*Aonesha ujasiri, utashi wa kisiasa
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuonesha ujasiri na utashi wa kisiasa.
Pia Rais Dkt. Samia ameboresha demokrasia pamoja na kutengeneza mazingira rafiki ya kufanya siasa nchini.
Wadau wa siasa na demokrasia ya vyama vingi waliyasema hayo juzi katika ufunguzi wa mkutano maalumu wa siku mbili, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulilenga kutoa maoni kuhusu Miswada ya Sheria za Uchaguzi na Vyama vya Siasa.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alisema Rais Dkt. Samia ameimarisha hali ya demokrasia, kuunda kikosikazi kilichotoa maoni mengi ya namna ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.
Miongoni mwa maoni yaliyotolewa ni kufanyika marekebisho katika sheria za uchaguzi na zinazoratibu shughuli za vyama vya siasa nchini.
“Kwa kuwa Rais Dkt. Samia alikuwa na utashi wa kisiasa, baada ya kupokea ripoti ya kikosikazi alizielekeza taasisi mbalimbali za serikali kuanza kufanyia kazi mapendekezo hayo, kufanya marekebisho ya sheria,” alifafanua Jaji Mutungi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, alisema Rais Dkt. Samia anastahili pongezi kwa uamuzi wa kizalendo.
Rais Dkt. Samia amejenga siasa ya nchi kwa kuzingatia mfumo wa vyama vingi kwa maridhiano, kuvumiliana.
Mhagama alivitaka vyama vya siasa nchini kwenda na Falsafa ya Rais ya R4 kwa kujenga tabia ya maridhiano na ustahimilivu katika vyama vyao ili kujenga taifa lisilo na nyufa na matabaka.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Othman Masoud Othman. aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka wadau wa mkutano huo kutekeleza falsafa ya R4 ili kuwezesha ndoto ya Rais Dkt. Samia kutimia.
Aliwataka wadau hao ambao ni viongozi wa vyama vya siasa, dini, serikali, taasisi za serikali, zisizo za serikali, kujenga misingi ya uwajibikaji katika taasisi zao ili kupunguza malalamiko ya wananchi kutokana na kulegalega kwa uwajibikaji.
“Ili kuanza na kumaliza tukiwa wamoja, nawasihi muwe jasiri wa kusikiliza zaidi ya kuongea na kujenga misingi ya kuaminiana ili tufanikiwe kuwa na Taifa lenye umoja na mshikamano,” alisema Othman.
Aliwataka wadau hao kutoa maoni yao kwa kutanguliza uzalendo mbele, kutoa maoni yenye kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.
“Tusitoe maoni ya kuvunja umoja wa kitaifa ili kuwa na sheria zitakazodumu muda mrefu, mkutano huu maalumu wa kutoa maoni kuhusu Miswada ya Sheria za Uchaguzi na vyama vya siasa, unafanyika baada ya Miswada hiyo kuwasilishwa bungeni, kusomwa kwa mara ya kwanza mwaka 2023,” aliongeza..
Miswada hiyo inatokana na mapendekezo ya kikosikazi kilichoundwa na Rais Dkt. Samia kukusanya maoni ya namna bora ya kufanya maridhiano ya kisiasa ili kujenga taifa lenye umoja na mshikamano, ripotio hiyo iliwasilishwa kwake Oktoba, 2022.