Rais Samia afuta kilio cha miaka mingi ujenzi barabara ya Mtwara- Masasi.

Na Bwanku Bwanku.

Leo ukimuuliza mwananchi yeyote wa mkoa wa Mtwara au Lindi pamoja na Kusini kwa ujumla, ipi ni changamoto yako kubwa inayokutatiza, anaweza akakueleza changamoto mbalimbali lakini kamwe hawezi kutotaja changamoto kubwa ya barabara. Hawezi kuacha changamoto hii.

Hapa nazungumzia barabara iliyopachikwa jina la ‘barabara ya uchumi’ barabara kubwa na maarufu sana ya Mtwara hadi Masasi yenye Km zaidi ya 210.

Hii ni barabara inayounganisha mkoa mzima wa Mtwara kuanzia Makao Makuu ya mkoa huo pale Manispaa ya Mtwara Mjini mpaka wilaya ya mwisho wa mkoa huo ya Nanyumbu. Barabara hii inaunganisha mkoa wa Mtwara na nchi jirani ya Msumbiji na ni kiungo muhimu kuunganisha mkoa mpaka Mbambabay kupitia ushoroba wa Mtwara yaani Mtwara Corridor.

Inaunganisha pia mkoa wa Mtwara mpaka Ruvuma na Pwani kuelekea maeneo mengine ya Taifa ikibeba uchumi mkubwa wa eneo hili ikiwemo kusafirisha makaa ya mawe, zao kuu la kibiashara nchini la korosho, pia ufuta pamoja na mazao mengine na uchumi mkubwa wa ukanda wa Kusini.

Kifupi tu, hii ni barabara ya kiuchumi yenye manufaa makubwa sana ambayo kwa muda mrefu imekuwa kero kwa wakazi wa ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla na kudumaza maendeleo ya ukanda huu, sasa suala hili linakwenda kuwa historia.

Kero ya barabara hii inayounganisha kutoka Mtwara Mjini, Nanyamba, Tandahimba, Mahuta, Newala hadi Masasi ni ya muda mrefu sana toka kipindi tunapata Uhuru na imetumika sana kisiasa kwa muda mrefu sana na wanasiasa wa vyama mbalimbali kujipatia kura kwa wananchi wa Kusini kwa kuahidi kuijenga.

Imekuwa kero kubwa ya vumbi ya barabara hiyo, umuhimu wake kwa uchumi wa Kusini na Taifa kwa ujumla ni mkubwa sana kwahiyo kwa namna yoyote ile ilikuwa ukiitaja tu barabara hiyo lazima uungwe mkono kwa jinsi ilivyowatesa wananchi wa Kusini.

Barabara hiyo imepandisha gharama ya usafirishaji, uharibifu wa mapema wa vyombo vya usafiri, kupoteza muda mrefu barabarani na sababu zingine mbalimbali. Kwa umuhimu wake na kutokuwa na lami kwa muda mrefu imefanya gharama kubwa ya uendeshaji wa usafiri wa umma ikiwemo malalamiko ya muda mrefu ya magari kuharibika haraka kwasababu ya ubovu wake. Hatuwezi kumaliza kuhesabu kero kubwa ya barabara hii, lakini ni nyingi sana.

Ubovu wa barabara hii kwa muda mrefu sana imeumiza sana uchumi wa Mtwara, Kusini na Tanzania kwa ujumla kwasababu ndio barabara kuu inayounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji, ndiyo barabara inayopitisha mazao yote hasa korosho kutoka wilaya zinazozalisha korosho zaidi nchini za Tandahimba, Masasi, Newala, Nanyumbu na za mkoa wa Ruvuma kupeleka bandari ya Mtwara au Dar es Salaam ajili ya kusafirisha kwenda nje au Dar es Salaam na mikoa mingine.

Ubovu wake unasababisha gharama kubwa ya usafiri. Mfano kutoka Newala mpaka Mtwara mtu analazimika kutumia zaidi ya saa 4 wakati kama ingekuwa na lami ingekuwa suala la muda mfupi sana usiozidi hata masaa mawili.

Imesababisha uharibifu wa magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri kwenye eneo hili kiasi cha matajiri wengi kuacha kupeleka magari ya usafiri kuhudumia eneo hili hivyo kuleta kero kubwa kwa wananchi.

