Na Zahoro Mlanzi
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amenunua tiketi 20,000 za mzunguko ikiwa ni sehemu ya hamasa kuelekea mchezo wa leo wa kufuzu AFCON 2025 kati ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ itakayoumana na DR Congo katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 10 jioni kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ilionesha kumshukuru Rais Samia kwa kusema ‘Ahsante Mama’ huku wakiweka wazi kununua tiketi 20,000 za mzunguko.
Katika mchezo uliopigwa wiki iliyopita nchini DR Congo, Taifa Stars ililala kwa bao 1-0 hivyo kujikuta ikisalia katika nafasi ya pili Kundi H ikiwa na alama 4 huku Congo ikiwa na alama 9, nafasi ya tatu inashikiliwa na Guinea yenye alama 3 na Ethiopia inaburuza mkia ikiwa na alama 1.
Mchezo mwingine wa kundi hilo, utapigwa saa 4 usiku ambapo wenyeji Ethiopia wataumana na Guinea. Mchezo uliopita Guinea ilishinda kwa mabao 4-1 ikiwa nyumbani.
Stars chini ya Kocha Hemed Morocco, ina kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea kwenye mechi yao iliyofanyika mwezi uliopita lakini pia ilianza kwa suluhu dhidi ya Ethiopia kabla ya hapo walipata ushindi wa bao 1-0 nchini Zambia katika mechi za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia.
Tangu mwaka 2019, Stars na DR Congo zimekutana katika mechi nne za mashindano mbalimbali ambapo kila mmoja ameonja ushindi mara moja na sare kati yao zikiwa ni mbili.
Mechi ambayo iliwakutanisha hivi karibuni zaidi ilikuwa ni Januari 24, mwaka huu katika michuano ya Afcon nchini Ivory Coast na matokeo yalikuwa ni suluhu kabla ya wiki iliyopita kufungwa 1-0.