkt. Samia ameingia kwenye fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere.
“Kila mmoja wetu ni shuhuda, kwa Mtanzania wa kawaida anayetaka kufuata kasi zako basi aongozane nawe katika mikutano ya hadhara ataweza kujionea jinsi Watanzania wanavyokupenda na wanavyokukubali.
“Rais mambo unayofanya kwa Watanzania hasa wa kawaida ni makubwa, umeingia katika mioyo na fikra zao, umejenga shule za msingi 302, shule za kawaida zaidi ya 3000, shule za awali 365, sekondari 543, vituo vya afya na miundombinu mingine.
“Fikra, maono, mazingatio, maelekezo, mitazamo ya nyakati za TANU, nyakati za CCM za Rais wa Awamu ya Kwanza Mwl. Nyerere ilikuwa katika kuzingatia vita dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi,” alisema.
Alisema Rais Dkt. Samia amelifanya hilo kwa kuingia katika fikra za Baba wa Taifa.
“Ndio maana sikushangaa hata kidogo kumuona Baba Askofu akikutangaza uridhie kuwa Mama wa Taifa letu ukiwa Rais wa kwanza Mwanamke kwa kazi kubwa na nzuri ambayo unaifanya kwa Watanzani , hongera sana Rais wa Tanzania.
“Ukiangalia kiuhalisia, haiwezekani miaka 60 ya Mkoa huu wa Singida, unachangia chini ya asilimia 2 kwenye pato la taifa na kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa mitano maskini au maskini zaidi nchini.
“Fursa alizotuumbia Mungu ni nyingi mno, kakaeni muangalie na mjitathmini, mje na mpango ambao tutaweza kuwasaidia muende mbele zaidi,” alisema.