Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, limemkamata na kumhifadhi mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Igunga, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Athumani Francis Msabila.
Mkurugenzi huyo alikamatwa Novemba 5, 2023 mchana baada ya kurejea kutoka mkoani Dodoma ambako alienda kikazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao alithibitisha kukamatwa kwa Mkurugenzi huyo.
“Ni kweli Mkurugenzi huyo tunamshikilia akisubiriwa kupelekwa mkoani Kigoma alikotokea kwani ndiko ana kesi,” alisema.
Hata hivyo, Abwao hakuweza kutaja tuhuma wala kesi inayomkabili Mkurugenzi ambaye aliwahi kuhudumu kwa wadhifa huo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa aliwasimamisha kazi watumishi 4 kutokana na makosa mbalimbali ya kiutumishi.
Kati ya watumishi hao, Msabila alikuwa ni miongoni mwao ambapo alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.
Pia Mchengerwa alimuagiza Katibu Mkuu kuwasimamisha kazi watumishi wawili wa Ofisi ya Rais Tamisemi, Aidan Mpozi na Tumsifu Kachira kuanzia juzi.
Hatua hiyo imefika baada ya kupokea taarifa ya timu ya uchunguzi katika Halamshauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kuhusu mtandao wa upotevu wa fedha za umma kupitia mfumo wa utoaji fedha kutoka hazina kwenda Mamlaka za Serikali za mitaa.
“Kamati imethibitisha pasipo shaka kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Msabila na maafisa tajwa wa Ofisi ya Rais Tamisemi wamehusika na upotevu wa fedha za umma,” alisema.
Wakati huo huo, Mchengerwa alimuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kumsimamisha kazi mwekahazina wa Halmashauri hiyo, Kabwenge Nteminyanda kwa tuhuma za ubadhirifu wakati akifanya kazi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko na Uvinza mkoani Kigoma.
Mchengerwa aliwaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanaingia kwenye vikao vya kamati ya fedha vya Halmashauri bila kukaimisha na ambaye hatoingia vikao vya Kamati mara mbili mfululizo atachukuliwa hatua za kinidhamu.