Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuhudhuria mjadala wa Kimataifa wa Norman E. Borlaug unaotarajiwa kufanyika Des Moines, Iowa, nchini Marekani.
Mjadala huo umeandaliwa na Taasisi ya World Food Prize Foundation ya nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Sharifa Nyanga, alieleza kuwa mjadala huo hufanyika kila mwaka na kuhudhuriwa na viongozi, wataalamu, watu mashuhuri, watunga sera, hususan za kilimo, lishe na usimamizi wa rasilimali.
Alisema Shabaha ya majadiliano hayo ni kutafuta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa chakula duniani, ambayo inachochewa na mabadiliko ya tabianchi.
Nyange alisema Rais Dkt. Samia ni miongoni mwa Marais wanne kutoka Afrika, waliopewa heshima ya kushiriki na kuchangia kwenye mjadala huo wenye kaulimbiu isemayo: Mbegu za Fursa: Kuunganisha Vizazi na Kustawisha Diplomasia (Seeds of Opportunity: Bridging Generations and Cultivating Diplomacy). Viongozi wengine watakaoshiriki ni kutoka nchi za Sierra Leone, Madagascar na Nigeria.
Licha ya Mjadala huo, Rais Dkt. Samia pia atashiriki hafla ya utoaji tuzo ya World Food Prize kwa mwaka 2024 kwa watu wenye mchango mkubwa katika sekta ya kilimo, ikiwa. ni mwendelezo wa kumuenzi Hayati Dkt. Norman E. Borlaug aliyehamasisha usalama wa chakula duniani kwa watu wote.
Sambamba na kushiriki kwenye majadiliano hayo, Rais Dkt. Samia atakutana na kufanya mazungumzo (round tables discussion) na viongozi kutoka Serikali na sekta binafsi ya Marekani, hususan waliopo kwenye sekta ya kilimo kwa lengo la kujadili uwekezaji katika sekta hiyo na kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.