Zaidi kwa miundombinu yake mibovu ikafunga kufunguka kwa uchumi zaidi kwa mikoa ya Kusini huku wananchi wakiendelea kupata adha, kero na shida kubwa sana. Kama nilivyosema, barabara hii imeahidiwa na kusubiliwa kwa kipindi kirefu sana na wananchi wa Kusini na ndio maana ukimuuliza mwananchi wa Kusini, moja ya changamoto yake kubwa basi ni barabara hii ya Mtwara hadi Masasi.

Barabara hii ya Km 210 inayoanzia Mtwara mjini kupitia Nanyamba, Tandahimba, Newala hadi Masasi, tangu uhuru barabara hiyo ilikua haijajengwa kwa kiwango cha lami hali iliyopelekea usafirisha wa korosho hasa kipindi cha masika kua ngumu sana na hivyo kuongeza gharama za tozo ya usafirishaji kwa mkulima wa korosho, lakini pia shughuli zingine za uzalishaji mali na maendeleo kwa wakazi wa wilaya hizo kuwa ngumu.

Kutoka Km 50 tu zilizojengwa kutoka Mtwara Mjini hadi eneo la Mnivata, sasa Serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanikisha kupatikana kwa mkopo nafuu kutoka Banki ya Maendeleo Afrika(AFDB) wa shilingi Bilioni 268 kwa ajili ya kumalizia Km 160 zilizobaki kwenye barabara hiyo kuanzia Mnivata Mtwara vijijini, Tandahimba, Newala hadi Masasi. Fedha hizi zitawezesha ujenzi wa barabara hiyo kujengwa kwa awamu moja huku sasa mikataba miwili ya ujenzi wa barabara hii ikisainiwa.

Miaka kwa miaka ya kero hii na kusubili kwa wakazi wa mikoa ya Kusini, hatimaye mikataba ya kuanza ujenzi wa barabara hii muhimu ya kiuchumi imeingiwa rasmi wiki hii Jumatano Juni 21, 2023 ili kuanza kujenga kabla ya kukamilika mwaka keshokutwa 2025.

Ujenzi wa barabara hii yenye Km 160 mpaka kukamilika kwake mwaka 2025 utagharimu takribani Bilioni 234.512 na Serikali imesaini mikataba miwili ya kuanza ujenzi wa barabara hii, wa kwanza ukiwa kutoka Mnivata- Mitesa Km 100 kipande kikijengwa na kampuni ya China WEE Company Limited kwa Bilioni 141.964 na mkataba wa pili wa ujenzi wa barabara hii kipande cha pili kutoka Mitesa hadi Masasi chenye Km 60 kikijengwa na kampuni ya China Communication Company Limited kwa Bilioni 92.548 na kukamilisha Jumla ya Bilioni 234.512 ya ujenzi wa barabara hii.

Tukio hilo limefanyika wiki hii Juni 21, 2023 wilayani Newala mkoani humo ambapo limeshuhudiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na viongozi wengine wa mkoa, wabunge na wananchi ambapo pamoja na mambo mengine Prof. Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaboresha mtandao wa barabara na madaraja katika ukanda wa Kusini.

Ujenzi huu unakwenda kuondoa kero ya muda mrefu ya barabara hii na itaboresha usafiri na usafirishaji wa malighafi za viwandani kama makaa ya mawe na saruji, mazao ya chakula na kilimo, mifugo, uvuvi, bidhaa za kibiashara na mazao ya misitu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mtwara pamoja na mikoa jirani ya Lindi, Ruvuma na Pwani kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Kukamilika kwa barabara hii mwaka 2025, kutazidi kuifungua Mtwara na Kusini kwa ujumla ukizingatia Serikali imeshakamilisha uboreshaji mkubwa wa Bandari ya Mtwara kwa thamani ya Bilioni 157 na imeendelea na upanuzi wa uwanja wa ndege Mtwara kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 50.

Pia, Serikali imeshafungua majadiliano ya mradi mkubwa wa kuchakata na kusindika gesi asilia wa LNG, Lindi utakaogharimu Trilioni 70 huku shughuli za uchimbaji wa gesi zikiwa zimeanza kurejea kwa kasi kubwa ukanda huo. Hatua ya ujenzi wa barabara hii, naiona Mtwara na Kusini ikienda kubadilika kabisa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Ni wakati wa wakazi wa Mtwara na Kusini kwa ujumla kuchangamkia fursa zote zitakazotoka na mradi huu akiwemo ajira na usambazaji wa bidhaa mbalimbali kwenye maeneo ya mradi na mengine mengi. Hakika, Mtwara Kuchelee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *