Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
TANZANIA iko katika orodha ya nchi 10 barani Afrika zenye akiba kubwa ya gesi asilia, huku ikishika nafasi ya sita kutokana na akiba yake iliyothibitishwa ya futi za ujazo trilioni 57.54.
Nchi hii iko nyuma ya Nigeria yenye futi za ujazo trilioni 206.53, Algeria (159.1tcf), Senegal (120tcf), Msumbiji (100tcf), na Misri (77.2tcf).
Inaizidi Libya ambayo ina futi za ujazo trilioni 53.1, Angola (13.5tcf), Congo-Brazzaville (10.1tcf), na Guinea ya Ikweta (5tcf).
Akiba hii ya gesi asilia iliyothibitishwa Tanzania inapatikana katika maeneo yake makuu matatu ya mafuta – Kisiwa cha Songo Songo, Mnazi Bay, na Kiliwani Kaskazini – Tanzania ina jumla ya uzalishaji wa kila mwaka wa futi za ujazo bilioni 110 za gesi asilia.
Ugunduzi mwingi umepatikana katika vitalu vitatu, na futi za ujazo trilioni 22 za gesi zinapatikana kwenye kitalu namba 2, na kitalu namba 1 na 4 chenye jumla ya futi za ujazo trilioni 25.4.
Kiasi cha futi za ujazo trilioni 10 za akiba ya gesi asilia iliyothibitishwa imepatikana katika maeneo madogo kadhaa nchini, Mnazi Bay yenye futi za ujazo trilioni 5 na Kisiwa cha Songo Songo bilioni 551.
Suala la mapato ndilo muhimu sana katika uchumi huo wa rasilimali asilia zisizohuishika, hivyo, kampuni zote zilizowekeza nchini lazima ziingie mikataba yenye manufaa kwa taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority – Pura), Eng. Charles Sangweni, taasisi yenye dhamana ya kusimamia rasilimali hizi, anasema kwamba, shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi nchini zinatekelezwa kwa kupitia Mikataba ya Ugawanaji Mapato yaani Production Sharing Agreements – PSA, ambapo kampuni kubwa za mafuta duniani huingia mkataba na Serikari na kuwekeza katika nyanja hiyo.
Anasema, kwa sasa zipo kampuni zipatazo nane (8) na mikataba iliyopo ni kumi na moja (11), ambapo kati ya mikataba hiyo, mitatu ipo katika hatua ya uzalishaji na uendelezaji wa gesi asilia wakati iliyobaki bado ipo katika hatua ya utafutaji.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika mfululizo wa vikao vinavyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Eng. Sangweni alisema, kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, Kifungu cha 1, majukumu ya Pura yamegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni pamoja na Kuishauri Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana ya nishati hususan mafuta na gesi juu ya masuala yanayohusu shughuli za mkondo wa juu wa petroli, Kudhibiti na kusimamia shughuli zote za mkondo wa juu wa petroli na kusimamia miradi ya kubadili gesi kuwa katika hali ya kimiminika (Liquified Natural Gas – LNG), majukumu ambayo awali yalikuwa yakitekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) baada ya kukasimishwa na Kamishna wa Mafuta na Gesi.
Mkataba wa kugawana mapato
Kabla ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar, wakati utafiti wa kwanza wa mafuta na gesi ulipofanyika kati ya mwaka 1952 na 1964, aina ya mikataba iliyotumika baina ya taifa chini ya Serikali ya Kikoloni ya Waingereza na kampuni zilizofanya utafiti ilikuwa ya Maridhiano (Concessional Agreements).
Kwa hiyo hata kampuni za Shirika la Petroli la Uingereza (British Petroleum – BP) na Royal Dutch Shell ya Uholanzi zilipopewa sehemu ya kufanya tafiti na uchimbaji katika ukanda wa pwani pamoja na visiwa vya Mafia, Pemba na Unguja, zilitumia mikataba hii.
Mikataba hii ya CA haiwezi kuinufaisha nchi mwenyeji na yenye rasilimali zake, kwa sababu mkandarasi anamiliki mafuta yote yaliyoko ardhini na kulipa kiasi kidogo kwa serikali.
Tushukuru kwamba katika awamu hiyo ya kwanza mafuta hayakupatikana na kampuni hizo ziliondoka nchini wakati huo, vinginevyo kama zingalikuwa zimepata mafuta na gesi enzi hizo, leo hii Tanzania ingekuwa inalia kwa kukosa mapato ya kutosha.
Hata hivyo, katika awamu ya pili ya utafiti wa mafuta nchini iliyokuwa na matukio muhimu mawili – kwanza kuanzishwa kwa kampuni inayomilikiwa na serikali, TPDC, mnamo mwaka 1969, na pili ugunduzi mkubwa wa gesi katika eneo la Songo Songo, ndipo yalitokea mabadiliko.
Baada ya kuanzishwa kwa TPDC, mkataba wa kwanza wa Kugawana Mapato (PSA) ulisainiwa kati ya TPDC na AGIP (Aziende Generale Italian Petroli – kampuni ya mafuta ya Italia) kwenye eneo ambalo lilikuwa chini ya usimamizi wa kampuni za BP na Shell katika Awamu ya Kwanza.
Mnamo mwaka 1973, AGIP iliingia ubia na kampuni ya AMOCO na kuchimba visima vitano, vitatu ufukweni na viwili mbali na ufukwe – kwenye bahari kuu. Maandiko mengine yanaonyesha kwamba jumla ya visiwa sita vilichimbwa na AGIP na AMOCO huku vitatu vikiwa ufukweni na vitatu baharini.
Uchimbaji huu ulisababisha ugunduzi mkubwa kule Songo Songo mwaka 1974. Ugunduzi huo ulithibitishwa na TPDC katika programu yake ya visima vitatu iliyotekelezwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1979.
Kuanzia 1978, TPDC ikaingia katika utafiti kwenye maeneo ya ufukweni na baharini. Utafiti wa ufukweni ulijumuisha maeneo ya Ruvu, Kimbiji/Bigwa, Pemba, Mafia na Ruvuma, wakati ule wa mbali na ufukwe ulijumuisha Songo Songo, Pemba na Zanzibar.
Sheria ya Mikataba Sura ya 345 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002) ndiyo inayosimamia mikataba nchini. Mkataba (ambao kwa mtazamo mwingine wa kisheria unajulikana kama makubaliano) unatekelezwa kwa kufuata sheria, ukitanguliwa na pendekezo la mkataba (ofa), makubaliano na mwisho ahadi ya utekelezaji.
Kwa mfumo wa sheria ya Jumuiya ya Madola, mkataba una vipengele vifuatavyo: Uhalali wa kisheria, uwepo wa pande zinazoingia mkataba, utoaji wa ofa na kukubali kutekeleza ofa iliyotolewa, uzingatiaji wa sheria na wajibu wa pamoja miongoni mwa pande mbili au zaidi zinazoingia mkataba. Sheria hii inatoa mwongozo wa jumla, athari za kisheria kwa aina zote za mikataba inayoingiwa Tanzania.
TPDC imepewa mamlaka ya kisheria kuingia mkataba, kumiliki hisa, kutoa leseni na kuendesha shughuli za mafuta na gesi nchini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.
Mikataba inayoingiwa kwenye sekta ya mafuta na gesi ni makubaliano kwa mujibu wa Kifungu Namba 14 cha Sheria ya Petroli (Utafiti na Uzalishaji) ya mwaka 1980. Makubaliano hayo yanasimamiwa na Kifungu Namba 42 cha sheria hiyo hiyo ambacho vipengele vyake vinasimamia masharti ya leseni ya uendelezaji katika sekta ya mafuta na gesi.
