Rais Samia akabidhi fidia ya Mil. 354/- kutoka NBC kwa wakulima walioathirika na mafuriko

Rais Samia Suluhu Hassan (wa pili kulia) akimkabidhi Mrajisi wa Vyama Vya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege (Kushoto) mfano wa hundi ya Sh. milioni 354 iliyotolewa na  Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti nchini, mwishoni mwa wiki jijini Dodoma alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (wa tatu kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. milioni 354 iliyotolewa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao Tumbaku walioathirika na mvua za mawe.

Wakulima hao waliathirika katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti hapa nchini na fidia hiyo inatokana na huduma ya bima ya kilimo inayotolewa na benki ya NBC kwa kushirikiana kampuni ya Shirika la Bima la Taifa (NIC)

Aidha, Rais Samia amekabidhi pia bima ya afya kwa wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao cha mkoani Lindi kupitia huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance.

Rais Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi (Kulia) akifafanua kuhusu huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo mahususi kwa wakulima wakati Rais Samia alipotembelea banda la Maonesho la Benki ya  NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Kushoto).

Rais Samia amefanya makabidhiano hayo mwishoni mwa wiki jijini Dodoma alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki ya NBC Theobald Sabi, kuhusiana na huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo ikiwamo huduma za bima ya kilimo na bima ya afya mahususi kwa wakulima.

“Bima hii ya kilimo ni moja ya suluhisho muhimu katika kuwahakikishia wakulima kipato cha uhakika bila kuhofia changamoto nyingine zikiwemo zile za asili ikiwemo mvua za mawe. Nitoe wito kwa wakulima nchini kutumia vema fursa hii muhimu kwa kuhakikisha wanapata huduma hizi za bima ya kilimo na bima ya afya. Zaidi nawapongeza sana NBC na wadau wote wanaoshiriki kwenye mpango huu,’’ alisema. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kushoto) akikabidhi kadi ya Bima ya Afya kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao, Hassan Mnumbe (wa pili kushoto) akiwa ni mnufaika wa huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance.  Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye banda la  maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.Wengine ni maofisa wa Kampuni ya Bima ya Assemble insurance Lilian Deogratius (Kulia) na Christina Luanda (wa pili kulia).

Akifafanua zaidi, kuhusu huduma ya Bima ya Kilimo mbele ya Rais Samia, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, alisema itasaidia kuondoa changamato ya hasara walizokuwa wakizipata wakulima kutokana na majanga mbalimbali yaliyo nje ya uwezo wao ikiwemo mafuriko, moto na mvua za mawe ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiathiri ustawi wa wakulima na kusababisha baadhi yao kuhofia kuwekeza kwenye sekta hiyo muhimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa  Shirika la Bima la Taifa (NIC) Kaimu Mkeyenge wakati Mkeyenge alipotembelea banda la maonesho la benki hiyo lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.

“Hata hivyo Mheshimiwa Rais hatua hii ya NBC ni mwazo tu kwa kuwa huu ndio mwaka wa pili tangu waanze kutoa huduma hii na tayari mafanikio yanaonekana. Kama serikali tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji mkubwa zaidi  wa huduma hii lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba huduma hii ya bima ya kilimo inawafikia wakulima wengi zaidi.” alipongeza Bashe.

Kwa mujibu wa Sabi wakulima walionufaika na malipo hayo wanatoka kwenye vyama vikuu vya ushirika 23 kutoka mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Mbeya, Katavi na Kigoma.

Mkuu wa kitengo cha wateja wadogo wadogo, wariba na wakulima kutoka Benki ya NBC, Raymond Urassa (Alievaa kofia) akimpongeza mkulima Alberto Kacheza ambaye ni mnufaika wa mkopo wa trekta kutoka benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Mahindra. Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye banda la  maonesho la Benki ya NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma.Wengine ni pamoja na Mkuu wa Biashara ya Kilimo kutoka Kampuni ya Mahindra, Praveen Chandra pamoja na maofisa wengine wa benki hiyo.

“Mbali na huduma huduma hizi za kibima, kama benki kupitia maonesho haya tumeendelea na utaratibu wetu wa kutoa elimu ya fedha na fursa mbalimbali za kibenki kwa wakulima sambamba na kutoa mikopo mbalimbali kwao ikiwemo mikopo ya zana za kilimo hususani mwa matrekta kwa wakilima mbalimbali waliokidhi vigezo na masharti ya mikopo hiyo,’’ aliongeza Sabi.

Akiwa bandani hapo Rais Samia pia alipata wasaa kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo mahususi kwa wakulima ikiwemo Akaunti ya Mifugo inayolenga kuwahudumia wadau wa sekta ya mifugo nchini huku pia akipata  nafasi ya kuzungumza na wanufaika wa huduma hizo akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao, Hassan Mnumbe ambaye chama chake kimekabidhiwa kadi ya bima ya afya kutoka benki hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *