*Akerwa na malalamiko ya wananchi
*Ahimiza amani, umoja, mshikamano
Na Mwandishi Wetu, Manyara
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa mikoa yote nchini (Ma-RC) na Wakuu Wilaya (Ma-DC), kuyafanyia kazi kwa vitendo malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi ya watumishi wa umma.
Alisema nidhamu, uadilifui kwa watumishi wa umma ni eneo ambalo bado lina changamoto hivyo kusababisha malalamiko kwa wananchi wanaohudumiwa.
Rais Dkt. Samia aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Mbio za Mwenye wa Uhuru katika Uwanja wa Tanzania Kwaraa, Mjini Babati, mkoani Manyara.
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na kumbukizi ya miaka 24 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere kilichotokea Oktoba 14, 1999 na Siku ya Vijana Kitaifa.
Alisema yapo malalamiko yanayotolewa na wananchi kwa watumishi wa umma kutoa lugha chafu, kudai rushwa na kuchelewesha huduma.
Alieleza kuwa, Wakuu wa mikoa na Wilaya wanapaswa kuyabeba malalamiko hayo na kuyafanyia kazi ili kurudisha imani ya wananchi kwa serikali yao.
“Huko chini kuna shida kubwa, Wakuu wa mikoa na Wilaya hakikisheni kero za wananchi zinafanyiwa kazi kwa vitendo, serikali ya Awamu ya Sita haipo tayari kuona malalamiko hayo yakiendelea,” alisema.
Aliwataka Watanzania kutekeleza maelekezo ya wataalamu kuhusu lishe akisema licha ya jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto hiyo, hali hairishishi.
Kwa mujibu wa Rais Dkt. Samia, takwimu za udumavu zinaonyesha asilimia 28 ya wanawake walio katika hatua ya kujifungua wana upungufu wa damu ambapo asilimia 32 wana uzito uliozidi.
Tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ni asilimia 30, uzito pungufu asilimia 12, ukondefu asilimia tatu, uzito uliopitiliza asilimia nne.
“Kazi imefanyika lakini jitihada zinahitajika, kiwango cha udumavu asilimia 30 ni kiashiria cha hali mbaya ya lishe kwa mujibu wa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO),” alieleza Rais Dkt. Samia.
Alitaja mikoa yenye kiwango kikubwa cha udumavu na udumavu zaidi ya wastani wa kitaifa ni Iringa (56.9%), Njombe (50.4%), Rukwa (49.8%) na Geita (38.6%).
Mikoa mingine ni Ruvuma (35.6%), Kagera (34.3%), Simiyu (33.2%), Tabora (33.1%), Katavi (32.2%), Manyara (32%), Songwe (31.9%), Mbeya (31.5%).
Rais Dkt. Samia aliwahimiza Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano, kufanya kazi kwa bidii kila mmoja kwa nafasi yake ili kuchangia ujenzi wa Taifa na kuelekea katika kujitegemea.
“Tunapohitimisha kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, tunapaswa kujitafakari kama Taifa jinsi tunavyotekeleza kwa vitendo msingi wa falsafa ya Mwenge.
“Je, tumeendelea kulinda, kudumisha amani, umoja mshikamano wa kitaifa, je, tunadumisha uzalendo, uadilifu na nidhamu,” alisema.
Alieleza kuwa, mwisho tujiulize kila mmoja kwa nafasi yake anafanya kazi kwa bidii ili kushiriki kikamilifu katika ujenzi wan chi yetu?
Alioongeza kuwa, ili uhuru uwe na maana, hakuna budi Watanzania kudumisha umoja, kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kujitegemea na vijaja ndiyo nguvu kazi katika Taifa lolote linalojitegemea.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilibeba kauli mbiu inayosema; “Tunza mazingira, ikoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa”.
Akiizungumzia kauli mbiu hiyo, Rais Dkt. Samia alisema ni ujumbe muafaka kwa nchi na dunia nzima kutokana na changamoto iliyopo ya mabadiliko ya tabia nchi kutokana na shughuli za kibinadamu zinazoathiri ikolojia, bionuwai na kuleta athati za mafurika, ukame, ongezeko la joto.