Tangu TPDC ilipoanzishwa, mikataba ambayo imekuwa ikiingiwa na wakandarasi ni ya Kuchangia Uzalishaji (PSA). Makubaliano hayo kwenye sekta ya mafuta na gesi uliandaliwa na TPDC kama mwongozo wa makubaliano ya kimkataba kwa ajili ya utafiti na uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi nchini.
Kwa hakika, ni mwongozo wa namna hii unaosimamia makubaliano/mikataba kwenye sekta ya mafuta na gesi kwenye nchi nyingi zinazoendelea.
PSA haimpi mkandarasi umiliki wa mafuta yaliyoko ardhini; umiliki wa rasilimali unakuwa kwa dola.
Katika hali hii mkataba huo unaandikwa kwa mkandarasi kuweza kuchimba mafuta ya serikali kwa niaba ya serikali.
Makubaliano ya kuchangia uzalishaji yalianza kutumika Indonesia mwaka 1966, wakati serikali ilipoamua kuhodhi umiliki wa mafuta ardhini, na hivyo kampuni ya kimataifa ilikuwa na haki ya kufanya utafiti wa mafuta lakini ikapata haki ya kumiliki na kuyauza (au kiasi fulani cha mafuta hayo) mara yanapochimbwa.
Kule Indonesia, kwa mujibu wa jarida la Revenue Watch, sasa National Resources Governance Institute, mtindo wa kutoa leseni ya maridhiano (CA) uliondolewa kwa kuchukuliwa kama ni sera ya kibeberu na ya wakati wa ukoloni na mfumo wa makubaliano ya kuchangia uzalishaji ulianzishwa katika muktadha wa harakati za “utaifa katika rasilimali” miongoni mwa nchi zizalishazo mafuta duniani kote.
Tangu wakati huo, makubaliano ya kuchangia uzalishaji yameenea duniani na sasa ni mfumo wa kawaida wa kufanya biashara, hususan katika maeneo ya Asia ya Kati na Caucasus.
Katika mfumo huu, kampuni za mafuta zinapewa haki ya kurudisha gharama za uwekezaji na matumizi mengine na zinapata mapato ya mwaka yajulikanayo kama – “gharama za mafuta” (Oil Costs). Baada ya kutoa gharama za uwekezaji na matumizi mengine, kiasi kinachobaki kijulikanacho kama – “faida ya mafuta” (oil interest) – kinagawanywa kwa kufuata mgawanyo wa asilimia uliokubalika katika mkataba.
Faida na hasara zake
Katika mfumo huu wa PSA ambao Tanzania inautumia, gharama zote na tahadhari za uendeshaji zinakuwa juu ya kampuni ya kimataifa ya mafuta katika mpangilio wa makubaliano ya kuchangia gharama, na serikali mwenyeji inakuwa na faida ya ziada kwamba inakuwa na faida yoyote itakayopatikana bila ya kufanya uwekezaji, isipokuwa ikikubali kufanya hivyo.
Mtaji mkubwa wa serikali ni eneo pamoja na rasilimali zilizomo chini yake, lakini pia hapa inaruhusiwa kupeleka wataalamu wake kuwa miongoni mwa watumishi na inaweza kufuatilia kwa karibu uzalishaji na masoko yalivyo kuliko ilivyo kwenye Mkataba wa Maridhiano (CA).
Hasara ya makubaliano ya kuchangia uzalishaji kwa serikali mwenyeji ni kwamba, kampuni inaweka gharama kubwa za ziada kwa makubaliano ya kitaalam, na serikali lazima ipate wataalamu wa kiufundi, kimazingira, kifedha, kibiashara na kisheria.
Hii inawezekana zaidi katika baadhi ya nchi zenye utajiri wa mafuta zaidi kuliko nyingine, kwa sababu serikali inatakiwa kuandaa mazingira ya kuwasomesha wataalamu wake ambao watakuwemo kwenye utendaji.
Aina nyingine za Mikataba
Ukiacha Mkataba wa Uzalishaji wa Pamoja au Mkataba wa Ugawanaji Mapato (PSA), kuna aina nyingine za mikataba katika sekta ya mafuta na gesi. Hata hivyo, kitabu cha ‘Oil Contracts: How to read and understand them’ kinaeleza bayana kwamba ni nadra kukuta mkataba ambao unaendana kikamilifu na aina hizo.
Katika uhalisia, mikataba mingi ni zao la mchanganyiko wa vipengele vilivyomo ndani ya kila moja ya mikataba hiyo.
Mikataba yote ya mafuta na gesi ni lazima izingatie masuala makuu mawili, kwa mujibu wa taasisi iitwayo Revenue Watch Institute: jinsi faida, ambayo mara nyingi huitwa “kodi za pango”, inavyogawanywa kati ya serikali na kampuni zinazohusika, na jinsi gharama zinavyopaswa kushughulikiwa.
Mkataba wa Maridhiano
Mkataba wa Maridhiano (Concessional Agreement) ni utaratibu wa zamani kabisa wa mikataba ya mafuta, ukiwa umeanzishwa mara ya kwanza wakati wa mfumuko wa mafuta nchini Marekani miaka ya 1800.
Kwa mujibu wa National Resource Governance Institute, wakati mfumo wa maridhiano ulipoanzishwa duniani kote, uliegemea upande mmoja zaidi wa kampuni kuliko nchi nyingi zenye rasilimali leo hii ambazo wakati huo zilikuwa tegemezi, makoloni, au nchi zilizowekwa chini ya udhamini wa dola nyingine au tawala nyingine.
Maridhiano yanafuata mfumo wa umiliki wa ardhi wa Marekani, ambapo mmiliki wa ardhi anamiliki rasilimali zote zilizomo ardhini katika eneo analomiliki na kinadharia rasilimali zote zilizomo juu yake.
Maridhiano yanatoa sehemu ya ardhi, na rasilimali zilizo chini ya ardhi zikijumuishwa, kwa kampuni, ili kama kampuni itagundua mafuta kwenye kipande cha ardhi, inamiliki mafuta hayo.
Katika mikataba ya maridhiano mkandarasi pia ana haki zilizotengwa kuchunguza na kutafuta mafuta katika eneo hilo.
Wakati faida kwa kampuni inakuja moja kwa moja katika muundo wa umiliki wa mafuta au gesi iliyopatikana, serikali iliyotoa maridhiano inafaidika katika mfumo wa kodi na malipo mengine ya uzalishaji katika mafuta na gesi iliyozalishwa.
Kampuni hushindana kwa kupandishiana dau, pamoja na kutiliana saini bonasi, kwa ajili ya leseni ya haki hizi.
Aina hii ya makubaliano ni ya kawaida duniani kote na inatumika Kuwait, Sudan, Angola na Ecuador, miongoni mwa nchi nyingine.
Faida na hasara zake
Kwa serikali, mikataba ya maridhiano ina faida ya moja kwa moja zaidi kuliko makubaliano ya aina nyingine, na kiwango cha msaada wa kifani na kitaaluma unaotakiwa si wa hali ya juu kama inavyohitajika kujadili na kufikia makubaliano kwenye mkataba wa ubia au makubaliano ya kuchangia uzalishaji.
Serikali inakuwa haina haja hata ya kutafuta wataalamu ama kuwasomesha wataalamu wake, kwa sababu kampuni inayowekeza ndiyo yenye jukumu la kuwatafuta wataalamu hao mahali kokote.
Kampuni husika pia ndiyo inayotoa mtaji pamoja na zana nyingine zinazotakiwa, hivyo serikali haina haja ya kuingia gharama yoyote.
Pia serikali mwenyeji inapata malipo yanayotolewa na mkandarasi bila ya kujali kwamba mafuta yamepatikana au uzalishaji wa kibiashara unafanyika.
Tahadhari zote za kifedha za uendelezaji, ikiwa ni pamoja na gharama za uchunguzi (utafiti) zinachukuliwa na mkandarasi.
Hasara kuu kwa serikali ni kwamba, kampuni inayoingia katika uzabuni wa mkataba ina kawaida ya kuchukua tahadhari katika zabuni zao.
Kama mafuta na gesi hayakuhakikishwa kunakuwa hakuna uhakika kwamba gharama za kampuni zitalipwa, kwa hiyo serikali inaweza ikakosa kiasi kikubwa cha kipato kilichotarajiwa.
Wakati mwingine inakuwa vigumu kufuatilia na kujua kiundani hasa uzalishaji uliofanyika na kampuni inaweza kudanganya kwa sababu serikali haina wataalamu wabobezi kwenye eneo hilo ambao wanaweza kusaidia ufuatiliaji.
Mikataba ya Huduma
Mkataba wa Huduma (Service Agrement) hautoi haki ya kumiliki mafuta ardhini. Tofauti na makubaliano ya kuchangia uzalishaji, katika mkataba wa huduma kampuni ya kimataifa haipati kabisa umiliki, au haki ya kumiliki mafuta yazalishwayo.
Katika hali hii kampuni inalipwa malipo kwa huduma yake katika kuchimba mafuta ya serikali.
Hii inawezekana kwa nchi zenye utajiri wa kutosha, ambazo zinaweza kuilipa kampuni fedha hata kabla mafuta ama gesi haijapatikana.
Ni vigumu kwa nchi zinazoendelea zenye rasilimali kama Tanzania, ambazo hata bajeti zake zimekuwa zikishindwa kufikiwa kila mwaka, huku wananchi wakitegemea utajiri mara wanapoambiwa kwamba kumegunduliwa mafuta ama gesi nchini mwao bila kutathmini gharama zilizopo.
Mikataba ya Ubia
Mpangilio mwingine, ambao mara nyingine huchukuliwa kama ni aina ya nne ya mipangilio ya kimkataba, ni Ubia (Joint Venture), ambao unahusisha dola kupitia kampuni ya taifa ya mafuta, kuingia ubia na kampuni au kikundi cha kampuni za mafuta.
Ubia wenyewe katika hali hii unapewa haki ya kutafiti, kuendeleza, kuzalisha na kuuza mafuta.
Kwa sababu hakuna mfumo wa ubia uliokubalika kwa pamoja, mikataba ya ubia haitumiki sana kama mikataba ya msingi kati ya kampuni ya mafuta na serikali mwenyeji.
Ubia unazitaka serikali wenyeji na kampuni kufanya shughuli kwa pamoja, na hivyo kama wawili hao wakishindwa kufanya kazi pamoja, makubaliano yanaweza kuwa na usumbufu na mizozo hutokea mara kwa mara.
Faida na hasara zake
Kwa serikali, faida pekee ya ubia ni kwamba haiwi peke yake katika kutoa uamuzi kuhusu masuala ya mafuta na gesi, na inaweza kutegemea wataalamu na sehemu ya ubia wa kampuni kubwa ya kimataifa.
Moja ya hasara kubwa ya mikataba ya ubia ni kwamba, inahitaji majadiliano marefu zaidi na inahitaji ushauri mkubwa zaidi wa kisheria na kitaalamu kwa sababu miundo yake inakuwa na utata sana.
Zaidi ya hayo, gharama pia lazima zichangiwe na pande zote mbili, ikimaanisha kwamba serikali mwenyeji ni mshiriki wa moja kwa moja na mwenye kuwajibika katika uchimbaji wa rasilimali, na uwajibikaji pia unakuja na suala la kuhusika na masuala mengine, ikiwa ni pamoja na suala la uharibifu wa mazingira.
Kwa maana hiyo, mikataba ya PSA ambayo Tanzania inaitumia ina tija kubwa sana kwa taifa na ikiwa Pura itasimamia kwa umakini hasa katika uzalishaji, basi Serikali inaweza kunufaika na mapato makubwa ya mafuta na gesi.
0629-299688