Rais Samia aifagilia REA

RAIS Samia Suluhu Hassan ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi nzuri wanazofanya.

Rais ametoa pongezi hizo Agosti 4 wilayani Kilombero, Mkoa wa Morogoro alipotembelea Kituo cha Kupokea na Kupoza umeme cha Ifakara kilichojengwa na Serikali ya Tanzania kupitia REA kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya kilichotatua changamoto ya muda mrefu ya umeme wa uhakika katika Wilaya ya Malinyi, Ulanga na Ifakara.

Awali akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga, alimshukuru Rais Samia kwa kuridhia kupitia Wizara ya Nishati kujenga vituo 75 vya kupokea, kupooza na kusambaza umeme ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha wananchi katika maeneo yote wanapata umeme wa uhakika.

“Kabla ya mwaka 2021 nchi ilikuwa ina vituo 61 tu vya kupokea na kupoza umeme, tunakushukuru sana Rais kwa kuridhia ujenzi wa vituo vingine vipya 75,” Amesema Kapinga

Naibu Waziri Kapinga amesema kuwa, tayari vituo nane vimejengwa na kuanza kazi huku vituo sita vikifikia asilimia 97.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema kituo cha Ifakara kimejengwa kutokana na uhitaji mkubwa wa umeme wilayani Ifakara, Malinyi na Ulanga na hii pia inatokana na shughuli kubwa za kilimo na uchimbaji madini.

Mhandisi Hassan ameongeza kuwa, kabla ya ujenzi kituo cha Ifakara umeme kwa mwezi ulikuwa ukikatika mara 18 ambapo hivi sasa ikitokea umeme umekatika basi ni mara moja.

Ameongeza kuwa gharama ya ujenzi wa kituo hicho ilikuwa ni Sh. bilioni 24.5 ambapo serikali imechangia gharama hizo pamoja na wadau wa maendeleo ambao ni Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) na kukamilika kwa kituo hicho haujasaidia tuu kuongeza thamani ya mazao bali pia umesaidia kuboresha huduma za kijamii kama afya kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika hospitali na zahanati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *