PURA yawasilisha rasimu ya CSR kwa H’shauri ya Kilwa

Na Mwandishi Wetu,Lindi

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imewasilisha rasimu ya mwongozo wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

PURA imewasilisha rasimu hiyo mwishoni mwa wiki katika kikao kilichohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sangweni, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Wakili Mary Kavula na wataalamu kutoka ofisi hizo.

Akizungunza katika kikao hicho, Sangweni amesema kuwa mwongozo huo utasaidia, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inayotekelezwa na kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini inaakisi mahitaji ya jamii hizo kulingana na vipaumbele vya jamii husika.

“Miongoni mwa sehemu kuu za mwongozo huu ni maandalizi ya mpango wa CSR utakaoshirikisha wananchi kupitia uongozi wa Serikali za mitaa. Ushirikishwaji huu utawezesha vipaumbele vya jamii lengwa kuzingatiwa hivyo kuongeza tija katika miradi hiyo,”amesema Sangweni.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wiaya ya Kilwa, Wakili Mary amesema kuwa, PURA imefanya jambo jema kuanzisha mchakato wa kuwa na mwongozo huo kwa kuwa itasaida mawazo ya walengwa kuzingatiwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi.

“Tunaishukuru sana PURA kwa kulibeba jambo hili na kujitoa kuandaa rasimu ya mwongozo huu. Ofisi ya Mkurugenzi imeupokea kwa mikono miwili na itauboresha kwa namna itakavyoona inafaa kisha kuwashirikisha wadau wengine kabla ya kuuidhinisha na kuanza kutumika. Ni matumaini yetu kuwa ifikapo Septemba 2023 mwongozo huu utakuwa tayari” ameongezea Wakili Mary.

Mwongozo huu umeandaliwa kwa kuzingatia Kifungu namba 222(4) cha Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *