Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limemtangaza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi katika shindano la kusoma na kuhifadhi Quran kwa wanawake, linalotarajiwa kufanyika Agosti 31, mwaka huu Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Shindano hilo la kwanza kufanyika nchini litaenda sambamba na tukio la kumpa tuzo Rais Samia, kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kulitumikia Taifa, likipangwa kuanza mapema asubuhi hadi orodha ya washindani itakapokamilika uwanjani hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Sheikhe Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally, amesema ni furaha kubwa kwa shindano hilo kuhudhuriwa na Rais, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi huyo wa nchi kushiriki kama mgeni rasmi katika mashindano ya kusoma na kuhifadhi quran tangu akabidhiwe madaraka ya urais.
“BAKWATA inamtangaza Rais Samia kama mgeni rasmi katika shindano hili la wanawake linalofanyika nchini kwetu kwa mara ya kwanza likishirikisha wanawake wa nchi 12 duniani, lenye dhumuni kubwa la kumuheshimisha mwanamke katika ulimwengu wa Quran.
“Pamoja na mambo mengine, siku hiyo kutatolewa tuzo kwenda kwa Rais Samia, sambamba na wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wana mchango mkubwa katika ukuzaji na utangazaji wa dini yetu ndani na nje ya nchi yetu,” amesema Mufti Zuber.
Katika hatua nyingine, Rais Samia atashuhudia pia uzinduzi wa ‘Msahafu’ uliokuwa kwenye mfumo wa Eletroniki, kama njia ya kurahisisha usomaji wa Quran ulimwenguni, haswa kwa wakati huu Dunia inapiga hatua kubwa katika Sayansi na Teknolojia.
“Ulimwengu mzima umetega sikio kusubiri uzinduzi mkubwa wa Msahafu katika ardhi yetu ya Tanzania, yakiwa ni mafanikio makubwa ya dini yetu, katika nchi ambayo imepata bahati kubwa kuongozwa na Rais mwanamke, Dkt. Samia, ambapo wote tunashuhudia nchi ikipiga hatua kubwa,” amesema Mufti Zuber.
Kwa upande wa Sheikhe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikhe Walid Alhad Omar, amesema uhudhuriaji wa Rais kwenye tukio hilo linalowahusisha wanawake wa ndani na nje ya nchi, wamepata faraja kubwa.
“Wamepita marais wengi nchini, lakini Dkt. Samia ndio wa kwanza kuhudhuria mashindano ya kimataifa ya uhifadhi na usomaji wa Quran, kama ilivyo kwa Sheikhe Mkuu wa Tanzania kuwa wa kwanza kuanzisha mambo mbalimbali yanayoikuza na kutangaza dini ya uislamu ulimwenguni,” amesema Omar.
Amesema kufanyika kwa tukio hilo kubwa nchini katika Uwanja wa Taifa kuanzia asubuhi, ni sehemu mahususi ya kuombea nchi iwe na amani, mshikamano, weledi na mapenzi makubwa ili kuleta maendeleo.
Kuanzishwa kwa mashindano hayo ya wanawake nchini Tanzania kunatajwa kama njia ya kukuza maadili ndani ya jamii haswa wakati huu ambao baadhi ya watu wanafanyiana ukatili huku chanzo kikitajwa kama ukosefu wa maadili.