Na Bwanku Bwanku.
Mwishoni mwa wiki iliyopita Jumamosi Mei 20, 2023 historia imeandikwa nchini Tanzania na hatimaye ndoto ya Muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imetimia, ndoto ya kuwa na Makao Makuu rasmi Dodoma na hiyo ni baada ya Ikulu ya Chamwino kuzinduliwa rasmi.
Uzinduzi rasmi wa Ikulu yetu hii ni tukio kubwa la historia kwa Taifa letu baada ya maono haya kupangwa na Hayati Mwalimu Nyerere mwaka 1971 pamoja na Uongozi wa Chama tawala cha TANU kipindi hicho.
Baada ya michakato mbalimbali ya kuhakikisha Serikali na makazi ya Rais yanahama kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma. Hatimaye Rais wa Awamu ya 5 Hayati John Pombe Pombe alianza mchakato wa ujenzi wa Ikulu hiyo mwaka 2016 kabla ya mwaka 2020 kuweka Jiwe la Msingi la kuanza ujenzi wa Ofisi hiyo namba ya Taifa.
Hatua hii adimu na adhimu, miaka 50 toka Serikali ilipoweka azimio la kuhamisha Makao Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma sasa yametimia.
Ikulu hii mpya ya Dodoma ina utofauti mkubwa sana na ile ya Dar es Salaam. Utofauti upo katika upande wa eneo. Hili eneo la Ikulu ya Dodoma ni kubwa sana na ni Ikulu kubwa kuliko yoyote Barani Afrika na pengine Duniani kwa ujumla.
Muonekano wa Ikulu mpya ya Chamwino Dodoma inahusisha lango la kuingia katika Jengo la Ofisi ya Rais Ikulu ikiwa ina ukubwa wa ekari 8,473 ambazo ni ongezeko kutoka ekari 66 za awali. Ikulu hiyo pia ina eneo kubwa zaidi ya mara 200 ukilinganisha na ile ya Dar es Salaam (Magogoni) ambayo inaketi katika eneo la ukubwa wa Ekari 41 tu.
Lakini pia Majengo yake ni ya kisasa na yanapendeza na mandhari ni nzuri sana ikilinganishwa na hii ya Dar es Salaam.
Sasa Ikulu hii imejengwa na Watanzania wenyewe, wataalamu wetu walichora wakasanifu na kutoa pesa zetu wenyewe kujenga na hivyo kuhitimisha dhamira ya Baba wa Taifa ya kuhamishia Makao Makuu ya Dar es salaam kuyaleta Dodoma, uamuzi uliofanyika mwaka 1971 lakini leo Rais Samia Suluhu Hassan amekamilisha maono haya na kilele cha uamuzi ule ni Rais kuhamia Dodoma na kuwa na Ofisi yake Dodoma.
Ikulu hii imejengwa na Watanzania wenyewe na rasilimali za Taifa. Kwa mara ya kwanza Watanzania tumeweza kujenga yetu kwa kutumia rasilimali zetu na kutumia wataalamu wetu wa Kitanzania.
Ikulu hiyo imejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kushirikiana na Vijana wa Suma JKT ambayo ni tofauti na Ikulu ya Dar es Salaam ambayo ilijengwa na Wakoloni mwaka 1923.
Kila awamu kuna yaliyofanyika na kila uongozi ulifanya kwa namna yake toka kipindi cha Baba wa Taifa kuhamasisha moja kwa moja Ikulu, Ofisi na Makazi ya Rais kuwa Dodoma. Yapo yaliyofanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, akaja Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na katika kipindi cha Rais wa Awamu ya 4 Dkt. Jakaya Kikwete aliyeamua kujenga Chuo Kikuu kikubwa zaidi Dodoma pale Chimwaga ambapo mwanzo ndipo palipangwa kujengwa Ikulu na kuelekeza Ofisi ya Rais na Makazi ya Rais yajengwe Chamwino na Ofisi za Mawaziri zijengwe karibu na hapo pia.
Rais Kikwete kipindi hicho akatuma Watalaamu kwenda Malyasia kajifunza walivyojenga Ikulu yao.
Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli akaanza ujenzi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo anakamilisha ujenzi wa Ikulu hiyo kwa kiwango cha juu sana na cha kisasa kabisa.
Rais Samia alikuta Hayati Magufuli amefikisha asilimia 70 ya ujenzi wa Ikulu hiyo kabla ya kumalizia asilimia 30 zilizobaki na kuzinduliwa rasmi.
Hakika viongozi wote 6 walioliongoza Taifa hili mpaka sasa wanastahili pongezi kwa kila mmoja kwa wakati wake kuweka msingi wa kutimiza maono haya na zaidi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya ujenzi wa majengo mapya ya Ofisi ya Rais Ikulu Chamwino na kutimiza dhamira ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia Chama cha TANU ambacho mwaka 1973 waliweka Azimio la Dodoma kuwa Makao makuu ya Serikali.