Akiendelea na ziara yake nchi China aliyoianza jana, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi, leo asubuhi alifungua rasmi ofisi za Kampuni ya Silent Ocean maarufu Simba wa Bahari, inayojishughulisha kusafirisha mizigo kutoka China kwenda Tanzania.
Dk . Mwinyi amesema kuna biashara kubwa kati ya Tanzania na China na kwa kuifungua ofisi hiyo ushirikiano wa kibiashara utaongezeka zaidi baina ya nchi mbili hizo.
Pia amewahimiza wawekezaji wa China kuwekeza zaidi Zanzibar na angependa Kampuni za China zije Tanzania kuangalia fursa zaidi za kuwekeza.
Akimkaribisha Rais Dk. Mwinyi kufungua rasmi kampuni hiyo, Balozi wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki amesema kufunguliwa kwa Kampuni ya Silent Ocean iwe ni chachu kwa Kampuni nyingine za Tanzania kuendeleza ushirikiano wa biashara na China.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Silent Ocean Bwana Saleh Said Mohamed amesema wanahudumia kupeleka mizigo kutoka China kwenda chi zore za Afrika Mashariki na Kati kwa miaka 19 sasa.
Alibainisha uwezo wa kampuni yake kuusafirisha makasha 600 hadi 1000 kwa mwezi na kupongeza uamuzi wa Rais Samia Suluma Kassim wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Xi Jing Ping wa Jamhuri ya watu wa China kufungua njia ya ushirikiano kati ya China na Afrika.